Home Mchanganyiko ZIARA YA DPP SINGIDA YAWAWEKA HURU WASHTAKIWA 99

ZIARA YA DPP SINGIDA YAWAWEKA HURU WASHTAKIWA 99

0

 Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk Rehema Nchimbi (katikati, na wajumbe wa Jukwaa la Haki Jinai mkoa wa Singida, muda mfupi baada ya mkuu wa mkoa kulizindua rasmi.
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Biswalo Mganga (kushoto) akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk Rehema Nchimbi na Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. Angelina Lutambi muda mfupi baada ya hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Haki Jinai ngazi ya Mkoa.
 
Na Godwin Myovela, Singida
 
IDADI ya waliofutiwa Mashtaka na Ofisi ya Mashtaka ya Taifa kwa makosa mbalimbali kwenye magereza ya wilaya za Manyoni na Iramba mkoani hapa sasa imefikia 99.
 
Watuhumiwa 85 walioachiwa kwenye gereza la Manyoni ni wale wenye makosa yanayohusiana na kesi za uhujumu uchumi, udanganyifu na rushwa, huku 14 wa gereza la Iramba Kiomboi ni wale wa makosa mchanganyiko.
 
Akiwa kwenye ziara ya kutembelea wadau wa ‘Haki Jinai’, mkoani hapa, hivi karibuni, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, alisema baada ya kutembelea magereza husika, kuangalia mwenendo mzima wa upelelezi na wapelelezaji, na kupata fursa ya kusikiliza mahabusu mbalimbali na kujiridhisha ndipo alipoamua kufuta kesi hizo.
 
“Nimefuta kwa wale ambao nimejiridhisha kwamba kesi zao hazina sababu ya kukaa gerezani, na hawa wengine wa uhujumi uchumi ni ambao waliingia kwenye hifadhi ya Rungwa wakiwa na mitambo na kuchimba madini, baada ya kukiri mbele yangu kwamba ni kweli wamefanya hayo makosa na ukiangalia gereza limejaa nikaona na wenyewe niwapatie nafasi ya mwisho,” alisema Mganga.
 
Alisema, lengo hasa la ziara yake kwa wadau ilikuwa ni kufanya ukaguzi wa kesi zinazohusiana na rushwa na udanganyifu, kukagua kama kesi hizo zinaendeshwa na kupepelezwa ipasavyo, na kama kuna tija na matokeo tarajiwa, lakini pia kama kuna changamoto.
 
Aidha, katika hatua nyingine, DPP alishuhudia uzinduzi wa Jukwaa la Haki Jinai ngazi ya Mkoa, ambalo kwa mujibu wa sheria jukwaa hilo litakuwa na jukumu la kuweka mipango na stratejia zote za kuhakikisha linakabiliana na ikiwezekana kufuta kabisa uhalifu ndani ya mkoa.
 
“Jukwaa hili majukumu yake yapo kisheria, ambapo pamoja na mambo mengine ni wajumbe wake kuweka mazingira ya kuhakikisha shughuli za kijinai ndani ya mkoa zinakwenda vizuri… kuweka stratejia, mipango na mikakati ya pamoja na kwa umoja, na pale wanapokwama walete mapendekezo yao kwenye Jukwaa la Jinai ngazi ya taifa” alisema Mganga.
 
DPP, akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi ili afungue rasmi Jukwaa hilo, alisema mathalani kama kwenye mkoa husika wajumbe wakabaini inapofika kipindi fulani cha mwaka aina fulani ya uhalifu huwa inaongezeka, lakini wao wanashindwa jinsi ya kutatua changamoto hiyo, basi wafikishe mapendekezo kwenye Jukwaa ngazi ya taifa.
 
Pia kupitia chombo hicho, kama kuna uhitaji wa mabadiliko ya sheria au suala lolote linalohitaji mabadiliko ya sheria linapaswa kusemwa, huku akisisitiza kwamba ni chombo muhimu sana ambacho kama kikitumika vizuri kinakwenda kupunguza hata mlundikano wa mahabusu magerezani.
 
“Mwanzoni  hapakuwa na kifungu cha namna hii kinachowalazimisha wajumbe wa jukwaa hili wakae wote kwa pamoja tena bila kutuma mwakilishi ili kuweka mikakati ya kuhakikisha amani na usalama ndani ya mkoa vinaendelea kuwepo, lakini sasa chombo hiki na shughuli zake vipo kisheria,” alisema na kuongeza:
 
“Nitumie fursa hii nikiwa hapa Singida kuwataka Wakuu wa Mikoa kufanya uzinduzi rasmi wa Jukwaa hili kila mkoa, na nitashangaa kama nitaona uhalifu unaongezeka na hatupati stratejia yoyote ya jinsi ya kukabiliana na uhalifu huo ndani ya mkoa husika,” alisema Mganga.
 
DPP alisema uanzishwaji kisheria wa majukwaa hayo ya wadau ndani ya Mkoa na Wilaya ni kuhakikisha haki, amani na usalama vinaendelea kuwepo huku akisisitiza kwamba ili kuyafikia hayo yote ni lazima ofisi yake ifanye kazi na wadau.
 
Mwaka 2008 wakati sheria ya Taifa ya Mashtaka inatungwa kulianzishwa Jukwaa la Haki Jinai Taifa ambalo mwenyekiti wake ni Mkurugenzi wa Mashtaka, Katibu wake ni Mkurugenzi wa Upelelezina viongozi wengine wanaotajwa kwa mujibu wa sheria.
 
Hata hivyo, mwaka 2018 wakati Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inaundwa upya, pamoja na mambo mengine ikabainika kuna changamoto kwenye maeneo fulani , huko juu viongozi hukutana mara kwa mara lakini kwenye ngazi za mikoa na wilaya ambako ndipo kesi zilipo viongozi wake wakati mwingine hawakai pamoja.
 
“Kwahiyo sheria ikabadilishwa ikaweka kifungu ambacho sasa kinataka uwepo wa jukwaa la haki jinai wilaya pamoja na mkoa,” alisema Mganga.