Home Mchanganyiko KIBAJAJI ACHANGISHA HARAMBEE UJENZI WA NYUMBA UVCCM WILAYA YA CHAMWINO

KIBAJAJI ACHANGISHA HARAMBEE UJENZI WA NYUMBA UVCCM WILAYA YA CHAMWINO

0

Mbunge wa Jimbo la Mtera, ambaye pia ni MNEC,Mhe. Livingston Lusinde ‘Kibajaji’ akiwa ameshika pesa zilizochangishishwa katika harambee hiyo. Kulia kwake ni Katibi wa UVCCM Wilaya ya Chamwino, Peter Dafi na wengine ni wajumbe wa chama hicho

Mbunge wa Jimbo la Mtera, ambaye pia ni MNEC,Mhe. Livingston Lusinde ‘Kibajaji’ akisisitiza kwa Katibi wa UVCCM Wilaya ya Chamwino, Peter Dafi wakati akihutubia kwenye shughul ya Harambee hiyo.

……………………………………………………………………………………………….

NA MWANDISHI WETU, CHAMWINO.

MBUNGE wa Jimbo la Mtera, ambaye pia ni (MNEC), Mhe. Livingston Lusinde ‘Kibajaji’ ameongoza zoezi la Harambee ya ujenzi wa nyumba ya Katibu Mtendaji Wilaya Chamwino shughuli iliyoratibiwa na kuongozwa na UVCCM Wilaya ya Chamwino.

Kibajaji ambaye alikuwa mgeni rasmi wa Shughuli hiyo alifanikiwa kukusanya kiasi cha pesa taslim Tsh Millioni 2,195,000/= huku ahadi mbalimbali zikitolewa.

Miongoni mwa ahadi hizo ni pamoja na; Nondo pc 23, Kokoto trip =5, Misumari kg 12, Cement mifuko 280, Bati bundle 10, Mchanga tripu 13 na vingine vingi.

Katika tukio hilo ambalo limefanyika kwenye jengo la CCM kijiji cha Chamwino, Kibajaji amewaasa Viongozi wa UVCCM Chamwino kuhakikisha pesa hizo zinatumika kama iliyokusudiwa huku vijana wakitakiwa kukisaidia chama.

“Pesa hizi na zitakazokuwa zikipatikana zitumike kwa jambo lililokusudiwa.
Ikitokea pesa hizo zikaliwa zitawatokea puani” Alisema Kibajaji.

Mbali na hilo amewakumbusha Vijana wajibu wao kwenye kuhakikisha wanakisaidia Chama na Taifa kwa Ujumla.

“Nitafurahi sana kama sitasikia Vijana wanaomba Pesa za mafundi wa ujenzi kwani Vijana mafundi ndio hao hao Vijana wa UVCCM.

“Vijana wajitolee kujenga ili pesa zinazopatikana zitumike kununua vifaa na sio nguvu kazi ya ujenzi wa jengo lao Vijana na Chamwino hakuna Vijana wapinzani sasa iweje tutumie pesa kumlipa fundi?” Alisema Kibajaji.

“Vijana lazima mjue thamani yenu kwa Kujituma na Kujitafutia vyakwenu ili kuondoa tabia omba omba na kusababisha kubeba Wagombea hasa nyakati kama hizi tunapoelekea kwenye chaguzi kuu.” alimalizia Kibajaji.

Aidha, Mhe. Kibajaji alisema kuwa miradi ya Umoja wa Vijana itawezesha Vijana kuweza kujitegemea hivyo waendelee kukiamini chama.

Kwa upande wake Katibu wa UVCCM Wilaya ya Chamwino, Peter Dafi ameahidi kutekeleza na kuyafanyia kazi yale yote walioagizwa na mgeni rasmi huyo.

Zoezi hilo la kujenga nyumba za Watendaji wa Wilaya na Mkoa kwa nchi nzima ni agizo la Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM, Kheri James ilikuimalisha chama na taasisi hiyo ya Vijana kufanya kazi kwa weredi.