Home Mchanganyiko KAMOGA AMSHUKURU RAIS MAGUFULI KWA KUWAPA FEDHA ZA MIRADI MBULU

KAMOGA AMSHUKURU RAIS MAGUFULI KWA KUWAPA FEDHA ZA MIRADI MBULU

0

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga (katikati) akiwa na wakandarasi wa kampuni ya Mzinga wanaojenga jengo la utawala la Halmashauri hiyo jana ambapo limefikia asilimia 70 ya ujenzi kwenye Kata ya Dongobesh litakalogharimu shilingi bilioni 4.7.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga akikagua jengo la utawala la Halmashauri ambapo limefikia asilimia 70 ya ujenzi kwenye Kata ya Dongobesh.

…………………………………………………………………………………………

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Stanley Kamoga amemshukuru Rais John Magufuli kwa kuwapatia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya na jengo la utawala la Halmashauri hiyo.

Kamoga aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu mapya ya halmashauri ya wilaya hiyo yaliyopo kata ya Dongobesh.

Alisema wanamshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia fedha za jengo jipya la makao makuu mapya ya halmashauri hiyo ambalo limefikia asilimia 70 ya ujenzi wake.

Alisema Rais Magufuli aliwapatia sh4.7 bilioni za ujenzi wa jengo la utawala wa halmashauri hiyo ambalo linajengwa na wanajeshi kupitia kampuni ya Mzinga.

“Tunamshukuru Rais Magufuli kwani tulipata fedha hizo kwani ujenzi ulianza April 2019 na tunatarajia kukamilisha April mwaka huu na kuanza kutumika,” alisema Kamoga.

Alisema pia walipatiwa sh1.5 bilioni ya ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya ambapo upo katika hatua ya mwisho kwani usimamizi ulikuwa mzuri.

Alisema pia kituo cha afya Dongobesh kimeboreshwa baada ya kupatiwa sh4 milioni na kujengwa jengo la mama na mtoto ambalo ni maalum kwa kujifungua.

“Pamoja na hayo tunamshukuru Rais Magufuli kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni alipokuwa anagombea urais mwaka 2015 ya kuweka lami Dongobesh na Haydom,” alisema Kamoga.

Alisema kwenye kata ya Dongobesh tayari Mita 600 za lami tayari na mchakato wa kilomita 1.4 baada ya wiki moja ujenzi utaanza.