Home Mchanganyiko Viongozi wa umma epukeni kukili Ahadi ya Uadilifu kama kasuku: Nsekela.

Viongozi wa umma epukeni kukili Ahadi ya Uadilifu kama kasuku: Nsekela.

0

Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela akionyesha fomu ya Ahadii ya Uadilifu kwa viongozi wa mkoa wa Mbeya (Hawapo pichani) walioshiriki mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma hivi karibuni katika ukumbi wa Benjamini Mkapa jijini Mbeya.

Waheshimiwa Majaji wa Mkoa wa Mbeya walioshiriki mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma wakimsikiliza Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela, Kamishna wa Maadili (Hayuko pichani) hivi karibuni katika ukumbi wa Benjamini Mkapa jijini Mbeya.

Baadhi ya viongozi wa umma wa mkoa wa Mbeya walioshiriki mafunzo ya maadili wakimsikiliza Mhe. Jaji (Mst) Harold Nsekela (hayuko pichani) katika ukumbi wa Benjamini Mkapa jijini Mbeya.

***************************

Viongozi wa umma waliokula kiapo cha Ahadi ya Uadilifu wametakiwa kutokili ahadi hiyo kama kasuku bali waishi kama walivyoahidi na kuepukana na vitendo vya rushwa katika utumishi wao vinginevyo hakuna sababu ya kula kiapo hicho.

 

Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela, Kamishna wa Maadili ametoa wito huo hivi karibuni jijini Mbeya wakati wa mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma wa
mkoa huo. Mafunzo hayoyalifanyika katika ukumbi wa Benjamini Mkapa jijini humo, na kuandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa
kujumuisha viongozi wa umma wa mkoa wa Mbeya.

 

“Kukili Ahadi hii tu haitoshi, tunapokili ahadi hii tusikili kama kasuku. Ahadi hii ya Uadilifu iingie moyoni mwetu na tuishi kama tulivyokili kwasababu yote yaliyomo kwenye ahadi hii chimbuko lake ni Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977, kama hatuyaishi, hatuna sababu ya kukili,” alisema.

 

Wakati wa mafunzo hayo ya Maadili, Kamishna Nsekela alinukuu Ibara ya 132 (5) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inayozungumzia misingi
ya Maadili ya Viongozi wa umma. Ibara hiyo inasema, “itapiga marufuku mienendo na tabia inayopelekea kiongozi kuonekana hana uadilifu, anapendelea au
si muadilifu au inaelekea kukuza au kuchochea rushwa katika shughuli za umma au inahatarisha maslahi au ustawi wa jamii.”

 

“Viongozi muelewe kwamba jambo hili halikubuniwa , msingi wa Ahadi ya Uadilifu ni wakikatiba. Naomba viongozi nyote mlio apishwa ahadi hii tuishi kama
tulivyokili sio tukili na tukisha mpa Rais kisogo tuna kula rushwa,” alisema.

 

Katika hatua nyingine Jaji Nsekela amesema kuwa, baada ya kanuni za kudhibiti Mgongano wa Maslahi kutangazwa katika gazeti la Serikali, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma itaanza kufuatilia Viongozi wa Umma wanaojihusisha na Mgongano wa Maslahi kwa kutumia sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995.

 

“Zamani hatukuwa na Kanuni za utekelezaji wa suala la Mgongano wa Maslahi, lakini sasa hivi tunazo, tutazifuatilia kisheria kudhibiti mgongano wa maslahi
miongoni mwa viongozi wa umma, hakuna ubabaishaji tena,” alisema.

 

Mgongano wa maslahi utokea pale kiongozi wa umma anapozingatia maslahi yake binafsi katika utoaji wa maamuzi badala ya kuzingatia maslahi ya umma.

 

Kanuni za kudhibiti Mgongano wa Maslahi kwa Viongozi wa Umma zimetolewa katika Tangazo la Serikali GN 113 la 2020 tarehe 14 Februari, 2020.

 

Kwa mujibu wa Jaji Nsekela, suala la Mgongano wa Maslahi ni la kisheria na limekuwepo tangu mwaka 1995 Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilipotungwa. Hata hivyo, tangu wakati huo hakukuwepo kanuni za utekelezaji wa Mgongano wa Maslahi.

 

“Suala la Mgongano wa Maslahi sio jepesi, linatuletea viongozi matatizo mengi katika utekelezaji wa majukumu yetu. Kila kiongozi anapofanya uamuzi anatakiwa
kuzingatia maslahi ya umma sio maslahi yake binafsi,” alisema.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Albert Chalamila Mkuu wa Mkoa wa Mbeya aliwataka viongozi wa umma kuepuka mgongano wa maslahi kwa kukuza uchumi wa Taifa badala ya kukuza uchumi wao binafsi.

 

Mhe. Chalamila alisema, “Kila mmoja wetu hapa ajiulize anatamani kuwa kioo cha jamii kwa namna ipi, tajiri wa namma ipi, pesa ni sabuni ya roho, zana ya maadili
ni nzuri na kila mmoja wetu ajipime kama ana mali zisizokuwa na kiasi alizozipata kutokana na mgongano wa maslahi.”