Home Mchanganyiko DKT NCHIMBI AWATWISHA MZIGO TBS NA SIDO

DKT NCHIMBI AWATWISHA MZIGO TBS NA SIDO

0

 

 Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dkt. Rehema Nchimbi
Na John Mapepele
Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dkt. Rehema Nchimbi amelielekeza Shirika
la  Viwango nchini (TBS) na
Shirika la Viwanda Vidogo nchini (SIDO) kuanzisha mara moja  operesheni maalum ya  kuwatafuta wamiliki wa viwanda  na wazalishaji wakubwa wa mafuta ya alizeti katika Mkoa wa Singida.
Lengo kubwa ni kukagua viwango vya  mafuta
hayo na kuwaelimisha  ili  kuhakikisha ubora wa mafuta hayo yaweze
kuingia kwenye  masoko ya
kimataifa hatimaye kuinua  uchumi wa  mwananchi mmoja mmoja  na taifa kwa ujumla.
Dkt. Nchimbi ametoa
maelekezo hayo kwenye mafunzo maalum ya kudhibiti ubora wa bidhaa yaliyotolewa
na TBS kwa wajasiliamali  wa zao la
alizeti  na asali yaliyofanyika katika
ukumbi wa VETA  hivi karibuni.
Ambapo
pia amelipongeza TBS na SIDO kwa kubuni utaratibu wa kutoa mafunzo  hayo
nchi nzima  huku akiwataka kwenda
mbali zaidi  kwa kuwa karibu na  kufanya tathmini ya mara kwa mara  kwa mafunzo wanayoyatoa kwa wajasiliamali na
kuchukua hatua stahiki.

Amesema  katika dunia ya sasa suala la kuzingatia
viwango katika  bidhaa zote hususan   bidhaa za vyakula kwa binadamu la lazima na
la kisheria  hivyo  mafunzo
yanayotolewa na TBS na SIDO lazima
yawaguse wahusika ili mafunzo hayo yawe na tija  badala ya kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa
mazoea.
“Inapofika  suala la
viwango  na ubora wa mafuta
yetu  ya alizeti kwenye Mkoa wetu wa
Singida linakuwa siyo suala la kubembelezana tena ili kinachozalishwa  kufika salama kwa mlaji” alisisitiza Mkuu wa
Mkoa
Amewataka  wazalishaji na wamiliki wa viwanda vya
alizeti na asali kuondokana  na fikra
potofu za  kuona kuwa TBS ni adui badala
yake kujenga ushirikiano wa karibu  ili kuhakikisha
kuwa wananufaika  na huduma zinazotolewa
na  hatimaye kuboresha  bidhaa wanazozizalisha  na kupata ushindani kwenye masoko ya ndani na
nje ya nchi.
Aidha  amesema TBS ni daraja   baina ya mzalishaji, soko na mlaji  na kuwataka
wajasilia mali  kuwa  karibu ili kutengeneza fursa za biashara zao.
Amesema  tafiti nyingi zimeonesha kuwa  magonjwa mengi ya binadamu yanatokana  na
vyakula   tunavyokula hivyo
udhibiti wa ubora  ni jambo lisilokwepeka  kwa sasa ili kunusuru vifo ambavyo vingeweza
kuepukika.
Akitolea mfano katika
kitabu kitakatifu  cha Mungu  cha Biblia amesema  maandiko
yanasema  hata kabla  ya kumuumba binabamu  Mwenyezi Mungu  alimtengenezea   chakula na pia  kinasisitiza kuwa mtu asiyefanya kazi na
asile hivyo ni muhimu kuangalia chakula tunachokula  kwa afya ya mlaji.
Aliongeza kuwa  vitabu vyote vitakatifu  hakuna sehemu yoyote vinaposema mfanyabiashara
awe  muongo akawataka  wasifanye
mchezo  na maisha ya  binadamu
kwa kukiuka  viwango  ili kupata
faida  ambapo alisisitiza  kwamba baada ya masomo hayo wajasiliamali
wote watoke na viapo  vya moyoni vya
kutenda haki na kuwa na hofu ya Mungu katika
utekelezaji wa biashara zao.
Amesema  Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na
Rais John Pombe Magufuli imedhamilia kwenda kwenye safari ya uchumi wa kati wa
viwanda  kwa kuwashirikisha  wajasiliamali wote hapa nchini  hivyo kila mjasiliamali ana haki sawa  kwenye
safari  hii ambayo imeshatoa
mafanikio makubwa.
 Naye
Mwalimu Hamis Sudi ambaye  ni
Kaimu Mkurugenzi wa udhibiti ubora amemshukuru Mkuu wa Mkoa  na kumhakikishia  usimamizi shirikishi kwenye  udhibiti wa ubora kwenye  bidhaa zinazotokana na zao la alizeti katika
mkoa wa Singida na kwamba operesheni maalum itafanyika ili kuwafikia  watengenezaji na wamiliki wa viwanda vya
alizeti badala ya kutoa  mafunzo kwa
wajasiliamali waliofika kuhudhulia mafunzo hayo.
“Mkuu wa Mkoa naomba  nikuhakikishie  hatujafika hapa Singida kupoteza  fedha na muda wa Serikali bali  kuwafikia wadau wetu wote ambao tutawafikia
na tutaleta taarifa ya  utekelezaji
katika ofisi yako” aliongeza Sudi.
Mkuu wa Idara ya Uhusiano
wa TBS, Rhoida Andusamile amesema
Shirika lilianzishwa kwa
Sheria ya Bunge – Sheria ya Viwango Na.3 ya mwaka 1975,iliyofanyiwa marekebisho
na Sheria Na. 1 ya mwaka 1977.Sheria
hiyo ilifutwa na nafasi yake kuchukuliwa na Sheria ya Viwango Na.2 ya
mwaka 2009 ambayo ililipa Shirika uwezo mkubwa zaidi wa kutekeleza majukumu
yake
.
Ameongeza
kuwa Shirika lina majukumu mengi kama yalivyoainisha katika Sheria ya Viwango
Na.2 ya mwaka 2009, lakini majukumu makuu manne.
Aliyataja mambo hayo ni kuweka
viwango vya kitaifa vya bidhaa,huduma na mifumo ya usimamizi wa ubora katika
sekta zote
kutekeleza
viwango vya kitaifa katika sekta za viwanda,biashara na huduma kwa kutumia
skimu mbalimbali za udhibiti ubora.
Hata hivyo aliongeza kwamba pamoja na hayo lakini pia upimaji wa bidhaa kwa lengo la kuhakikisha
ubora wake,pamoja na uthibitisho wa usahihi wa vipimo vinavyotumika viwandani
na kutoa mafunzo kwa wazalishaji pamoja na wafanyakazi katika taasisi na
viwanda kuhusiana na uzalishaji wa bidhaa bora,uzalishaji salama na usimamizi
wa ubora.