Home Mchanganyiko ZAIDI YA BILIONI 25 KUTUMIKA MATENGENEZO YA BARABARA

ZAIDI YA BILIONI 25 KUTUMIKA MATENGENEZO YA BARABARA

0

Kazi zikiendelea za kukarabati barabara ya Kahama – Solwa – Mwananga (km 148) kwa kiwango cha changarawe, wilayani Kahama.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akiruka katika mtambo wa kuchonga barabara wakati alipokuwa akikagua barabara ya Kahama – Solwa – Mwananga (km 148) inayokarabatiwa kwa kiwango cha changarawe, wilayani Kahama.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kahama – Solwa – Mwananga (km 148) kwa kiwango cha changarawe, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga. Barabara hiyo inaunganisha wakazi wa Wilaya ya Kahama na mkoa wa Mwanza.

………………………………………………………………………………………………………..

Imeelezwa kuwa zaidi ya kiasi cha shilingi Bilioni 25 zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara zilizoathiriwa na mvua nyingi zilizonyesha toka kipindi cha mwisho wa mwaka 2019.

Amezungumza hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati akiwa mkoani Shinyanga akiendelea na ziara yake ya kukagua athari za mvua katika miundombinu ya barabara.

Naibu Waziri Kwandikwa amekagua barabara inayotoka Kahama kuelekea Mwananga yenye urefu wa kilometa 148 ambapo sehemu ya barabara hiyo imeathiriwa na maji mengi yanayopita kwenye mkondo wa Ziwa Victoria.

“Hii ni barabara fupi inayounganisha wakazi wa Kahama na Mwanza kupitia Solwa ambapo kilometa 2. 3 ndizo zilizoathirika na hivyo kufanya mawasiliano ya wananchi hawa kuwa ni ya kuzunguka na muda kuongezeka”, amesema Naibu Waziri huyo. 

Ameongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo tayari usanifu wa kina ushafanyika na hivyo Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.

“Mvua hizi pia zinatupa sisi fursa ya kutazama eneo hili upya kwa kuhakikisha usanifu wetu unaenda sambamba na hali iliyojitokeza na hii itangaliwa maeneo yote nchini”, amefafanua Naibu Waziri Kwandikwa.

Ametoa wito kwa wasafirishaji wanaotumia barabara hiyo kutowasumbua wananchi kwa kutumia barabara hiyo na badala yake watumie barabara ya lami ile itokayo Kahama – Isaka – Tinde mpaka  Mwanza kwa kuwa inapitika vizuri kabisa.

Aidha, ameeleza mkakati wa Serikali katika kipindi hiki cha mvua kuwa inaendelea kufuatilia maeneo yote ambayo ni korofi na kuona namna nzuri ambayo inaweza kufanya ili kuwanusuru wananchi kuondokana na adha hizo na waweze kuendelea kupata huduma mbalimbali kwa kutumia barabara.

Kwandikwa amewahakikishia wananchi wa maeneo yote nchini ambao wameathiriwa na uharibifu wa mvua hizi katika miundombinu ya barabara kurejeshewa kwa mawasiliano katika maeneo hayo huku mwarobaini wa maeneo hayo korofi ukiandaliwa.

“Niwahakikishie wananchi kuwa Serikali yao iko makini, inasimamia rasilimali zote kwa makini na inakusanya fedha kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma kwa wananchi”,amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

 Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS),mkoa wa Shinyanga Mhandisi Frednand Mdoe, ameeleza kuwa wanapata changamoto kubwa ya kurudisha mawasiliano katika barabara hiyo kutokana na maji kuzidi kuongezeka na tayari washakusanya mawe kwa ajili ya kurudisha barabara hiyo ili iweze kupitika.

“Huu ni mkondo wa Ziwa hivyo maji yamekuwa mengi na kuvuka barabara na kasi ya kupungua kwa maji haya imekuwa ndogo lakini tumejipanga mipango ya sasa na mipango ya kudumu ambayo ni ujenzi wa madaraja katika barabara hii katika mwaka wa fedha unaokuja”, amesema Mhandisi Mdoe.

Naibu Waziri Kwandikwa yupo katika ziara ya kikazi mkoani Shinyanga ya kukagua athari za mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.