Home Siasa DKT. BASHIRU ATOA ONYO KWA MAKATIBU WA CCM WA WILAYA NA MIKOA

DKT. BASHIRU ATOA ONYO KWA MAKATIBU WA CCM WA WILAYA NA MIKOA

0

******************************

15 Februari, 2020

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally ametoa onyo kwa Makatibu wa CCM wa Mikoa na Wilaya ambao hawajatekeleza agizo la kuandaa vitambulisho kwa ajili ya Wenyeviti wa mashina (Mabalozi) katika maeneo yao.

Dkt. Bashiru ametoa onyo hilo kutokana na kuwepo kwa taarifa ya baadhi ya Watendaji wa Mikoa na Wilaya kutotilia mkazo maagizo hayo yanayolenga kuwajali na kuwaweka karibu mabalozi wa mashina ambao ndio viungo muhimu na wanafanya kazi kubwa ya kukiletea ushindi Chama Cha Mapinduzi.

Ameyasema hayo leo tarehe 15 Februari, 2020 akihutubia Mkutano Mkuu maalum wa utekelezaji wa Ilani Jimbo la Morogoro Mjini.

“Kwa mikoa ambayo Mabalozi hawajapata vitambuliso, watendaji wanaonisaidia, wanisikilize, nitapita kuhakiki, nikibaini vitambulisho havijatolewa kwa mabalozi wetu waliopo katika maeneo yenu, nitawatumbua.”

Akitoa sababu ameeleza kuwa, “Kwa sababu bila mabalozi mimi Ukatibu Mkuu wangu hauna maana, kwa Nchi kubwa kama hii Chama kikubwa kama hiki, kama huna mtandao wa viongozi walioko karibu na wananchi chama hakitaenda na nchi haitaenda.”

Akitoa umuhimu wa hilo ameeleza kuwa, vitambulisho hivyo vitawasaidia mabalozi kuingia ofisi yoyote ya umma kuanzia Mtendaji wa Kijiji au Mtaa, Kata, Mkuu wa wilaya, Mkoa na ofisi ya Waziri yeyote na kueleza shida zao, ambazo shida nyingi za mabalozi hawa huwa ni za wananchi wanaowaongoza.

Amesisitiza kuwa, “Mkuu wa Mkoa au Wilaya ambaye hatajua na kuthamini nini maana ya viongozi wa mashina, kama CCM ipo madarakani, Mkuu huyo wa Mkoa au Wilaya hatufai.”

Aidha wakati huo huo, Dkt. Bashiru ameendelea kusisitiza uundwaji wa Mabaraza ya wazee wa CCM ambao kitakuwa ni chombo cha kutoa ushauri na kukikumbusha Chama katika ngazi zote pale ambapo itaonekana kimetoka katika misingi ya kuasisiwa kwake.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu amegusia umuhimu wa moyo wa kujitolewa, na kueleza kuwa wenyeviti wa mashina kazi zote wanazozifanya ni kutokana na kuwa na moyo wa kujitolewa, lakini amesisitiza kuwa huwezi kuwa na moyo wa kujitolewa kama hujali shida za wananchi.

Awali, Katibu Mkuu alipita nakukagua maendelao ya ujenzi wa soko kubwa la kisasa linalojengwa Manispaa ya Morogoro Mjini ambapo ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Soko hilo, ambapo baada ya ukaguzi huo, alijumuika katika nyumba ya balozi wa shina namba tatu kata ya Uwanja wa Taifa na kupata Chai ya pamoja ikiwa ni sehemu ya kuenzi usawa, umoja na mshikamano ndani ya Chama.

Viongozi mbalimbali wamejumuika katika ziara hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa Ndg. Innocent Kalogeris na Mkuu wa Mkoa Ndg. Loatha Sanare.

Leo amehitimisha Ziara yake ya siku tatu mkoani Morogoro ambapo ametembelea wilaya za Kilombero, Morogoro Vijijini na Morogoro Mjini.