********************
NJOMBE
Wakazi zaidi ya 1600 wa kijiji cha Utalingolo halmashauri ya mji wa Njombe wamelazimika kukutana kwa dharura kuwekeana mikakati ya kukabiliana na wimbi la wizi na ujambazi wa ajabu ulioibuka kijijini hapo ambao unahusishwa na imani za kishirikiana .
Wakazi hao wamesema watekelezaji wa matukio hayo wanaziba sura na kisha kuvamia majumbani usiku na mchana huku wakiwa na siraha wakitaka kupewa vitu vya thamani na fedha na kisha kutokomea kama mizuka.
Kutokana na hali hiyo serikali ya kijiji imelazimika kuunda kamati yenye watu kutoka makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo wazee pamoja vikundi vya vijana 10 kila kitongoji ambao wanakwenda kuanza operesheni ya kuwasaka wahusika wa uhalifu huo
Anna Poul na Felis Msigwa ambao ni wananchi wa kijiji hicho wanasema wanahisi watu hao wanatumia nguvu za giza kutekeleza matukio hayo kwani wakishatenda uhalifu wanatoweka katika mazingira yakutatanisha.
Akiweka bayana maazimio yaliofikiwa mtendaji wa kata ya Utalingolo Atanasio Thomas anasema mbali na suala la usalama katika mkutano huo wananchi wamekuliana kuanzisha kamati za maadili ambazo zinakwenda kushughulika na vijana wanaovalia milegezo,wacheza kamali pamoja na unyoaji usio na maadili kwani ndiyo chanzo cha yote.
Petro Mahenge ni moja kati ya vijana wengi waliojumuishwa kwenye kikosi cha ulinzi shirikishi ambacho kinakwenda kupewa mafunzo ya usalama ili kuanza kazi ambaye anasema watatumia kila mbinu kuwanasa waalifu na kurejesha amani kijijini kwao.