Home Mchanganyiko Sekta ya Uvuvi inakua kwa kasi- Ulega.

Sekta ya Uvuvi inakua kwa kasi- Ulega.

0

********************************

Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewahakikishia wadau wote wanaokusudia kuwekeza kwenye sekta ya Mifugo na Uvuvi kuwa Serikali ya awamu ya tano ipo tayari kuondoa changamoto zote zinazowakabili katika uwekezaji wao na kuwawekea mazingira rafiki ya kuendesha shughuli zao hapa nchini.

Mhe. Ulega aliyasema hayo jana (12.02.2020) muda mfupi kabla ya kufungua kituo cha ufugaji wa samaki kwa njia za kisasa kinachojulikana kama “Big Fish” kilichopo Wilaya ya Kigamboni jijini Dar-es-salaam.

“Ninatambua kuwa vifaa vinavyoletwa hapa nchini kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kukuza sekta mtambuka huwa vinaondolewa tozo mbalimbali hivyo nimemuagiza Katibu Mkuu wa sekta ya Uvuvi ashughulikie nyaraka za msingi tuweze kuziwasilisha kwenye mamlaka husika ili hata vifaa vinavyoletwa nchini kwa ajili ya kukuza sekta ya uvuvi viondolewe kodi na tozo hizo” Alisema Mhe. Ulega.

Mhe. Ulega alisema kuwa kwa hivi sasa takwimu zinaonesha Tanzania inazalisha jumla ya samaki tani elfu 18 kupitia shughuli za ufugaji wa samaki kwa kutumia mabwawa na lengo ni kuhakikisha idadi hiyo inaongezeka na kufikia tani elfu 50.

“Hitaji la samaki kwa sasa hapa nchini ni tani laki 7 hadi 8 na uwezo wetu wa kuzalisha samaki kwa njia zote mpaka kufikia mwaka 2018/19 tumezalisha tani laki 4.4 hadi 4.5 hivyo hili ombwe la takribani tani laki 4 ni fursa nzuri kwa watanzania kupitia kwa wadau mbalimbali kuhakikisha tunalifikia na kupita hitaji la taifa” Alisisitiza Mhe. Ulega.

Awali kabla ya kumkaribisha Mhe. Naibu waziri, Balozi wa Uholanzi nchini Bw. Jeroen Verheul aliisifu Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wenye nia ya kutekeleza miradi mbalimbali hapa nchini ambapo alitoa rai kwa wadau wengine kuendelea kubuni miradi ambayo haitaathiri mazingira.

“Tukio la leo linaashiria ni kiasi gani ushirikiano baina ya nchi ya Uholanzi na Tanzania ni imara na unatekelezwa kwa vitendo sio tu kuishia kwenye makaratasi”Aliongeza Bw. Verheul.

Takwimu zinaonesha kuwa mpaka sasa kila Mtanzania anakula wastani wa kilo 8 za samaki kwa mwaka huku mpango wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ukiwa ni kuhakikisha kufikia 2025 kila Mtanzania awe anakula kilo 10 za samaki kwa mwaka.