Home Biashara BENKI YA STANDARD CHARTERED YAWEZESHA MKOPO WA TRILIONI 3.3 KUSAIDIA UJENZI WA...

BENKI YA STANDARD CHARTERED YAWEZESHA MKOPO WA TRILIONI 3.3 KUSAIDIA UJENZI WA MRADI WA SGR

0

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Bw.Sanjay Rughan akizungumza na wadau mbalimbali katika mkutano wa kutia saini makubalino ya mkopo wa kuwezesha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa wa SGR.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Philip Mpango na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Bw.Sanjay Rughan akitia saini mkataba wa mkopo kwaajili ya kuwezesha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Philip Mpango na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Bw.Sanjay Rughan wakionesha mikataba waliosaini kwaajili ya mkopo utakaosaidia kurahisisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR.

Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Mhe.Masanja Kadogoa akifuatilia kikao cha usainishaji wa mkataba wa mkopo ambao utasaidia kurahisisha ujenzi wa reli ya kisasa wa SGR.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Philip Mpango akizungumza na wadau mbalimbali katika mkutano wa usainishaji wa mkataba wa mkopo wa kuwezesha ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa wa SGR.

Baadhi ya wadau mbalimbali wakifuatilia mkutano wa usainishwaji wa mkataba wa mkopo wa kusaidia ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa wa SGR.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Philip Mpango na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered wakipata picha ya pamoja na baadhi ya wadau mbalimbali waliowezesha kufanikisha mkopo wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa wa SGR.

(PICHA NA EMMANUEL MBATILO FULLSHANGWE BLOG)

************************************

NA EMMANUEL MBATILO

Serikali kupitia Wizara ya fedha imeweza kupata mkopo wa shilingi trilioni 3.3 kupitia waabia 17 wakishirikiana na benki ya Standard Chartered ili kuwezesha mradi wa reli ya kisasa kukamilika kwa wakati.

Akizungumza katika hafla ya usainishaji wa mikataba ya mkopo huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Philip Mpango amesema kuwa kila mara wamekuwa wanaomba mabenki ya hapa nchini kuchangia katika miradi mikubwa ya vipaumbele vya taifa ili kuweza kufikia malengo yetu kama taifa.

“Mradi huu wa kujenga reli ya kisasa ni mradi ambao unakwenda kubadilisha maisha ya wananchi wakitanzania, hivi sasa unavyojengwa unawaajiri watanzania wengi, mradi huu unatumia baadhi ya vifaa ambavyo vinazalishwa hapa nchini hususani saruji, mchanga lakini nguvu kazi ni ya vijana wetu”. Amesema Dkt.Mpango.

Aidha Dkt.Mpango amesema kuwa deni la nchi yetu bado ni himilivu na ni lazima tukope kwasababu reli hii tunawekeza takribani miaka 200 ijayo. Hii reli iliyopo (Ya zamani) imekuwepo takribani miaka 100, hii ya kisasa itakaa zaidi ya miaka 200.

“Kuna baadhi ya waabia wetu tena wa siku nyingi tuliwaomba waingie kwenye safari hii ya kuchangia mkopo wala si kama wanatupa bure lakini walinikatalia kwahiyo tunashukuru sana kupitia kwenu serikali ya Denmark na serikali ya Sweden kuwa waabia wazuri na marafiki wa watanzania”. Ameongeza Dkt.Mpango.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Bw.Sanjay Rughani amesema kuwa zoezi la kuwekeana saini ya makubaliano ya mkopo kwaajili ya mradi wa reli ya kisasa ni hatua kubwa hasa katika suala la uchumi pamoja na upande wa uwekezaji.

“Afrika inabaki kuwa kipaumbele kwa biashara yetu na wateja kwa ujumla, tunajivunia kutumia utaalamu wetu kusaidia serikali ya Tanzania na fedha zinazohitajika kwenye mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa wa SGR”. Amesema Bw.Sanjay.

Pamoja na hayo Bw.Sanjay amesema kuwa upatikanaji wa wawekezaji 17 kusaidia mkopo huo ni juhudi kubwa imefanyika hivyo tutegemee kuwepo kwa maendeleo pamoja na ukuaji wa uchumi.

Nae Mkurugenzi wa Shirika la Reli hapa nchini Mhe.Masanja Kadogosa amesema kuwa mpaka kuwezesha upatikanaji wa mkopo kwaajili ya mradi huo, kutaongezeka kwa kasi ya ujenzi huo kwani mpaka sasa ujenzi kutoka Dar es Salaam mpaka mkoani Morogoro umefikia asilimia 73, hivyo mkopo huo utawezesha ujenzi wa reli hiyo kutoka mkoani Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida.