Home Mchanganyiko SERIKALI IMEFUNGUA BARABARA YA NYAHUA-CHAYA

SERIKALI IMEFUNGUA BARABARA YA NYAHUA-CHAYA

0

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Tabora Eng. Raphael Mlimaji, wakati alipokagua ujenzi unaoendelea wa barabara ya Nyahua – Chaya (km 85) kwa kiwango cha lami na athari za mvua zilizonyesha na maji kupita juu ya madaraja ya zamani na kusababisha
barabara hiyo kufungwa kwa muda.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akikagua athari za mvua katika barabara ya Nyahua – Chaya (km 85) iliyosababisha kufungwa kwa wiki moja na hapo jana aliifungua kuanza kupitika tena kwa magari ya kutokea
Kigoma, Tabora kuelekea mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam.

*************************

Serikali imeifungua  barabara ya Nyahua – Chaya yenye urefu wa kilometa 85 iliyokuwa imefungwa kwa kipindi cha wiki moja kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na maji kupita juu ya madaraja ya zamani na kuhatarisha usalama wa wananchi.

 
Amezungumza hayo Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa, mara baada ya kukagua miundombinu ya madaraja makubwa yanayoendelea kujengwa katika barabara hiyo ambayo ni daraja la nyahua (m 68) na
daraja kizengi (m 68) na kusema kuwa  Serikali imejipanga kikamilifu kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mawasiliano yanarudi katika maeneo yote korofi katika barabara kuu hapa nchini.

 

“Niseme tu kuwa sasa hali ni salama, wananchi wa Dar es salaam, Dodoma, Katavi na Kigoma  ni ruhusa kutumia tena barabara hii", amesema Naibu Waziri huyo.

 

Mhe. Kwandikwa amesema kuwa lengo la Serikali ni kuboresha miundombinu imara katika  kila maeneo ambayo yanaleta shida na kwa kuzingatia usalama wa wananchi kwanza.

 

Aidha, Naibu Waziri huyo ametoa tahadhari kwa wananchi wote ambao maeneo yao yamekubwa na mafuriko kupita kwa tahadhari na kuacha kufanya shughuli za kijamii kama kufua na kuvua  samaki katika maji mengi na huku hawana uzoefu wa kuogelea.

 

“Naelekeza kwamba pamoja na kuruhusu magari kupita lakini lazima tupite kwa usalama hivyo mkandarasi atakuwa hapa kuhakikisha hamna dosari zozote zinazoweza kujitokeza” Amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

 

Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unaoendelea, Naibu Waziri Kwandikwa amesema mkandarasi ameshamilisha kilometa 42 kujengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi anaendelea na kazi zake ndani ya
muda.

 

“Barabara hii ina umuhimu mkubwa kwa mkoa wa Tabora na Kanda za Magharibi na mkandarasi wa Kampuni ya Chico amenihakikishia kukamilisha mapema kabla ya muda uliopo katika mkataba",  amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

 

Kwa upande wake wa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Tabora Eng. Raphael Mlimaji amesema kuwa   barabara hiyo ilifungwa kutokana na mvua kubwa na walikesha hapo usiku na mchana na sasa barabara inaweza kuendelea kutumika.

 

Naye Afisa Mtendaji wa Serikali ya kijiji cha Kizengi, Bw. Asas Gwishushega, amesema kuwa mafuriko yaliyotokea mbali na kusimamisha mawasiliano pia yameharibu mashamba yao ya mpunga.

 

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo katika ziara yake ameshiriki katika kutoa pole kwa familia ya mwanafunzi Shaban Saidi aliyekuwa anasoma Shule ya Sekondari ya Kizengi kidato cha kwanza na kusombwa na maji wakati alipokuwa anafua nguo pembeni mwa mto huo.

 

Naibu Waziri Kwandikwa yupo katika ziara ya kikazi mkoani Tabora ya kukagua athari za mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.