Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Stegomena Taxi leo katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bi. Mara Marwick
wakati Bi. Marwack alipomtembelea Waziri katika ofisi ndogo za Wizara leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bi. Mara Marwick akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) wakati walipokuwa na mazungumzo katika ofisi ndogo za Wizara leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bi. Mara Marwick akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi
(Mb) mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika ofisi ndogo za Wizara leo jijini Dar es Salaam.
*******************************
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia hapa nchini Tanzania, Bi. Mara Marwick ameihakikishia Serikali ya Tanzania ushirikiano katika sekta mbalimbali ili kufikia
maendeleo yaliyokusudiwa.
Bi. Marwick ameyasema hayo leo tarehe 5 Februari 2020 alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi katika Ofisi Ndogo za Wizara zilizopo jijini Dar es
Salaam.
Bi. Marwick amesema uhususiano baina ya benki hiyo na Tanzania ni mzuri na kwamba Benki ya Dunia inathamini uhusiano huo wa tangu miaka ya 1960 hadi leo na
iko tayari kuendelea kuunga mkono kwa njia ya ufadhili au mikopo miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
“Tuna uhusiano mzuri katika miradi na uwekezaji ambapo tunaiwezesha serikali katika maeneo mbalimbali. Pia tunafanya kazi pamoja katika masuala muhimu kama vile uchambuzi wa sera za maendeleo hii inaashiria kuwa Benki ya Dunia itaendeleza ushirikiano huu katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na mahusiano imara pamoja
na maendeleo endelevu”. Amesema Bi. Marwick.
Ameongeza kuwa katika mazungumzo hayo, wamejadili masuala muhimu kuhusu maendeleo ya Tanzania hususani elimu, miradi ya miundombinu, uchumi wa viwanda,
pamoja na maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema Tanzania itaendeleza mahusiano na Benki
ya Dunia na kuwataka watanzania kupuuza uzushi na uvumi unaosambazwa katika mitandao ya kijamii kuhusu mahusiano baina ya Tanzania na Benki hiyo na badala yake
wasubiri taarifa rasmi kutoka kwa Serikali na Benki ya dunia.
“Uhusiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia ni imara na unaendelea vizuri, na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia ametuhakikishia kwamba katika kipindi hiki ambacho
yeye ni mkurugenzi hapa atauendeleza uhusiano huo huo. Mengi yanasemwa lakini mengi hayana ukweli na wakati mwingine si busara kwa kila yanayosemwa kuyajibu
kwasababu yanaweza kuwaondoa kwenye shughuli za msingi na mkajikuta kila siku mnajibu uvumi au uzushi katika mitandao ya kijamii na mambo mengine”. Amesema Prof. Kabudi.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa katika mazungumzo hayo pia wamegusia miradi ya kimkakati ambayo Tanzania inaitekeleza, mingine kwa fedha za ndani au kwa kupata
mkopo kutoka Benki ya Dunia.
“Tumezungumza kwa kirefu kuhusu mashirikiano katika elimu hasa elimu ya wasichana na kukuza rasilimali watu na kutaja maeneo mengine ya mashirikiano ambayo ni
pamoja na sekta za miundombinu, afya, maji na nishati”. Ameongeza Prof. Kabudi.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa Tanzania inakopesheka kwenye benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Afrika Mashariki ya Maendeleo na taasisi nyingi sana za kifedha na daima Serikali huhakikisha kuwa vigezo vyote vinavyotakiwa vinasimamiwa lakini kikubwa hulipa madeni iliyokopa na ndiyo maana inaaminiwa na
kukopeshwa zaidi na fedha yote inayokopwa hupelekwa kwenye miradi ya msingi ya kulifanya taifa kujitegemea lenyewe katika miaka michache ijayo.
Katika tukio jingiene, Waziri kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Stegomena Taxi
na kujalidiana nae mambo mbalimbali kuhusu SADC.