Mwanafunzi mwenye ulemavu wa uoni hafifu Ombeni Wilhard kutoka shule ya msingi Mgori akieleza changamoto zinazowakali watoto wenye ulemavu.
Afisa Miradi kutoka shirika la Medo, Hassan Rasuli akifafanua majukumu makubwa ya shirika hilo na kubainisha mafanikio toka wameanza mradi huo katika Halmashauri ya Singida.
Makamu Mwenyekiti Halmashauri ya Singida Mh.Omar akifungua kikao cha viongozi,wadau na mashirika binafsi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Singida akieleza mafanikio makubwa yaliyofanyika katika halmashauri hiyo kwa kipindi cha awamu ya tano.
Wadau wakiwa kwenye kikao hicho.
Mwanafunzi Ombeni Wilhard akiendelea kueleza changamoto zinazowakabili mbele ya Madiwani,wadau,wanafunzi we Halmashauri.
Na Mwandishi wetu, Singida
VIONGOZI mbalimbali wakiwemo Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida wamekutana na mashirika yasio ya Serikali kujadili namna ya kuweza kutatua changamoto zinazokabili sekta ya elimu
Katika kikao hicho kilichofanyika juzi kilichoandaliwa na Shirika la Mtinko Education Development Organisation (MEDO) kimeibua na kubainisha changamoto mbalimbali katika sekta hiyo hasa kwa upande wa watoto wenye ulemavu ambao baadhi yao waliopata fursa ya kushiriki kikao hicho walisema licha ya baadhi ya jamii kutambua umuhimu wa kuwapeleka watoto wao wenye ulemavu shule lakini bado wanakutana na vikwazo vingine ikiwemo mazingira bora ya kujifunzia
Ombeni Wilhard ni mwanafunzi mwenye ulemavu wa uoni hafifu kutoka Shule ya Msingi Mchanganyiko Mgori alisema wazazi wao wametambua na wamewapeleka shuleni kusoma lakini mazingira ya kujifunzia sio rafiki kwao kwani hukaa nje ya ofisi ya mwalimu mkuu jua lao baridi yao, hivyo akawaomba viongozi hao kuwajengea vyumba vya madarasa ili kuondokana na adha hiyo ambayo imekuwa ya mda mrefu,huku Amiri Mohamed mwenye ulemavu wa macho mwanafunzi kutoka shule hiyo ya Mgori akilia na mabweni yaliopo sio salama kwao kutokana na ulemavu wao ikizingatiwa wao hawawezi kuona huku vitanda vikiwa vya ngazi
Awali Afisa Miradi kutoka Shirika la MEDO Hassan Rasuli alieleza majukumu ya Shirika hilo kuwa ni kutoa elimu ya kuwajengea uwezo na uelewa wa haki na wajibu wa kulipa kodi wanafunzi ili watakapo kua baadaye wawe na uelewa huo, huku wakihamasisha jamii kuwapa haki watoto wao zikiwemo za elimu.
Rasuli alisema jamii nyingi bado haioni umuhimu wa kuwasomesha watoto wao hivyo wengi wao huwaacha wakiwa wamezagaa mitaa wamesahau kuwa wanatengeneza jamii dhaifu hapo baadaye ambayo itakuwa mzingo mkubwa kwa Serikali,hivyo akawaomba viongozi hao na madiwani kuendelea kuielimisha jamii juu ya masuala ya haki za watoto hasa haki ya kupata elimu itakayo msaidia kwenye maisha yake
Baada ya kuwekwa bayana changamoto hizo na nyingine kutoka kwa wanafunzi walioshiriki kikao hicho, wadau na mashirika binafsi.Sasa kazi ikabaki kwa wenye mamlaka nini kifanyike,ambapo madiwani walisema kuna haja ya kufanya ziara ya kuzitembelea shule hizo hasa zile zenye watoto wenye ulemavu kujionea na kuchukua hatua za maksudi kuondoa changamoto zilizopo kwani bahati nzuri huu ni wakati wa kutengeneza bajeti ambapo kikao cha baraza la madiwani cha kupitisha bajeti kitaketi hivi karibuni
Huku Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Rashid Mandoa akiwatoa wasiwasi wadau,mashirika binafsi,wanafunzi na viongozi wengine waliokuwepo kwenye kikao hicho kuwa changamoto hizo zitatatuliwa kwani serikali ya awamu ya tano haiwezi kushindwa kuondoa changamoto hizo ikizingatiwa ni mengi makubwa iliyofanya katika Halmashauri hiyo katika sekta ya afya na elimu.