Home Biashara SBL yafikisha ujumbe wa usalama barabarani kwa maelfu ya wakazi wa Iringa

SBL yafikisha ujumbe wa usalama barabarani kwa maelfu ya wakazi wa Iringa

0

Kamanda wa polisi kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa  SP. Yusuf Kamote (pichani kulia) akiongea na madereva wa vyombo vya moto kwenye kampeni ya usitumie kilevi na kuendesha chombo cha moto iliyoratibiwa na kampuni ya bia ya Serengeti Breweries Limited SBL mjini Iringa leo.

Kamanda wa polisi kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa  SP. Yusuf Kamote (pichani kulia) akimvisha Kiakisi mwanga Mwenyekiti wa Umoja wa Bodaboda Iringa, Juma Gamba wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usitumie kilevi na kuendesha chombo cha moto iliyoratibiwa na kampuni ya bia ya Serengeti Breweries Limited, hafla iliyofanyika katika viwanja vya Stendi ya Daladala Manispaa ya Iringa leo. Pichani kushoto ni Meneja mahusiano wa SBL, Neema Temba.

*****************************

Iringa, Februari 1, 2020 –

Maelfu ya wakazi wa mji wa Iringa na maeneo ya jirani, ikiwa ni pamoja na watumiaji barabara, madereva wa magari binafsi na ya usafiri wa umma wamepatiwa elimu ya usalama barabarani kupitia kampeni inayoendeshwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa kushirikia na Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani.

 

Ikijulikana kama ‘Usitumie Kilevi na Kuendesha Chombo cha Moto’, kampeni hii inalenga kuiunga mkono Serikali katika kuhamasisha usalama barabarani ili kuepusha ajali
zinazosababishwa na matumizi ya vilezi na kuendesha vyombo vya moto, alisema Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa SBL , John Wanyancha.

 

“Kampeni hii inawalenga madereva wa mabasi ya abiria, waendesha bodaboda, waenda kwa miguu, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu pamoja na wateja katika mabaa,” alisema Wanyancha.

 

Aliongeza “Usitumie Kilevi na Kuendesha Chombo cha Moto’ ni kampeni ya kitaifa inayolenga kuwaelimisha watumiaji wote wa barabara na haswa madereva juu ya unywaji wa kistarabu.

 

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kampeni hii imeweza kufika katika mikoa kama Mwanza, Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tanga Moshi na Arusha huku elimu iliyotolewa ikiwafikia takribani watu 100,000,”

 

Baadhi ya mbinu zinazotumika kufikisha ujumbe kwa umma juu ya usalama barabarani ni pamoja na redio, vipeperushi, makoti ya usalama barabarani, mabango, kuwafikia watu mmoja mmoja pamoja na kuwafikia watu kupitia vyombo vya habari kama televisheni na magazeti.

 

Akizungumza katika tukio la uzinduzi wa kampeni hiyo lililofanyika mjini Iringa, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Iringa Yusuph Kamota aliishukuru SBL kwa kuipeleka kampeni hiyo Iringa na kuongeza kuwa itasaidia kuongeza uelewa wa madereva na watumiaji wa barabara juu ya masuala ya usalama barabarani.

 

“Wote kwa pamoja kuanzia Jeshi la Polisi, madereva, jamii na wadau wengine tunajukumu la kuzifanya barabara zetu ziwe salama. Nimefurahi kuona kuwa pamoja na kwamba biashara yao ni ya kuuza pombe, wanalo jukumu la kuhamasisha unywaji wa kistarabu,” alisema RTO Kamota.