Home Mchanganyiko JNIA YAJIPANGA KUKABILI VIRUSI VYA HOMA YA CORONA

JNIA YAJIPANGA KUKABILI VIRUSI VYA HOMA YA CORONA

0

Wataalam wa Kitengo cha Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), leo wakijiandaa kabla ya kutua kwa ndege zinazofanya safari zake kutoka nchi mbalimbali kwenye Jengo la Tatu la abiria (TB3).

Moja ya eneo la ukaguzi wa afya kwa abiria wanaowasili kupitia Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakitokea nchi mbalimbali.

Wataalam wa Kitengo cha Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), leo wakijiandaa kabla ya kutua kwa ndege zinazofanya safari zake kutoka nchi mbalimbali kwenye Jengo la Tatu la abiria (TB3).

Abiria waliowasili kwa ndege ya Qatar wakikaguliwa kwa mashine maalum za kupima joto la mwili, ili kubaini walioingia nchini na virusi vya Homa ya Corona iliyoanzia nchini China hivi karibuni, na kuua watu kadhaa.

Afisa Afya Mkuu Mazingira, Onesmo Kitange (mwenye mashine ya mkono), leo akimpima Maitrick Dave, raia wa India, aliyewasili kwa ndege ya Kenya Airways alipowasili leo  kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

……………………………………………………………………………………………………..

Na Bahati Mollel, TAA

KITENGO cha Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza, kilichopo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kimejipanga kukabiliana na wagonjwa watakaobainika kuwa na virusi vya homa ya Corona,  vilivyoanzia nchini China.

Daktari George Ndaki, ambaye ni Mdhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza wa JNIA, leo amesema Wizara ya Afya imekabiliana na ugonjwa huo na tayari imefunga mashine tano zinazotumia komputa zinazopima joto la mwili la abiria bila kujitambua, na mashine sita za mkononi, ambazo abiria anapimwa endapo ataonekana kuwa na joto kali zaidi. 

Amesema mashine moja imefungwa kwenye Jengo la Watu Mashuhuri (VIP) , nyingine imefungwa Jengo la Pili la abiria na tatu zipo jengo la Tatu la abiria; wakati za mkono zimeganywa kwenye majengo hayo. 

Dkt Ndaki amesema wataalam wa afya wanaokuwa kwenye mashine zinazotumia komputa wanamtambua abiria mwenye jotokali mara anapopita mbele ya kamera, na endapo litabainika ni zaidi ya nyuzijoto 37.4 anahakikiwa zaidi kwa kutumia mashine ya mkono, huku akihojiwa zaidi juu ya afya yake na nchi aliyotoka, ili kubaini endapo anavirusi hivyo.

“Hadi sasa hakuna abiria aliyebainika kuwa na ugonjwa huu, lakini tunaendelea kwani hapa Kiwanja cha ndege ni moja ya njia kuu au lango Kuu la abiria hususan wa nje ya nchi wanapotumia kuingia nchini, na ndio maana tunawakagua na tunashukuru Serikali yetu kupitia Wizara ya Afya kwa kuwa na mashine hizi mbili, ambazo zinafanyakazi mara mbili na kwa uhakika zaidi ili kubaini abiria mwenye virusi, ambaye atapelekwa eneo maalum kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” amesema Dkt Ndaki.

Dkt Ndaki amesema pamoja na kukaguliwa kwa abiria wote wanaowasili kutoka nje ya nchi, pia wanaweka mkazo zaidi kwa abiria wanaotoka nchi zilizoathiriwa na ugonjwa huom, ambapo abiria wake mbali na kupimwa joto la mwili, pia wanaandikwa majina yao na maeneo wanayokwenda baada ya kutoka JNIA.

“Ukiangalia kuna ndege ambazo zinakuja na abiria waliotoka China baada ya kuunganisha ndege kama Kenya Airways, Qatar, South Africa, Fly Emirates na  na Shirika la ndege la Tanzania (ATCL), zinakuwa aidha zimebeba abiria waliounganisha ndege kutoka nchi zilizoshambuliwa na homa ya Corona”. Amesema Dkt Ndaki.

Hata hivyo, amesema siku zote wamekuwa wakijiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana magonjwa mbalimbali ya mlipuko na kuambukiza, ili yasiweze kuingia nchini kupitia mipaka mbalimbali, pamoja na viwanja vya ndege.

Mbali na China nchi nyingine zilizoathirika na homa hii ni pamoja na Thailand, Australia, Marekani, Singapore, Malaysia, Japan, Korea Kusini, Ufaransa, Canada, Vietnam, Ujerumani, Nepal, Sri-lanka na Cambodia. Hata hivyo, kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona sasa ni tishio hadi Barani Ulaya.

Corona ni kundi kubwa la aina ya virusi, ambavyo huweza kumuathiri binadamu na wanyama, ukubwa wa maambukizi unahusisha homa za kawaida pamoja na homa kali na wakati mwingine matatizo katika mfumo wa upumuaji.

Dalili za kuathiriwa na virusi vya Corona ni pamoja na kukohoa, homa kali, nimonia, kupumua kwa tabu, kutapika na kuharisha; na hali ikiwa mbaya dalili hizi hujidhihirisha matatizo kwenye mapafu na figo kushindwa kufanya kazi.

Namna mtu anavyoambukizwa homa hii ni pamoja na kugusana moja kwa moja bila kinga na muathirika; kushika kwa mkono vifaa vya muathirika na baadaye kushika mdomoni au puani, ambapo virusi husambaa kwa kasi. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, hivi karibuni amesema hakuna Mtanzania yeyote anayeishi nchini China, aliyekumbwa na maambukizi ya virusi vya homa ya Corona, vilivyozuka katika Mataifa ya Marekani, China, Thailand, Korea Kusini na Japan.

Waziri Kabudi ameyasema hayo wakati akitoa ufafanuzi juu ya hali ya Watanzania waishio nchini China na kusema kuwa Tanzania ina wanafunzi takribani 4000, ambapo katika mji wa Wuhan kuna wanafunzi 400 na kwamba kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania Nchini China, Balozi Mbelwa Kairuki, ameihakikishia Serikali kuwa mpaka sasa hakuna mtanzania yeyote aliyeathiriwa ama kukumbwa na maradhi hayo.

Ameongeza kuwa Tanzania inaendelea kufuatilia kwa ukaribu kujua maendeleo na hali za Watanzania wanaoishi jimboni Wuhan na China kwa ujumla na kuwataka Watanzania kuwa makini na suala la kutoa taarifa zisizo rasmi ama uvumi, kwani kwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za Tanzania na kuwataka kuwa na subira ili kupata taarifa rasmi kutoka serikalini.

Kutokana na maradhi haya kuwa mapya hadi sasa hakuna chanjo ya homa hii , na badala yake wagonjwa wamekuwa wakipewa dawa za kutuliza maumivu pekee.

MWISHO