Home Mchanganyiko KAMATI YA URASILIMISHAJI WA ARDHI YAVUNJWA BAADA YA KUTOTEKELEZA MAJUKUMU YAKE

KAMATI YA URASILIMISHAJI WA ARDHI YAVUNJWA BAADA YA KUTOTEKELEZA MAJUKUMU YAKE

0

******************************

KAMATI ya Urasilimishaji wa ardhi ya Mtaa wa Bangulo, Kata ya Pugu Stesheni, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam imevunjwa rasmi baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake kama ilivyotakiwa.

Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Bangulo katika kata hiyo Bw.Goodluck Mwele amesema kuwa kabla ya kuvunja kamati alitahadharisha viongozi kutochezea maslahi na roho za wananchi wa Dangulo kwa kuhoji kamati hiyo ilikuwa na nguvu ipi zaidi kuliko wananchi.

 

“Kama viongozi tumejaribu kukaa pamoja kabla ya kuvunja kamati hiyo kuona namna gani ya kupata taarifa za wananchi kuhusu kamati hiyo bila mafanikio,” alisema.

Baada ya kuvunjwa kwa kamati hiyo yenye wajumbe tisa, mjumbe mojawapo Amina Mongi alishangaa kuvunjwa kwa kamati hiyo kwa maelezo kuwa kazi hiyo waliyokuwa wamepewa ilikuwa inafikia mwisho kwani mwezi ujao zoezi hilo lingehitimishwa.

Alisema mpaka siku hiyo kamati hiyo ilipovunjwa tayari viwanja zaidi ya 3000 vilikuwa vimepimwa na kupandwa mawe.

Awali mwenyekiti huyo wa serikali ya mtaa wa Bangulo alielezea mpango kazi wake ni pamoja na kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarika katika eneo hilo.

Alisema wananchi hawawezi kufanya mambo ya maendeleo endapo usalama wao ni mdogo.

Pia alizungumzia barabara kwa kueleza kuwa mtaa huo hauna barabara zinazopitika mara kwa mara lakini wamechukua hatua tayari ya kutatua changamoto hiyo.

“Wapo wananchi si waaminifu wanaona mchanga unaopita kwenye barabara ni fursa kwao. Tuache kuvunja sheria kwa kusomba mchanga huo kwa ajili ya ujenzi ama kuuza,” alisema.