Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu ,Sera, Bunge, Ajira na Wenyeulemavu, Jenista Mhagama akizungumza wakati akifungua semina ya Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini iliyofanyika leo jijini Dodoma.
Waziri wa Madini Mhe.Dotto Biteko akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini iliyofanyika leo jijini Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto (wa kwanza kulia) akiwa na makamanda wengine wakifatilia kwa umakini hotuba ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu ,Sera, Bunge, Ajira na Wenyeulemavu, Jenista Mhagama alipokuwa akifungua semina ya Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini iliyofanyika leo jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wakifatilia hotuba ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu ,Sera, Bunge, Ajira na Wenyeulemavu, Jenista Mhagama alipokuwa akifungua semina ya Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini iliyofanyika leo jijini Dodoma.
Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi la Polisi, Benedict Wakuryamba,akitoa neno la shukrani kwa niaba ya vyombo vya ulinzi na usalama kwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu ,Sera, Bunge, Ajira na Wenyeulemavu, Jenista Mhagama alipokuwa akifungua semina ya Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini iliyofanyika leo jijini Dodoma.
…………………..
Na.Aex Sonna,Dodoma
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu ,Sera, Bunge, Ajira na Wenyeulemavu, Jenista Mhagama ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuangalia kama kuna tija kwa baadhi ya migodi kulindwa na kampuni za ulinzi kutoka nje ya nchi.
Wito huo ameutoa leo wakati akifungua semina ya Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini iliyofanyika jijini Dodoma.
Semina hiyo iliwashirikisha Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,Makamanda wa Polisi Mikoa,Wakuu wa Upelelezi Mikoa na Watendaji wa Taasisi na Wizara ya Madini kwa lengo la kujadili mbinu za kulinda rasilimali za madini na kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali hiyo muhimu.
Mhe.Mhagama amesema kuwa ni muhim vyombo vya ulinzi na usalama vihusike kulinda rasilimali hizo muhimu ili kuhakikisha maslahi ya taifa yanasimamiwa ipasavyo.
“Nashangaa baadhi ya walinzi kutoka Nje ya Nchi hili tuliangalie kama lina tija ni kweli tunahitaji wageni wenye ujuzi lakini haya tunatakiwa kuyazungumza,”amesema.
Aidha amesema kuwa ulinzi na usalama ni nyenzo muhimu katika kuwezesha sekta ya madini inawanufaisha Watanzania.
“Sekta ya madini imekuwa na changamoto nyingi ikiwemo utoroshwaji wa madini kwenda nchi za nje bila kulipiwa tozo zinazotakiwa, ukwepaji wa kodi stahiki na mambo ambayo ni kinyume na sheria, kanuni na taratibu zilizopo,” amesisitiza.
Waziri amesema kuwa uthubutu uliofanywa na Rais Dk. John Magufuli, kuleta mageuzi katika sekta ya madini kwa kuangaliwa upya Sheria ya Madini ya mwaka 2010, yamewezesha Watanzania na wawekezaji kunufaika kwa usawa.
Hivyo ni wajibu kuhakikisha sekta hiyo inaimarika, uzalishaji unaongezeka kwa kutoa mchango stahiki kwa taifa, kuhamasisha uwekezaji mpya na uwepo wa mtandao wa mawasiliano ya ndani ya kiserikali kabla ya kufanya maamuzi ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kuzorotesha ukuaji wa sekta ya madini.
“Nitoe rai, vyema mnapofanya maamuzi yanayohusu ulinzi na usalama kwenye shughuli za madini, muwe mmejiridhisha vya kutosha na vyanzo vya habari,pia kupata taarifa au ufafanuzi kutoka kwa mamlaka zinazohusika kabla ya kuchukua hatua,” amesema Mhagama
Awali ,Waziri wa Madini, Dotto Biteko, amesema kuwa mwelekeo na malengo ya wizara hiyo ni kuhakikisha sekta ya madini inaongeza mchango wake kwenye uchumi wa nchi.
Mhe,Biteko amesema kuwa wanatarajia ifikapo mwaka 2025, sekta ya madini itachangia zaidi ya asilimia 10 kwenye pato la taifa.
Hata hivyo Mhe. Biteko amesema baada ya marekebisho yaliyofanyika mwaka juzi ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 pamoja na kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini, mwaka wa fedha 2018/19 mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa (GDP) ulikua kwa asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilimia 4.8 kwa Mwaka 2017/18.
Aidha amesema kuwa katika kipindi cha nusu mwaka kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana kasi ya ukuaji wa sekta ya madini ilikuwa kwa asilimia 13.7 ambapo ilishika nafasi ya pili kiukuwaji ikitanguliwa na sekta ya ujenzi.
“Katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara imeweza kukusanya sh. bilioni 242 sawa na asilimia 103 ya lengo la nusu mwaka la kukusanya sh. bilioni 237.5,”amesema Waziri Biteko.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya vyombo vya ulinzi na usalama, Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi la Polisi, Benedict Wakuryamba, amesema kuwa bila ulinzi na usalama kuimarika, hakuna jambo litakaloweza kufanyika kwa manufaa ya Watanzania.
“Sisi kwa pamoja tunahakikisha tunalinda rasilimali zetu kwa weledi na nguvu ili taifa letu litoke kwenye utegemezi na kuwa taifa lenye kujitegemea,” amesisitiza