Home Mchanganyiko WAKURUGENZI WA HALMASHAURI TATUENI UHABA WA VYUMBA VYA MADARASA NA MATUNDU YA...

WAKURUGENZI WA HALMASHAURI TATUENI UHABA WA VYUMBA VYA MADARASA NA MATUNDU YA VYOO- WAITARA

0

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Mhe. Mwita Waitara akizungumza na Makatibu tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri(hawapo pichani) leo wakati wa kufunga mkutano mkuu wa kumi wa  Jumuiya ya Ushirikiano wa Wataalamu Tanzania na Osaka (TOA) Jijini Dodoma.

Baadhi ya Makatibu tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wakiwa katika mkutano mkuu wa kumi wa  Jumuiya ya Ushirikiano wa Wataalamu Tanzania na Osaka (TOA) Jijini Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Mhe. Mwita Waitara akisalimiaana na baadhi ya makatibu tawala na mikoa na wakurugenzi wa halmashauri leo wakati wa kufunga mkutano mkuu wa kumi wa  Jumuiya ya Ushirikiano wa Wataalamu Tanzania na Osaka (TOA) Jijini Dodoma.

…………….

Na Majid Abdulkarim,

Serikali imewataka viongozi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa wanawasimamia wananchi wachangie maendeleo ya elimu katika maeneo yao kwa kuboresha miundombinu mbalimbali ya shule ili waweze kutatua changamoto za uhaba wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.

 Agizo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Mhe. Mwita Waitara wakati akizungumza na Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri.

Amesema kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi hasa wale wanaojiunga na masomo ya kidato cha kwanza, kuwe chachu kwa wadau wa elimu nchini kuhakikisha kuwa miundombinu ya elimu inayokosekana katika shule zao inapatikana kulingana na mahitaji halisi ya shule husika. 

Mhe. Waitara ameongeza kuwa viongozi hao wana wajibu mkubwa wa kuwahamasisha wananchi wanaowaongoza kuchangia maendeleo mbalimbali katika maeneo yao yakiwemo kuongeza vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo ili waweze kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ambayo imeamua kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. 

 “Ili kutatua changamoto hizo mashuleni fanyeni uhamasishaji katika maeneo yenu ili wadau na wazazi waweze kuchangia katika kutatua changamoto hizo,” amesema Mhe. Waitara.

Akizungumzia kuhusu viongozi wapya waliochaguliwa na wananchi katika uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa, Mhe. Waitara amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa wanawasimamia viongozi hao waliochaguliwa ili waweze kutekeleza wajibu wao kwa weledi bila ya kubugudhiwa na viongozi wa kisiasa.

 “Mkilinda amani katika maeneo yenu mnayofanyia kazi italeta chachu kubwa ya kuleta maendeleo kwa watanzania mnao watumikia kama azma ya serikali ya awamu ya tano ilivyo katika kutekeleza wajibu wake kwa watanzania,” ameeleza Mhe. Waitara.

Aidha Mhe Waitara amewataka viongozi hao wa Mamlaka za serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa wanasimamia fedha za halmashauri zinazopaswa kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao ili miradi hiyo iendane na kiwango cha fedha iliyotolewa.