Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally ameweka wazi kuwa, jambo moja kubwa lililofanywa na Serikali ya awamu ya Tano chini Mhe. Rais John Pombe Magufuli ni kurejesha matumaini mapya kwa wanyonge na wavuja jasho waliokuwa wamekata tamaa.
Amesema kuwa, wanaCCM wote, watembee kifua mbele kwani, kati ya mambo makubwa ambayo serikali ya CCM ya awamu ya tano imeyafanya ni kurejesha matumaini ya wanyonge, ambapo hilo pekee ni jambo kubwa na limeleta faraja kwa watu wengi, sasa wanaimani kubwa na CCM.
Ameyasema hayo leo tarehe 19 Januari, 2020 Kigoma Mjini akizungumza na viongozi wa Mashina, Matawi, Kata, Wilaya na Mkoa.
“WanaCCM tembeeni kifua mbele, kati ya mambo ambayo awamu ya tano imeyafanya na makubwa hayatasahaulika, ni kurejesha matumaini ya wanyonge, na hilo katika siasa ni jambo kubwa, matumaini mapya kwa watu waliowahi kukata tamaa, matumaini mapya kwa wavuja jasho, matumaini hayo yamerejea chini ya uongozi shupavu, uongozi wenye maono, uongozi wa kizalendo wa Dkt. John Pombe Magufuli.”
Ameongeza kuwa, “wanaCCM mkiulizwa ni jambo gani jipya limefanyika linalopimika , linaloonekana kila mahala na kila mwenye akili na nia njema, waelezeni bila kupepesa macho, jambo kubwa jipya ni kurejesha matumaini mapya kwa wanyonge.”
Amesisitiza zaidi kuwa, kila analolifanya Mhe. Rais Magufuli, kila analolisimamia na kila analoliamua ni kwa maslahi ya kuwapa matumaini mapya watanzania wavuja jasho na katika hili mpaka sasa ameacha alama kubwa, ukiacha ujenzi wa barabara, reli, madaraja na mengine mengi anayoyafanya.
Aidha, Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wanaCCM wote kuwa, Chama Kimejipanga vya kutosha kurejesha Jimbo na Halmashauri ya Kigoma Mjini ambapo kwa sasa vyote vinaongozwa na upinzani, hivyo wanachama wote waendelee kuwa na umoja na mshikamano zaidi.
Wakati huo huo, Katibu Katibu amegawa vitambulisho kwa wenyeviti wa mashina ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo kwa wenyeviti hao nchi nzima kupatiwa vitambulisho na watambuliko katika ofisi zote za Umma.
Mkutano huo wa ndani umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma Ndg. Amandus Nzamba na Mkuu wa Mkoa huo Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga.
Leo Katibu Mkuu amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu Mkoani Kigoma iliyolenga kuimarisha na kuhuisha uhai wa Chama, ambapo tayari amewasili Dar es Salaam kuendelea na Majukumu ya kikazi.