Home Mchanganyiko KATIBU MKUU KAZI: UCHUMI WA VIWANDA UZINGATIE USALAMA NA AFYA KAZINI

KATIBU MKUU KAZI: UCHUMI WA VIWANDA UZINGATIE USALAMA NA AFYA KAZINI

0

Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Andrew Massawe, akiongoza kikao baina yake na menejimenti ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) alipotembelea ofisi za taasisi hiyo hivi karibuni kufuatilia utekelezaji wa maelekezo na miongozo ambayo ofisi yake imekuwa ikiitoa.

Wajumbe wa menejimenti ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wakimfuatilia Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Andrew Massawe, katika kikao alichokiendesha alipotembelea ofisi za Wakala za jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

*********************************

Na Mwandishi Wetu

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umetakiwa kuongeza jitihada katika kuwaelimisha wananchi kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Afya
na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa njia ya mtandao.

 

Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Andrew Massawe, alipotembelea ofisi za OSHA zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo alifanya kikao na menejimenti
ili kupata mrejesho wa utekelezaji wa maelekezo na miongozo mbali mbali ambayo ofisi yake imekuwa ikiyatoa katika kuboresha huduma kwa wananchi.

 

“Katika kipindi hiki ambacho serikali inaweka msukumo mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, tunataka mageuzi haya ya viwanda yaende sambamba na uzingatiaji wa viwango vya Usalama na Afya mahali pa kazi ili
kuepuka madhara yanayoweza kutokeaa endapo suala hili muhimu halitazingatiwa,” alisema Massawe na kuongeza:
“Mmezungumzia pia kuhusu kupanua wigo wa kazi zenu hizi katika maeneo mengi ya nchi; hilo nalo ni jambo la msingi japokuwa tunataka kuweka msisitizo katika utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao (automation) lakini
tunahitaji kuwa na ofisi walau katika maeneo yote muhimu. Hivyo tunatakiwa kujenga mahusiano mazuri na taasisi nyingine katika Wizara ili tuweze kutumia majengo yaliyopo kwa pamoja kwasababu hatuhitaji kujenga au
kukodisha majengo kila mahali.”

 

Maagizo hayo ya Katibu Mkuu yalitolewa baada ya kupokea taarifa fupi ya utekelezaji ya maagizo ya Wizara kutoka kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, ambapo pamoja na kuelezea utekelezaji mzuri wa maagizo
na miongozo mbali mbali ya serikali, alielezea mpango wa kufungua ofisi za Kanda ya Magharibi mkoani Tabora itakayohudumia mikoa ya Tabora, Kigoma, Rukwa na Katavi.

 

Aidha, katika taarifa hiyo, Mwenda ilielezea jinsi ambavyo taasisi yake imefanikiwa katika matumizi ya mifumo mbali mbali ya serikali ikiwemo mifumo ya malipo serikalini ya GePG, MUSE pamoja na mfumo Ununuzi na Ugavi serikalini wa TANePS.

 

Katibu Mkuu alisema: “Nimeridhishwa na utekelezaji wa mambo mbali mbali tuliyowaagiza hususan matumizi ya mifumo mbali mbali ya serikali.”

 

OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu ambayo husimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Kupitia sheria hii, OSHA husajili maeneo ya
kazi na kuyafanyia ukaguzi kuhakikisha kwamba yanazingatia viwango vya kiusalama na afya na hivyo kuwakinga wafanyakazi dhidi ya magonjwa na
ajali zitokanazo na mazingira ya kazi.