Home Mchanganyiko Serikali yaagiza Chuo cha Diplomasia kutoa elimu ya vitendo

Serikali yaagiza Chuo cha Diplomasia kutoa elimu ya vitendo

0

Mgeni Rasmi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Faraji Mnyepe wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa Mahafali ya 22 ya chuo cha Diplomasia. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Chuo, Dkt. Jeremia Ponera/

Baadhi ya Mabalozi na viongozi waandamizi wa Serikali wakiwa wanaimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa Mahafali ya 22 ya chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam.

Wahadhiri wa Chuo hicho nao wakiwa wamesimama huku
wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa mahafali

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika MasharikiDkt. Faraji Mnyepe akisoma hotuba yake kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), ambaye pia alikua mgeni rasmi wa Mahafali ya 22 ya Chuo cha Diplomasia, Dar es Salaam, akitoa hutuba yake wakati wa mhafali yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), akimkabidhi zawadi mmoja kati ya wanafunzi walifaulu vizuri masomo yake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika MasharikiDkt. Faraji Mnyepe na Kaimu Mkurugenzi wa Chuo, Dkt. Jeremia Ponera wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi walifaulu vizuri masomo yao.

********************************

Serikali imekitaka Chuo cha Diplomasia kutoa taaluma ya
vitendo kwa wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho ili
kuwawezesha wahitimu kuwa na mchango katika Taifa
hususani wakati huu wa utekelezaji wa sera ya
Diplomasia ya Uchumi.

Akihutubia mahafali ya 22 ya Chuo cha Diplomasia,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ambaye
ni Mgeni Rasmi katika mhafali hayo, amesema Serikali
itafurahi kusikia chuo kinatoa mafunzo ya stratejia,
jiopolitiki na demokrasia pamoja na haki za binadamu
hasa kwa muktadha wa kiafrika.

 

Waziri Kabudi ameongeza kuwa taaluma inayotolewa na
Chuo hicho isiwe ya nadharia pekee bali iambatane na
vitendo ili elimu hiyo itumike kusaidia kufafanua masuala
ya Kidiplomasia na uhusiano wa Kimataifa yanayotokea
duniani.

 

“Nakiagiza Chuo kuandaa mpango mkakati wa mafunzo kwa vitendo ili tuangalie ni jinsi gani Wizara inaweza kusaidia. Aidha, Chuo kipitie mitaala yake mara kwa mara kama ilivyopendekezwa ili kisipitwe na wakati.
Dunia inabadilika kwa kasi. Nasi hatuna budi kwenda kwa
kasi hiyo”. Amesema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa, ni vyema Chuo kikawa
mstari wa mbele kutoa mafunzo hayo kwa wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa,
na wafanyabiashara waliopo hapa nchini.

 

“Nimefarijika kusikia kuwa mmefanya mazungumzo na Chuo cha ISRI cha Angola kwa nia ya kufikia
makubaliano ya kutoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili
nchini Angola ambapo rasimu ya Hati ya Makubaliano
imeandaliwa na inasubiri kusainiwa”. Amesema Prof.
Kabudi.

 

Prof. Kabudi aliongeza kuwa, Serikali inatambua kwamba
Balozi za Iran, Libya, Urusi, Indonesia na China
zimekuwa zikitumia wigo huu wa ushirikiano na
kubadilishana uzoefu, kutoa mada mbalimbali chuoni
hapo.

 

Aidha, alitumia fursa hiyo kuzikaribisha ofisi
nyingine za kibalozi hapa nchini kutembelea Chuo cha
Diplomasia na kutoa uzoefu wao kwa vinafunzi pamoja
na wakufunzi. Hivyo basi, ni vyema menejimenti ya Chuo
kutoa mwaliko kwa Balozi zote na wawakilishi wa
kudumu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kuja
kutoa uzoefu wao kwani nayo itakuwa sehemu ya
diplomasia ya ulimwengu.

 

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dkt. Faraji Mnyepe amesema wahitimu 453
wametunikiwa vyeti baada ya kupata mafunzo na kufuzu
ambapo kati yao 98 ni wa ngazi ya Astashahada ya Msingi, 119 ni wa Stashahada ya kawaida, 130 ni wa
Shahada, 83 ni wa Stashahada ya Uzamili, 45
Stashahada ya uzamili wa diplomasia ya uchumi.

 

“Nina imani kuwa wahitimu wa leo kama wale wa miaka
ya iliyopita, wameiva ipasavyo katika fani za mahusiano
ya kimataifa, Diplomasia na Stratejia. Naamin pia kuwa
mtakuwa rasilimali kubwa kwa Taifa letu katika fani
mlizosomea”.Amesema Dkt. Mnyepe.

 

Dkt. Mnyepe ameongeza kuwa, katika mwaka wa
masomo 2019/20 chuo kimeweza kuongeza udahili wa
wanafunzi kutoka 1029 kwa 2018/19 hadi kufikia 1275
kwa mwaka wa masomo 2019/20 ambapo pamoja na
mambo mengine juhudi zinaendelea katika kutanua wigo
wa udahili kwa kuanziasha udahili wa mwezi Machi
pamoja na kuanzisha program mpya.

 

“Katika mwaka wa masomo 2019/20 chuo pia kimeweza
kupanua mawanda ya program zake kwa kuongeza idadi
ya program za muda mrefu. Chuo kimeanzisha
Stashahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Amani na
Udhibiti wa Migogoro ambapo kwa sasa program hii
inaendeshwa Dar es Salaam na Dodoma," Amesema Dkt. Mnyepe.

 

Chuo cha Diplomasia kilianzishwa rasmi tarehe 13
Januari 1978 kwa kusainiwa Makubaliano yaliyofanywa
na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi zetu mbili wa
wakati huo, Mhe. Benjamini William Mkapa wa Tanzania
na Mhe. Joaquim Chissano wa Msumbiji.

 

Kwa miaka yote hiyo, Chuo cha Diplomasia kimejikita kuwaandaa wanadiplomasia, wanastratejia na wabobezi wengi wa masuala ya Uhusiano wa Kimataifa.

 

Chuo kilitumika kuwaandaa wapigania uhuru wa nchi ya
Msumbiji na baadae kilipanua huduma zake na kutumika
kuwaandaa pia wapigania uhuru wa nchi za Angola,
Zimbabwe, Namibia n.k.