Home Mchanganyiko NAIBU WAZIRI AKAGUA SHULE YA SUNNI MUSLIM JAMAAT KABLA YA USAJILI

NAIBU WAZIRI AKAGUA SHULE YA SUNNI MUSLIM JAMAAT KABLA YA USAJILI

0

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha ameridhishwa na miundombinu ya Shule ya Sunni Muslim Jamaat (SMJ) ya Dar es Salaam na kwamba licha ya kukosekana kwa uwanja wa michezo, inapaswa kutazamwa kwa jicho la tatu kuiwezesha kusajiliwa kutoa huduma.

Ole Nasha amefanya ziara ya ukaguzi wa shule hiyo kwa niaba ya Waziri Joyce Ndalichako na amekiri kuwa SMJ iko katika mazingira mazuri yaliyozungukwa na miundombinu bora japokuwa inabanwa na Sheria ya Ukubwa wa Eneo la ujenzi wa shule kuwa hekari tatu, ambayo inapaswa kufanyiwa tathmini.

“Huduma zote muhimu zipo hapa kasoro uwanja tu, na hapa ni mjini, kupata eneo la kutosha kujenga uwanja ni ngumu. Kama Wizara tutajadili kwamba ikitokea shule ikiwa na huduma zote bora na muhimu, lakini kasoro uwanja tu, tunafanyaje?” amesema Ole Nasha.

Ameongeza kuwa Sheria inataka ukubwa wa eneo la shule inayopaswa kupewa usajili wa kudumu kuwa na ukubwa usiopungua hekari tatu, hata hivyo wanapaswa kuziweka sheria hizo kwa kuzingatia mazingira yaliyopo, hususani kwa wawekezaji wanaojenga shule mijini.

“Mazingira ya miji mikubwa kama Dar, ukizingatia kila shule iwe na uwanja, kuna zitakazofungwa kwa sababu nyingi hazina viwanja kutokana na ufinyu wa maeneo. Kama Wizara tumeanza kuona changamoto katika kulazimisha baadhi ya sheria.

“Kwa mfano sheria inataka ili kusajili Shule ya Msingi ni lazima iwe na madara sita, ofisi ya walimu, nyumba mbili za walimu na vyoo vya kutosha, sasa swali linakuja inapotokea wananchi wamejitahidi kujenga shule ya madarasa matano, unawezaje kuwanyima usajili kisa hawana darasa moja?” Amesisitiza Ole Nasha.

Wakati huo huo Ole Nasha amesema katika vikao vijavyo watazifanyia tathmini sheria hizo ili kutoa fursa pana kwa wadau wa elimu kuanzisha na kusajili shule zao ambazo kiuhalisia zinapoanza hutumia darasa moja na sio yote kwa mpigo, hivyo watakapofikia kujaza madarasa yote shule inaweza kuwa imejiongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sunni Muslim Jamaat, Salim Hassan Turky, ambaye pia ni Mbunge wa Mpendae visiwani Zanzibar, amemshukuru Naibu Waziri Ole Nasha kwa kutembelea shule hiyo kwa niaba ya Waziri Ndalichako.

“Tumefarijika sana sisi Sunni Muslim Jamaat kwa akututembelea kuona utendaji wetu. Tumekuwa tukiwaita Wizara kuona shule na miundombinu yetu, kwa ujio huu sasa, Naibu Waziri utaona namna tulivyo ‘serious’ katika hili,” alisisitiza Turky.

Aidha, Turky amesema Sheria inayowataka wajenge shule katika eneo lisilopungua heka tatu imewabana kwani eneo lao lina ukubwa wa heka moja na nusu unaofanya wasiwe na uwanja wa michezo. Hata hivyo amesema wamekuwa wakihakikisha kila wiki watoto wanashiriki michezo kwa kulipia uwanja wa JMK Youth Park.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ameshukuru kilio cha SMJ kusikika wizarani na kwamba wanaamini Naibu Waziri akitoka shuleni hapo, vikao vitakavyofanyika wizarani vitatumia busara katika kuridhia ombi la usajili na kukidhi kiu ya wanafunzi walio nao shuleni hapo kuweza kupata elimu.

Hata hivyo, Turky amesema wanaamini ombi la usajili wa shule yao litafanikiwa na iwapo ikitokea wakakataliwa, wataheshimu maamuzi ya Wizara na kwamba watawapeleka wanafunzi wao ambao wanafika 175 katika shule zilizosajiliwa.