Home Mchanganyiko WATUMISHI OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI WAASWA KUJIEPUSHA NA VITENDO...

WATUMISHI OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI WAASWA KUJIEPUSHA NA VITENDO VYA RUSHWA.

0

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa  kwa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa  Serikali na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU).

Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma kutoka TAKUKURU Bw. Joseph Mwaisalo ndiye aliyekuwa mwezeshaji wa mafunzo hayo akiwa amefuatana na  Bi. Stella Mpanju. Bw. Mwaisalo amesisitiza kwamba rushwa ni zaidi ya hongo na kuwataka watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kujiepusha na vitendo vya rushwa kutoka na unyeti wa Ofisi hiyo.

Washiriki wa Mafunzo hayo walikuwa ni Wakurugenzi, Wakurugenzi Wasaidizi, Wakuu wa Vitengo, Mawakili wa Serikali na  Watumishi wa Kada mbalimbali.

****************************************

Na Mwandishi Maalum, Dodoma

Imeelezwa kwamba, Ukiukwaji wa maadili, upendeleo, ubinywaji wa maslahi ya watumishi na watumishi kutopewa nafasi ya kutoa mawazo yao, ni baadhi ya mambo yanayoweza kupelekea uwapo wa vitendo vya
kutoa na kupokea rushwa sehemu ya kazi.

 

Hayo yameelezwa leo (Ijumaa) na Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rush(TAKUKURU) Bw. Joseph Mwaisalo, wakati alipokuwa akitoa mafunzo kuhusu uzuiaji na kupambana na rushwa kwa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali.

 

Mafunzo hayo na ambayo yalifunguliwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, DkT. Evaristo Longopa,yamewahusisha watumishi wote kuanzia
Wakurugenzi wa Idara, Wakurugenzi Wasaidizi, Wakuu wa Vitengo,

 

Mawakili wa Serikali na watumishi wa Kada Mbalimbali waliopo Jijini Dodoma.

 

“ Rushwa ni zaidi ya hogo”. Anasema Bw. Joseph Mwaisalo. Na kuongeza. “Rushwa ni mmomonyoko wa maadili, mtumishi anaponyimwa haki yake ya kupandishwa cheo, au stahili yoyote ile ambao ni haki yake inatengeneza mazingira ya rushwa.

 

Na kwa sababu hiyo, amewataka watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali siyo tu kuhakikisha wanazuia uwepo wa mianya ya utoaji na upokeji wa rushwa lakini ni vizuri kwao pia kuzitambua haki zao, kuzidai kwa misingi ya sheria, taratibu na kanuni na kwa
Menejimenti kuhakikisha kwamba inazingatia maslahi ya watumishi wake.

 

Akasema, watumishi wengi na hata wananchi waliowengi hawazijui haki zao na namna halali ya kuzidai haki zao na ndio maana wengi wao wanaishia kuombwa rushwa ikiwamo rushwa ya ngono.

 

“Rushwa ipo kila mahali, hata hapa katika Ofisi ya Mwanasheria kunauwezekano wa kuwapo kwa mazingira ya rushwa kupitia utekelezaji wa majukumu yenu hasa mkizingatia kwamba hii ni Taasisi nyeti sana na ambayo ni mdau wetu mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa”.
Anasisitiza Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma.

 

Akasema kutokana na unyeti wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na umuhimu wake kwa Taifa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jeneral John J. Mbungo, ameguswa sana na uamuzi wa Taasisi hii muhimu wa kuwa na mafunzo haya ya kuelimishna juu ya kuzuia na
kupambana na rushwa kwa watumishi wake.

 

Bw. Mwaisalo ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha kwamba, katika utekelezaji wa majukumu yake yakiwamo ya upekuzi wa mikataba, uandishi wa sheria, utoaji wa ushauri wa kisheria, hakuna mianya ya rushwa.

 

Akasema,Takukuru inaridhishwa sana na taarifa za kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itafanya kazi na kufuatilia kwa karibu michakato ya uandishi wa sheria ndogo ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwamba baadhi yake zinaviashiria vya rushwa , utoaji wa hongo na ukandamizaji.

 

“Niwasihi pia kwamba, hata katika Sheria nyingine na Mikataba mbalimbali, muendelee kuisaidia serikali kwa kubaini mianya au viashiria vya rushwa”.

 

Bw. Mwaisalo alizungumzia pia kwa kina kuhusu madhara ya rushwa ya ngono na akawataka wanawake na wasichana katika nafasi zao mbalimbali kujiamini kwamba wanaouwezo mkubwa na haki ya kupata
haki yao ikiwamo ajira pasipo kutoa rushwa ya ngono ambayo ameitaja kuwa ni udhalillishaji wa hali ya juu.

 

“Rushwa ya ngono ni udhalilishaji wa hali ya juu, mwanamke au msichana unauwezo na haki ya kuikataa, mjiamini. Rushwa ya ngono ni matokeo ya mmomonyoko wa maadili na inatakiwa kupingwa kuanzia katika ngazi ya familia zetu. Na viogozi ni muhimu mtambue kwamba
uongozi ni dhamana na si vinginevyo”.

 

Awali akifungua mafunzo hayo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa. Amesema, kufanyika kwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango kazi ambao Ofisi imejiwekea.

 

Akasisitiza kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama Taasisi ya Umma inayowajibu na inawajibika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa.

 

“Ni kwa sababu hiyo, tumeandaa mafunzo haya kwa kushirikiana na TAKUKURU ili tuwezeshwe na kukumbushwa kwa kupewa elimu na kufundishwa kuhusu kanuni, taratibu na sheria zinazohusiana na mapambano dhidi ya rushwa”. Akasema Naibu Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Na kusisitiza “ Niwaombe watumishi wenzangu tujiepushe na yale ambayo yanaweza kututia matatizoni kwa sababu tu ya kutozingatia kanuni, taratibu na sheria”.