***************************************
Na Mwandishi Wetu, Mara
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (Namba Tatu) amesema makada wanaoendelea kuvunja kanuni za chama kwa kuanza kutangaza nia kabla ya wakati watashughulikiwa kwa kuwa mbali na kuvunja kanuni za chama pia wanaifanyia hujuma Serikali iliyopo madarakani chini ya Rais Dkt.John Magufuli.
Kiboye alirejea msimamo huo jana baada ya kuutoa hivi karibuni mjini Butiama, Mara wakati wa sherehe fupi ya maadhimisho ya miaka 90 ya Mama Maria Nyerere ambaye ni mke wa Rais wa Kwanza, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
“Miongoni mwetu kuna watu au makada ambao hawasikii kabisa, badala ya kuheshimu kanuni na Katiba ya chama wameendelea kuivunja kwa kutangaza nia ya kuwania nafasi mbalimbali ikiwemo ubunge mkoani hapa.
“Naomba walifahamu na walielewe ili kwamba, kuvunja kanuni za chama ni miongoni mwa sababu kubwa za utovu wa nidhamu na kukidharau chama, hivyo hatuwezi kuwavumilia na hatutamuogopa mtu iwe ni kada ambaye ana cheo kikubwa, kwa kuwa muda wa kufanya hivyo bado na kuna taratibu zitapaswa kufuatwa wakati ukifika,” alifafanua Kiboye.
Aliongeza kuwa, muda ukifika vikao vya chama ndiyo vitakavyoamua ni nani ambaye anapaswa kuwania nafasi ipi ikiwa anakidhi vigezo vitakavyoainishwa muda ukifika.
“Vinginevyo wanaoendelea kujitangaza watambue wanapoteza muda wao na lazima hatua kali zitachukuliwa dhidi yao,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Kiboye alichukua nafasi hiyo kuwataka Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kuliletea Taifa maendeleo.
Alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli kwa miaka michache imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya kimkakati ambayo inalifanya Taifa kuweka rekodi ndani na nje ya Bara la Afrika.
“Uthubutu tu wa kuamua kujenga bwawa kubwa la Umeme la Julius Nyerere ambalo litazalisha Megawatt 2115 katika maporomoko ya Mto Rufiji ifikapo 2022 ni mafanikio tosha kwa Taifa letu.
“Huu ni mradi ambao utaliwezesha Taifa kuwa na nishati ya kutosha ya Umeme, pia ziada tutaiuza nje ya nchi, hivyo kupata fedha nyingi za kigeni kwa ajili ya kukuza miradi mingine ya maendeleo, kwa msingi huu tuendelee kumuunga mkono Rais wetu mpendwa na kumuombea kwa Mungu muda wote, anafanya mambo makubwa mno,”alifafanua Kiboye.
Pia aliongeza kuwa, Taifa limepiga hatua katika utoaji wa elimu bure, utoaji wa huduma za afya kwa viwango vya juu, maji, barabara, nishati, kuhamishia huduma zote za Serikali makao makuu ya nchi jijini Dodoma.
Aidha, Kiboye alisema Serikali ya Awamu ya Tano imewezesha kurejesha nidhamu katika utoaji wa huduma kwa taasisi na mashirika yote ya umma, usafiri wa anga, madini,udhibiti wa maliasili, kuongezeka kwa ukusanyaji mapato na huduma nyingine nyingi.