Home Michezo MTATURU AKABIDHI ZAWADI WASHINDI MBUNGE KILIMO CUP

MTATURU AKABIDHI ZAWADI WASHINDI MBUNGE KILIMO CUP

0

HATIMAYE mashindano ya Mbunge Kilimo Cup yaliyofadhiliwa na mbunge wa Singida Mashariki Mhe Miraji Mtaturu yamefikia tamati kwa timu ya Mawakala FC kuibuka mabingwa katika mashindano hayo.

Mashindano hayo yalizinduliwa disemba 3 mwaka huu na kushirikisha timu nanenyenye lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye msimu wa kilimo chini ya kauli mbiu ya ‘Kilimo ni uti wa mgongo.

Akifunga mashindano hayo disemba 26 yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Ikungi Mhe Mtaturu aliwapongeza viongozi na wachezaji wa timu zote zilizoshiriki.

“Wachezaji wote niwapongeze kwa kujitoa kwenu,mmecheza vizuri kwa kiwango  na kila mmoja alipambana ili timu yake ishinde lakini mchezo siku zote hamuwezi kuwa washindi wote ni lazima apatikane mshindi mmoja,waratibu wetu wa mashindano hongereni sana,

“Niliamua kuanzisha mshindano haya kama chachu kwa wananchi kujiandaa kwa msimu wa kilimo kwa kufuata kanuni bora za kilimo na kupanda mbegu zilizoshauriwa na wataalam ili kujitosheleza kwa chakula, na kwa dhamira hii sasa twendeni shambani,”alisema Mtaturu.

Aliahidi kuendelea kufadhili mashindano kama hayo ili kuwaweka vijana pamoja ikiwa ni kudumisha upendo,undugu na mshikamano,na kuunga mkono juhudi za serikali za kupambana na upatikanaji wa ajira kwa vile anajua michezo ni ajira.

“Nimekubali kuitunza timu ya Ikungi Combine kwa kuwaletea kocha ili iwe fursa ya kuendeleza vipaji vya vijana”alisema.

Akitangaza washindi mratibu wa mashindano hayo Yasin Ntandu amesema Mawakala FC wameibuka washindi wa nafasi ya kwanza na kujinyakulia shilingi laki 200,000 na mpira baada ya kuwafunga Sokoni FC bao nne kwa tatu.

Ametaja nafasi ya pili kuwa imeenda kwa Sokoni FC ambao wamejinyakulia shilingi 150,000 na mpira na mshindi wa tatu ni Mbwanjiki waliopata  Shilingi 100,000 na mpira ambapo zawadi hizo ziliambatana pia za mchezaji mwenye nidhamu,mfungaji bora na golikipa bora.

“Mbunge wetu Mtaturu aliamua kufadhili mashindano haya ili kuwaweka vijana ’,tunakushukuru mbunge kwa kukubali kuwa mfadhili na kutoa zawadi kwa washindi ikiwemo fedha taslimu na vifaa vya michezo kwa kila timu iliyoshiriki,”alisema Ntandu.

Mwenyekiti wa CCM wilaya Mika Likapakapa amempongeza mbunge kwa kuwa mdau muhimu wa maendeleo kwenye wa wilaya ikiwemo michezo na kumuomba aendelee kuandaa mashindano zaidi ili kuweweka vijana pamoja.

Timu nyingine zilizoshiriki mashindano hayo ni Matare,Nkuhi,Tanesco,Dung’unyi na Issuna.