Home Michezo MCHEZAJI  WA KMC ASAINI MIAKA MITATU KUJIUNGA NA STELLENBOSCH YA LIGI KUU...

MCHEZAJI  WA KMC ASAINI MIAKA MITATU KUJIUNGA NA STELLENBOSCH YA LIGI KUU AFRIKA KUSINI

0

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
KIUNGO mkabaji chipupizi wa Tanzania, Ally Msengi amesajiliwa na klabu ya Stellenbosch ya Ligi Kuu Afrika Kusini kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Kinondoni Municipal Council (KMC) ya Dar es Salaam.
Mratibu wa kampuni ya Siyavuma Sports Group, Michael Mwebe ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Msengi alizivutia klabu kadhaa za Afrika Kusini kabla ya kuamua kumwaga wino Stellenbosch baada ya kocha wa klabu hio kuonesha imani kubwa ya kumpa nafasi katika kikosi chake.
Msengi ambaye amezichezea timu zote za vijana za taifa kuanzia U17 na 20 anatarajiwa kuanza rasmi maisha mapya Katika Ligi Kuu Afrika Kusini Jumapili ya keshokutwa.

“Msengi anaanza ukurasa mpya baada ya kufanya vizuri akiwa na klabu ya KMC aliyoichezea kwa takriban msimu mmoja na nusu. Tunaushukuru uongozi wa KMC kwa ushirikiano mkubwa tangu alipotua hapo na pia kumpa baraka zote za kuondoka klabu kwa ajili ya kucheza soka nje ya mipaka ya Tanzania. 
Siyavuma inaendelea kuamini katika vipaji vya vijana wa Tanzania, Msengi akiwa muendelezo wetu wa kuwapatia fursa ya kucheza soka la nje ya nchi. Ikumbukwe tulianza na Abdi Banda tuliyemtoa Simba na kumpeleka Baroka, baadaye Himid Mao, Eliud Ambokile, Yahya Zaydi na sasa Msengi” amesema Mwebe.