Home Mchanganyiko DKT.BASHIRU AMETOA MAELEKEZO KWA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA KUHAKIKISHA VIBARUA WANALIPWA...

DKT.BASHIRU AMETOA MAELEKEZO KWA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA KUHAKIKISHA VIBARUA WANALIPWA KWA WAKATI

0

******************************************

Bukoba. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dkt Bashiru Ally ametoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhakikisha wale waliofanya kazi za ufundi, vibarua, wahudumu na kazi zingine katika miradi mbalimbali ya serikali wanalipwa kwa wakati hasa kwa miradi ambayo serikali tayari ilishatoa fedha hizo.

Dkt Bashiru amesema, kwa wale wasimamizi wa miradi hiyo ambao wamekula fedha na kushindwa kuwalipa wafanya kazi kwa wakati, wakuu wa mikoa na wilaya wasisite kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na warudishe fedha hizo ili jasho la wananchi wanyonge lisipotee.

Bashiru ametoa maagizo hayo Desemba 27, 2019 alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya halmashauri ya Bukoba vijijini, ambapo licha ya kuridhishwa na ujenzi huo lakini amekuwa akipokea malalamiko mbalimbali ya wafanayakazi kutokulipwa kwa wakati licha ya fedha zote shilingi bilioni 1.5 kufikishwa hospitalini hapo.

’’Natoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya na mikoa nchi nzima, kuhakikisha wanalinda miradi hii dhidi ya wadokozi na wezi wa rasilimali hizi za wananchi, na wale wote waliotoa jasho lao kujenga mradi huu, yaani mafundi, vibarua, wahudumu na wafanya kazi wengine, walipwe kwa wakati na jasho la mwananchi lisipotee, kama kuna waliohusika katika kuchelewesha malipo yao, wachuliwe hatua kali za kinidhanu kwa mujibu wa sheria za nchi.” Katibu Mkuu amesisitiza.

Aidha, Bashiru ametoa wito kwa wenyeviti wote wa vijiji na mitaa nchi nzima kutoa ardhi kwa shughuli za jamii ikiwemo ujenzi wa Hospitali, Shule, Ofisi za umma, n.k kama ambavyo imefanyika katika kijiji cha Kanazi kwa wananchi kujitolea eneo ambalo ujenzi wa hospitali hiyo ya halmashuri unaendele, ambapo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za ujenzi wa mradi huo.

“Nawashukuru sana wanakijiji cha Kanazi kwa kujitolea eneo hili kwa ujenzi wa Hospitali hii ya Halmashauri, na ninatoa rai kwa wenyeviti wote wa aserikali za mitaa na vijiji toeni ardhi kwa matumizi kama haya, na mfano huu wa kijiji cha Kanazi uigwe nchi nzima.’’

Ambapo ameongeza kuwa, utaratibu wa kugawa ardhi za vijiji ni lazima uwe shirikishi na ufanywe na mkutano kuu wa kijiji au mtaa na si wajumbe wa halmshauri ya kijiji pekee ili kupunguza migogoro na kuweka maamuzi kuwa ya uwazi kwa wananchi wote kama ilivyofanyika kijiji cha Kanazi.

wakati huo huo, Dkt Bashiru ametumia fursa hiyo kuwataka wanachi kuendelea kuiamini CCM na serikali yake chini ya Mhe. Dkt John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, ambapo ameweza kudhibiti nidhamu katika serikali na Chama, na mafanikio yanayopatikana sasa ya ujenzi wa Hospitali nchi nzima, vituo vya afya, zahanati, Barabara, Madaraja, Umeme, miradi ya maji n.k ni matokeo ya jitihada hizo.

Halmashauri ya wilaya ya Bukoba ni miongozni mwa halmashuri tatu za mkoa wa Kagera zilizopokea fedha za ujenzi wa hospitali za wilaya, nyingine ni karagwe na Kyerwa

Awali, Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Bw. Deodatus Kinawilo akimkaribisha Katibu Mkuu, ameeleza namna serikali ya wilaya, ilivyoridhidhwa na maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo ambapo licha ya changamoto mbalimbali ikiwemo hali mvua kwa muda mrefu ujenzi uliendelea na sasa kufikia hatua ya umaliziaji.

Katika hatua nyingine Bashiru amezitaka kamati za siasa za wilaya nchi nzima kuhakikisha ifikapo tarehe 15 Januari, 2020 kuwa tayari wamekamilisha mchahakato wa kukusanya maoni yatakayosaidia katika uandishi wa ilani mpya ya uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025 ikiwa ni maelekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa, kwa ilani kuwa shirikishi na jumuishi ambapo italenga zaidi katika kuvifanya vijiji kuwa ndio vitovu vya maendeleo nchini.

Katika ziara hiyo, viongozi na wananchi mbalimbali walikuwepo wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ndg. Evarist Babyegaya, Mkuu wa wilaya Bw. Deodatus Kinawiro na wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya.

Katibu Mkuu yupo nyumbani kwake, Kagera wilayani Bukoba kwa mapumziko ya siku kumi, ambapo anatarajiwa kumaliza mapumziko hayo mwazoni mwa mwezi Januari, 2020.