Home Mchanganyiko WASIOUNGANISHA UMEME KUCHUKULIWA HATUA-DKT KALEMANI

WASIOUNGANISHA UMEME KUCHUKULIWA HATUA-DKT KALEMANI

0

Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chemkeni mara baada ya kuwasha umeme kijijini humo.

Wananchi wa kijiji cha Chemkeni wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani alipokuwa akiwahutubia kijijini humo.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( mwenye shati la bluu) pamoja na viongozi mbalimbali wakielekea kuwasha umeme kwenye shule iliyopo kwenye kijiji cha Chemkeni.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akikata utepe kuashiria kuwasha kwa umeme katika kijiji cha Chemkeni.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na viongozi mbalimbali wa Wilaya na Wizarani wakiwa katika kituo cha kupoza umeme cha Uhuru.

**********************************

Hafsa Omar – Tabora

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani amesema Serikali itaanza kuchua hatua kwa wananchi wote ambao hawataunganisha umeme kwenye nyumba zao, ambao wanauwezo wa kulipia 27,000.

Ameyasema hayo, Desemba 22, 2019 katika kijiji cha Chemkeni kilichopo, kata ya Igwisi, Wilaya ya Kaliua, Mkoani Tabora, wakati alipokuwa akifanya ukaguzi wa nyumba ambazo hazijaunganishwa umeme kijijini humo.

Amesema, Hatua ambazo zitachukuliwa ni pamoja na kupigwa mnada mifugo ambayo wanamiliki na kulazimishwa kuunganishiwa umeme kwenye nyumba zao.

Alieleza kuwa Serikali inatumia gharama kubwa kuhakikisha umeme unafika nchi nzima, kwahiyo asingependa kuona wananchi hawatumi fursa hii ya kuweka umeme kwenye nyumba zao tena kwa gharama nafuu.

Aidha, Dkt. Kalemani alichukizwa na kitendo cha baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, kukataa kuweka umeme kwenye nyumba zao kwa madai ya kwamba wanasubiri kufungua biashara ambazo zitawalazimu kuunganisha umeme.

“Haiwezekani Serikali ilete bilioni 36 kwenye Mkoa huu, halafu mkatae kutumia umeme lazima tuanze kuwachukulia hatua na itafika mahala tutatumia nguvu kwa wananchi ambao hawataki kuweka umeme na nitarudi hapa mwakani kufuatilia nyumba kwa nyumba” alisema.

Waziri Kalemani, amewaagiza TANESCO kuendelea kuwahamasisha wananchi kulipia huduma ya umeme ili wananchi wapate hamasa ya kuweka umeme kwenye nyumba na taasisi za umma ambazo zipo karibu na maeneo yao.

Katika ziara yake mkoani humo, Waziri wa Nishati, aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kaliu Abel Busalama, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali, pia aliwasha umeme katika vijiji vya Ilege,Chemkeni vilivyopo wilayani Kaliua na kukagua ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Uhuru kilichopo wilaya ya Urambo.