Home Mchanganyiko TUME YA NGUVU ZA ATOMIKI TANZANIA YAZIFUNGIA HOSPITALI 95 KWA KIPINDI CHA...

TUME YA NGUVU ZA ATOMIKI TANZANIA YAZIFUNGIA HOSPITALI 95 KWA KIPINDI CHA MWAKA JANA

0
Mkurugenzi wa Tume ya nguvu za Atomiki Tanzania ,Profesa Lazaro Busagala akizungumza katika ufungaji wa mafunzo ya udhibiti na usalama wa mionzi katika maeneo yao ya kazi .
Happy Lazaro
……………..
Happy Lazaro, Arusha
Arusha.TUME ya nguvu za Atomiki Tanzania imezifungia hospitali 95 kwa kipindi cha mwaka Jana kuanzia  julai 2018 hadi June 2019 kutokana na kukosa sifa mbalimbali ikiwemo ya kutokuwa na wafanyakazi wenye sifa stahiki .
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Tume ya nguvu za Atomiki Tanzania,Profesa Lazaro Busagala wakati akizungumza katika ufungaji wa mafunzo ya udhibiti na usalama wa mionzi katika idara za Radiolojia nchini.
Aidha mafunzo hayo yamewashirikisha watumishi wanaofanya kazi katika idara ya Afya wapatao 104 kutoka mikoa yote nchini lengo kuu likiwa ni kupatiwa mafunzo namna ya udhibiti na usalama wa mionzi katika maeneo yao ya kazi.
Profesa Busagala amesema kuwa,kwa kipindi cha mwaka Jana walikagua jumla ya hospitali 664 ambapo hospitali 105 zilifungiwa na katika hizo hospitali 10 zilifanikiwa kukidhi viwango na kufunguliwa ,hivyo hadi sasa hivi hospitali 95 bado zimefungiwa.
Amesema kuwa,tayari kwa mwaka huu wameshaanza ukaguzi katika hospitali mbalimbali ambapo hadi sasa hospitali 3 zimefungiwa kuwa na huduma za Radiolojia.
Ameongeza kuwa,Tume hiyo inatekeleza kwa vitendo matakwa ya sheria ya Atomiki ya mwaka 2003 , sehemu ya 11 idara ya 5 (N na O)ambayo inaitaka Tume kutoa mafunzo kwa watumiaji wote wa teknolojia ya mionzi nchini na kuwadhibiti wanaopata mafunzo kwa kuwapa vyeti .
Profesa  Busagala ameongeza kuwa, wanataka kuhakikisha mtu yeyote anayetumia mionzi ahakikishe  anakuwa na utalaamu  wa kutosha juu ya matumizi  na namna ya kutumia mionzi hiyo ili isiweze kuumiza wengine ama kuleta madhara kwa jamii husika.
“naombeni Sana tuwe na ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha majukumu yetu tumeyafanya kwa umakini ili kuokoa maisha ya watanzania wasidhurike na mionzi na kuepuka matumizi holela ya mionzi ‘amesema Profesa Busagala.
Kwa upande wake  Kaimu Mkurugenzi wa teknolojia na ufundi wa TAEC ,Firmi Banzi amesema kuwa,lengo la kutoa mafunzo hayo  kila  mwaka ni kutaka kuhakikisha  watumiaji wa  mionzi wote wamekuwa na uelewa wa  kutosha juu ya matumizi sahihi ya mionzi kwa faida ya jamii .
Aidha amewataka wataalamu katika idara hiyo ya mionzi kuhakikisha wanatumia weledi katika utendaji kazi wao katika kuhakikisha watanzania wanabaki salama pindi wakienda hospitali ili wasirudi na magonjwa yanayowasumbua.
“Tunataka kuhakikisha mtu yeyote anayetumia vyanzo vya mionzi anatumia kwa usalama na sio kuumiza jamii ,kila anayetumia lazima awe na utalaamu wa  kutosha na ndio maana tumekuwa tukitoa mafunzo haya kila mwaka.”amesema Banzi.
Naye  Mtaalamu mkuu wa mionzi mkoa wa Pwani,Faustine Mulyutu wameomba kupatiwa barua za kuwatambua ili waweze kuwa wasimamizi katika idara hizo za mionzi katika maeneo yao ya kazi,kwani changamoto kubwa iliyopo ni kutokuwa kwa mtiririko mzuri wa utumishi katika mambo ya mionzi kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya.