Home Mchanganyiko TGT YATOA MAFUNZO YA JINSI YA KUINUA BIASHARA NA KUKUZA MITAJI KWA...

TGT YATOA MAFUNZO YA JINSI YA KUINUA BIASHARA NA KUKUZA MITAJI KWA WAJASIRIAMALI MKOANI PWANI

0

*****************************

NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
WANAWAKE wajasiriamali mkoani Pwani, wameitaka serikali kuangalia uwezekano wa kuzifungia kutoa huduma baadhi ya taasisi za mikopo zinazotoa  mikopo kwa masharti magumu ikiwa ni pamoja na kuwataka wakopaji kuweka dhamana samani za majumbani ili wakopeshwe.

Walieleza hayo, wakati wa mafunzo ya ujasiriamali yaliyoandaliwa na taasisi ya uwezeshaji na huduma za fedha kwa watu wenye ulemavu,wanawake na vijana ya TGT yenye Makao yake Makuu Jijini Dar es salaam.
Mariam Nzige na katibu wa Jukwaa la uwezeshaji  kiuchumi Wanawake Mkoani Pwani Elina Mgonja walisema ,masharti hayo ni magumu hasa ukizingatia kipindi cha ugumu wa maisha na wakati mwingine kuyumba kwa biashara zao.

“Tunatambua wajibu wa mtu kukopa dawa ya deni ni kulipa lakini kuna wakati biashara zinayumba ambapo mkopaji unaenda kutoa taarifa sehemu ulikokopa ili uongezewe muda wa marejesho lakini hali hiyo imekuwa inakataliwa na badala yake wanakuja kukunyang’anya vyombo”alisema Elina.
Kwa upande wake ,Tumaini Shao aliishukuru  taasisi hiyo kwa kuwapa mafunzo ya namna ya kusindika bidhaa mbalimbali hali ambayo imewawezesha kuzalisha bidhaa hizo kwa ufanisi ukilinganisha na kipindi cha nyuma kabla ya kupata mafunzo hayo.
Mgeni rasmi kwenye mafunzo hayo Katibu Tawala Msaidizi ,Mipango na Uratibu Mkoani Pwani ,Edward Mwakipesile  alisema serikali mkoani humo inatarajia kuendesha msako ili kubaini taasisi zinazojihusisha kutoa mikopo kwa wajasiriamali ,ambazo zinajiendesha bila kuwa na ofisi wala usajili kamili .
Alieleza kinachofuata ni kuzichukulia hatua za kisheria taasisi zilizoanzishwa bila kufuata taratibu badala ya kunufaisha jamii.
Awali mtendaji mkuu wa Taasisi ya TGT- Anna Lyimo alisema,  kwa kipindi cha miaka 27 wameanza kutoa huduma hapa nchini huku akidai wameweza kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuwasaidia wafanyabiashara,wajasiriamali wa makundi yote kukuza mitaji yao.