Home Mchanganyiko WAZIRI WA AFYA AIOMBA NMB KUENDELEA KUCHANGIA HUDUMA ZA AFYA

WAZIRI WA AFYA AIOMBA NMB KUENDELEA KUCHANGIA HUDUMA ZA AFYA

0

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vitanda vya wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalumu (PICU) ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, vitanda hivyo vimetolewa na Benki ya NMB.

Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi MNH Bi. Zuhura Mawona akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Mwakilishi wa Benki ya NMB Bw. Juma Kamoli akikabidhi rasmi vitanda hivyo kwa Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy Mwalimu akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Madaktari na Wauguzi wa wodi ya watoto wenye kuhitaji uangalizi maalumu (PICU),pamoja na wawakilishi wa Benki ya NMB.

………………..

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ameziomba sekta binafsi ikiwamo benki ya NMB kuelendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo wakati akipokea msaada wa vitanda vitano kutoka Benki ya NMB vyenye thamani ya shilingi milioni 35 kwa ajili ya wodi ya watoto wanaohitaji huduma ya uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na vitanda 10 pamoja na magodoro 10 kwa Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila vyenye thamani ya shilingi milioni 10. 

Amesema sekta ya binafsi ina wajibu mkubwa katika kuchangia shughuli za maendeleo ikiwamo huduma za afya kama ilivyofanya Benki ya NMB.

“Nawapongeza NMB kwa jitihada zake kwani msaada vitanda vya ICU ni msaada mkubwa kwa watoto na pia NMB inafanya vizuri kurejesha fedha zake kwa jamii,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Pia, Waziri Ummy amesema kutokana na juhudi za Serikali ya awamu ya tano, Muhimbili inaendelea kutoa huduma za ubingwa wa juu ikiwamo huduma ya kupandikiza figo, huduma ya kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto wenye matatizo ya kusikia.

Naye mwakilishi wa Benki ya NMB, Bw. Juma Kimori ameipongeza Muhimbili na serikali ya awamu ya tano kwa kuboresha huduma za afya.

Bw. Kimori amesema NMB imeweka utaratibu kutoa misaada katika sekta ya afya kwa kutenga fedha kwa ajili ya kutoa misaada mbalimbali kwa jamii.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi MNH, Bi. Zuhura Mawona ameishukuru NMB kwa msaada huo kwa kuwa umekuja wakati ambapo MNH kwa kushirikiana na wahisani imejenga wodi za uangalizi maalumu kwa watoto wenye umri kati ya siku 1 hadi siku 28 (NICU) na wenye umri wa siku 29 hadi miaka 14 (PICU), hivyo kuwa na uhitaji wa vitendea kazi mbalimbali ikiwemo vitanda.

 “Vitanda hivi vya kisasa vinatumia umeme na vinaweza kurekebishika kwa kupandishwa juu na kushushwa  kulingana na uhitaji, hivyo vinasaidia mgonjwa kulazwa katika mlalo unaofaa na pia kupunguza maumivu ya mgongo kwa wauguzi na madaktari wakati wa kutoa huduma,”amesema Bi. Zuhura.

Bi zuhura amesema kuwa vitanda hivyo pia vimesaidia wauguzi kutoa huduma kwa urahisi na ufanisi zaidi ikiwamo kumwezesha mgonjwa kupumua (Intubation) kwa urahisi.

Pia. Bi. Zuhura ameshukuru NMB kwa kutoa msaada huu na pia ameiomba kuongeza vitanda vingine kwani mahitaji ya vitanda ni makubwa kwa watoto wanaohitaji uangalizi maalumu.