
Katibu Mkuu idara kuu ya maendeleo ya jamii,Dokta John Jingu akifungua sanduku la kuhifadhi fedha kwa ajili ya kikundi Cha wanawake Cha Tuinuane Kama ishara ya uzinduzi rasmi wa kikoba hicho wilayani Monduli jana pembeni yake ni wanawake hao wakishangilia uzinduzi huo.
Happy Lazaro
……………..
Happy Lazaro,Arusha
Katibu Mkuu idara kuu ya maendeleo ya jamii,Dokta John Jingu amevitaka vyuo vya maendeleo ya jamii nchini kutoa elimu ambayo itakuwa ni nyenzo na silaha ya kupambana na changamoto zilizopo katika jamii na kuweza kuleta matokeo chanya.
Amesema hayo Jana wakati alipotembelea chuo Cha maendeleo ya jamii Monduli,sambamba na kujionea miradi mbalimbali ya wananchi iliyofanikishwa na chuo hicho .
Amesema kuwa,wamekuwa wakisisitiza kwa vyuo hivyo kuhakikisha wanatoa elimu ambayo itakuwa ni silaha ya utatuzi wa changamoto mbalimbali katika jamii ili uwepo wa vyuo hivyo uweze kutambulika kwa vitendo zaidi.
Ameongeza kuwa,ni wajibu wa wanafunzi katika vyuo hivyo kutambua kuwa wanapohitimu wasifikirie kwenda kuwa maafisa wa serikali ama wizarani au kwenye mashirika badala yake wabadili mtazamo na kufikiri kwenda kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii.
“unajua unaposema upo chuo unasomea kozi fulani mjue kabisa elimu sio sifa tu ama cheti bali jamii yenyewe inatakiwa ikutambua kwa kazi zako unazozifanya kwani ndizo zitaweza kukutambulisha kwa jamii katika kuhakikisha elimu uliyoipata italeta majibu kwenye matatizo yaliyopo.”amesema
Hata hivyo Katibu amefurahishwa na miradi mbalimbali ya kijamii iliyoanzishwa na chuo hicho ambayo bado wananchi wanaendelea kuitekeleza ambayo imewasaidia Sana kujikwamua kiuchumi .
Naye Kaimu Mkuu wa chuo hicho,Elibariki Ulomi amesema kuwa,wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jamii inayowazunguka ikiwemo ufugaji wa kuku,ng’ombe,ambayo imewasaidia kwa kiasi kikubwa Sana kujikwamua kiuchumi.
Amesema kuwa,chuo hicho kimekuwa kikitekeleza kwa vitendo elimu wanayoitoa chuoni hapo ambapo wameweza kuibadili jamii hiyo ya wafugaji kwa kusaidia miradi mbalimbali ya ujasiriamali sambamba na kutoa elimu namna ya kuhifadhi fedha zao wenyewe na kuweza kukopeshana.
Wakizungumzia namna walivyonufaika na chuo hicho wanakikundi cha Tuinuane kilichopo Monduli juu ,wamesema kuwa,chuo hicho kimeweza kuwapatia mafunzo mbalimbali namna ya ufugaji bora wa kisasa wa ng’ombe na kuku ambapo wameweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mradi huo na kuondokana kuwa tegemezi.
Katibu wa kikundi hicho ,Anna Losiloyi amesema kuwa,kikundi hicho kina jumla ya wanachama 30 ambapo wameweza kuwa na kuku Mia moja na ng’ombe mmoja huku wakijishughulisha na biashara ya kushona shanga pamoja na bangili ambazo wamekuwa wakiwauzia watalii na kuweza kutunisha kikundi chao.
Aidha kikundi hicho kimefika mbali zaidi kwa kumwomba Katibu Mkuu kuwazindulia rasmi kikoba ambacho kitawasaidia kuweka fedha zao ili waweze kukopeshana .