Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye kipaza sauti) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Liuli wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma, alipofika kuwawashia rasmi umeme, Desemba 11, 2019.
**************************************
Veronica Simba – Ruvuma
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amewataka baadhi ya wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri za wilaya ambao wamekuwa wakilalamika kuwa taasisi za umma katika maeneo yao hazina umeme, waachane na malalamiko, badala yake watenge fedha za kulipia huduma hiyo ili wapatiwe umeme.
Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti Desemba 11, 2019 akiwa katika ziara ya kazi wilayani Nyasa na Songea, mkoani Ruvuma.
Dkt Kalemani alieleza kuwa, uzoefu alioupata katika ziara zake sehemu mbalimbali nchini unaonesha kuwa sababu ya taasisi nyingi za umma kutounganishiwa umeme ni viongozi wake kutolipia huduma hiyo.
Alisema, wengi wamekuwa wakilalamika, lakini serikali inapofuatilia inagundua kuwa taasisi husika hazijalipia huduma hiyo.
“Wengi wao wanatenga fedha za ujenzi wa taasisi lakini wanasahau kutenga bajeti ya umeme halafu wanalalamika.”
Akitoa hamasa zaidi kwa viongozi hao kutekeleza maelekezo yake, Dkt Kalemani aliwataka watumie fursa iliyotolewa na serikali vijijini, ambapo gharama za uunganishaji umeme zimeshushwa.
“Hata taasisi zitakazounganishwa kwa mfumo wa njia tatu (three phase), bado gharama yake ni ndogo sana ukilinganisha na inayotozwa mjini. Badala ya kulipia mamilioni, utalipia laki na sehemu tu hivyo changamkeni.”
Katika ziara hiyo, Waziri aliwasha umeme katika vijiji vya Liuli na Kihagala vilivyoko wilayani Nyasa pamoja na vijiji vya Liganga na Nguvumoja vilivyoko wilaya ya Songea.
Aidha, pamoja na mambo mengine, alisisitiza umuhimu wa taasisi za umma na miradi mbalimbali ya maendeleo kupewa kipaumbele katika kuunganisha umeme ili ziweze kuwahudumia vema wananchi.
Waziri aliwapongeza viongozi wa maeneo hayo wakiwemo wabunge Stella Manyanya (Nyasa) na Jenista Mhagama (Peramiho) pamoja na Wakuu wa Wilaya husika, Madiwani na wengine ngazi ya halmashauri na vijiji, kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya umeme bila kuchoka ili kuhakikisha wananchi wao wanafikiwa na nishati hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi hao, akiwemo Mbunge wa Nyasa Mhandisi Manyanya pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo, Isabela Chilumba, wameipongeza Serikali kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme inayolenga kuboresha maisha ya wananchi, hususan walioko vijijini.