Home Mchanganyiko Wakala wa Vipimo Waadhimisha Miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika, kwa ...

Wakala wa Vipimo Waadhimisha Miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika, kwa Kufanya Ukaguzi wa Kustukiza

0

Afisa Vipimo namba Moja kutoka Wakala wa Vipimo nchini, Bw.Mohammed
akitoa maelezo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu matumizi ya
kifaa cha kupimia vipimo vya kuuzia nyama, mara baada ya Kufanya ukaguzi wa
Kustukiza katika mabucha ya Mwenge Jijini Dar es Salaam mapema leo Desemba
09, 2019.

Kaimu Meneja Wakala wa Vipimo Mkoa wa Temeke, Bw.Krishna Mahamba,
akieleza jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu umuhimu wa kutumia mizani iliyosawa kwa wauzaji wa mabucha , mara baada ya Kufanya
ukaguzi wa Kustukiza katika mabuchani yaliyoko Mwenge Jijini Dar es Salaam
mapema leo Desemba 09, 2019.

Mmoja ya Wauzaji wa mabucha yaliyoko Mwenge Jijini Dar es Salaam, Petro
Makole, akieleza jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu
umuhimu wa kutumia mizani iliyosawa kwa wauzaji wa mabucha , mara baada ya Kufanyiwa ukaguzi wa Kustukiza buchani kwake Mwenge Jijini Dar es Salaam mapema leo Desemba 09, 2019.

*************************************

Na. Mwandishi Wetu-MAELEZO.

Wakala wa Vipimo Nchini (WMA) imesema kuwa itaendelea kulinda maslahi ya
watumiaji na afanyabiashara kupata stahiki sahihi katika manunuzi na uuzaji wa
bidhaa zao kwa kutumia vipimo vinavyoendana na thamani ya pesa inayolipwa na mteja.

 

Akizunngumza Jijini Dar es Salaam katika ziara ya Kustukiza kwa Wafanyabiashara wa Mabucha, Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Temeke, Krishna Mahamba amesema kuwa dhumuni la ziara hiyo ni kuangalia kama vipimo vinazingatiwa na wauzaji ili kuleta usawa kwa wateja na wauzaji hao.

 

“Katika kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika, Wakala wa Vipimo leo
tumeamu kufanya zoezi hili ambalo linafanyika Nchi nzima ili kulinda haki za
biashara kwa wateja na wauzaji kwenye mabucha haya, kwani mara nyingi katika siku za sikukuu kama hizi wauzaji huwa wanachezea vipimo”, Krishna Mahamba Kaimu Meneje (WMA) Mkoa wa Temeke.

 

Alieleza kuwa wafanyabiashara wa mabucha wanapaswa kutumia mizani
iliyopimwa ili kumuwezesha mpata huduma katika mabucha yao kupata bidhaa
kulingana na thamani ya pesa yake na kuweza kuleta usawa pande zote mbili
yaani mteja na muuzaji.

 

Naye Kaimu Meneje Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kinondoni, Charles Mavunde
alisema kuwa leo wakala wa vipimo imefanya zoezi hilo ili kuangalia kama
wafanyabiashara wa Mabucha wanazingatia Sheria ya Vipimo nchini Sura namba
340 ambayo inamtaka mfanyabiashara kutumia vipimo sahihi kulingana na bei ya bidhaa yake aliyoipanga kwa wanunuzi.

 

Mavunde alito wito kwa watanzania kuwa wanapokuwa wanaadhimisha sikukuu
kama ilivyokuwa leo miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika wawe makini na
wafanyabiashara katika sehemu zote za biashara kuanzia kwenye mabucha, sokoni na kwenye vituo vya mafuta kwa kuwa siku hizo wafanyabiashara huchezea vipimo na kutoa bidhaa kwa kuwapunja wateja wao.

 

Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano kutoka (WMA), Irene John alisema kuwa
wakala wa vipimo hawajalala katika siku za sikukuu, wataendelea kufanya ziara za kustukiza kwenye sehemu mbalimbali za biashara ikiwemo kwenye mabucha,
sokoni na Vituo vya mafuta ili kuleta usawa kati ya Muuzaji na Mteja kupata stahiki zao kulingana na thamani ya pesa inayolipwa.

 

“Katika Maadhimisho haya ya Miaka 58 Uhuru Tanganyika hatujalala tumefanya
zoezi la ukaguzi wa kustukiza kwenye mabucha hapa Mwenge Jijini Dar es Salaam na zoezi hili linafanyioka nchi nzima, na lengo kuu ni kulinda stahiki za wateja na wauzaji ili kila mtu akitoa pesa ya lita moja apate lita moja, akitoa pesa ya kilo moja vilevile apate kilo moja”, Irene John Meneja Mwasiliano (WMA).