Home Makala SAUTI YA MWALIMU NYERERE NA MIAKA 58 YA UHURU WA TANGANYIKA

SAUTI YA MWALIMU NYERERE NA MIAKA 58 YA UHURU WA TANGANYIKA

0

**************************

Na Judith Mhina-Maelezo

Historia imeandikwa na itaendelea kuandikwa, kwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais wa kwanza
wa Jamhuri ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sauti yake itaendelea kuwa muongozo na
kielelezo cha kuwafunza Watanzania ili kuwa na Umoja na Utaifa alioujenga.
Hakika imetimia miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika ambapo Baba wa Taifa umeweka misingi
imara ya Utaifa na Umoja ambao dunia inashangaa uliwezaje, umefanyaje, kuunganisha
makabila zaidi ya 120 yaliyopo mashariki, magharibi, kusini, kati na kaskazini mwa Tanzania
na kuwafanya kuwa wamoja na kuwashangaa wale wote wanaoshabikia ukabila.
Mwalimu Nyerere kauli yako ya msingi kuhusu Afrika nanukuu “Uhuru wa Tanganyika na
baadaye Tanzania hautakuwa na maana kama nchi nyingine za Afrika hazitakuwa huru ”

 

Kila uchweo maandiko yako, sauti yako inasikika katika pande zote za Tanzania kuanzia kwenye magazeti, redio, televisheni, nyimbo, ngonjera, mashairi na ngoma za asili. Hii ikiwa ni pamoja na nyimbo za muziki wa dansi, muziki wa kizazi kipya, kwaya, michezo ya watoto halaiki na hafla mbali mbali za kitaifa na mataifa na vinywa vya watanzania kwa ujumla.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere misingi yako uliyoiweka inasikika katika sauti yako ambayo bado inatoa ulinzi na usalama duniani. Kutoka Lebanon, ambapo Jeshi la Wananchi wa Tanzania-JWTZ linalinda amani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa ni sehemu ya juhudi na matunda yako Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika-SADC pia, dhamira yako ya kuleta Uhuru na Umoja barani Afrika.

 

Sauti yako inasikika katika hotuba zako maarufu ulizowahi kuongeza na kusema kwa hisia kali yenye unyenyekevu na upendo kwa Watanzania. Sauti yako inaelimisha, inahamasisha, inatupa taarifa, kutuonya, kutuasa na kutupongeza kwa mambo mbalimbali yaliyotokea katika Jamii yetu, nje ya nchi na kwa watu mashuhuri hapa Tanzania na duniani kwa ujumla.

 

Mwalimu usiku wa kuamkia tarehe 09 Desemba mwaka 1961 ni siku ya kukumbukwa na Watanzania wote kwa kuwa wahenga walisema, ilikuwa kama ndoto ambayo ilitokea kweli.

 

Tanganyika kuwa huru na kujitoa katika makucha ya wakoloni bila kumwaga damu ilikuwa ni kielelezo tosha kama ulivyo toa hotuba yako fupi iliyokuwa na matumaini lukuki kwa Watanganyika ya Uhuru na Umoja.

 

Aidha, hotuba zako za mwanzo kama Waziri Mkuu wa Tanganyika Mwalimu Nyerere ulionekana pale Mnazi Mmoja ukielezea juu ya Katiba tarehe 31 Mei, 1962 na sherehe za ufunguzi wa chemchem ya maji ya mnazi mmoja Dar-es-salaam na tarehe 08 Desemba 1962.

 

Matamko yako ya awali ya “Uhuru na kazi”, “Uhuru na Maendeleo” ni vielelezo tosha kuwa hakuna kubwetekaukiwa huru lazima udhamini uhuru ulionao kwa kufanya kazi na kujiletea maendeleo. Siasa ya ujamaa na kujitegemea ulisisitiza usiwe kupe jitegemee na kuongeza hakuna mjomba wa kuijenga nchi yetu ila watanzania wenyewe.

 

Nimekariri na kutafakari baadhi ya hotuba zako kama zile za kisiasa na historia za kuapishwa kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo tukio la kuchanganya udongo wa Bara na Visiwani lilifanyika tarehe 01 Oktoba 1965 pale Zanzibar bado sauti yako ilitamka maneno haya;

 

“Kazi ya nchi na watu wa Tanzania ni kuwaunganisha waafrika kuleta uhuru na umoja kwa waafrika wenzao” huu ni msingi uliousimamia mpaka kuhakikisha Afrika yote inakuwa huru.

 

Hiki kilikuwa kishindo na mashangao mpaka leo dunia imeshindwa kufahamu kwa vipi umeweza kuunganisha Tanganyika na Zanzibar, hotuba ya kwanza ya mkutano wa hadhara aliofanya pale Zanzibar tarehe 20 Desemba 1964.

 

Uliwaeleza Watanzania kibaga ubaga kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar sio wa kwako na Shekhe Abeid Amani Karume bali ni wa Watanzania kwa kuwa asilia sisi tu wamoja.

 

Mwalimu Nyerere mnamo tarehe 1 April 1965 akafungua mkutano wa pili tangu Tanzania iwe Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ulijikita zaidi katika kuzungumzia rushwa makazini. Uligundua mapema kuwa ukifanya mzaha na rushwa nchi haitasonga mbele. Hili watanzania wamelidhibitisha na sasa wanapambana nalo kwa kila hali.

 

Sauti yako Mwalimu imesikika pale Zanzibar, katika sherehe za miaka 10 ya Azimio la Arusha na miaka 20 ya Afro Shiraz Party-ASP na wakati wa kuzaliwa kwa chama kipya yaani Chama cha Mapinduzi – CCM huko Zanzibar tarehe 05 Februari 1977. Nakumbuka hotuba yako uliyohutubia viongozi wa chama na serikali wakiwemo wazee wa Mkoa wa Dar-es-salaam
pale Diamond Jubilee tarehe 09 Desemba 1978.

 

Sauti yako Mwalimu inabakia kuwa gumzo na kuendelea kusikika kama katika hotuba yako uliyoitoa kwa wazee wa chama chako cha Tanganyika African National Union –TANU na wazee wa na Mzizima Jijini Dar-es-salaam. Mwalimu ukatoa maelezo zaidi na ufafanuzi juu ya utaifishaji wa majumba katika mtaa wa Lumumba tarehe 29 Mei 1971.

 

Kama hiyo haitoshi Mwalimu sauti yako bado inasikika katika hotuba uliyoitoa mwaka 1965 tarehe 03 Mei ukifungua semina ya wakuu wa madhehebu ya dini mbalimbali nchini huko Tabora. Ambapo uliwaasa kuwa na umoja upendo na kutobaguana kwa kuona dini hii ni bora kuliko nyingine, Mwalimu ulisisitiza wote tunajenga Tanzania moja inayohitaji maendeleo.

 

Sauti yako bado inapenyeza katika mioyo yetu tunaposikia hotuba uliyoitoa tarehe 05 mwezi wa Februari mwaka 1967, ukiwahutubia wananchi wakati ukitanganza Azimio la Arusha, siasa ya ujamaa na kujitegemea pale Mnazi Mmoja Dar-es-salaam. Pia, ulifanya mkutano wa hadhira ambapo Mwalimu Nyerere alihutubia wananchi wakati wa maadhimisho ya miaka
10 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 26. 04 1974 uliofanyika pale Amani Stadium Zanzibar.

 

Aidha sauti yako inasikika katika tafrija ya wazee wa CCM waliokuita kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, katika ukumbi wa Diamond Jubelee tarehe 08 Mei 1977. Hakika ulistahili pongezi kwa kuwa kazi uliyoifanya inaonekana hadi sasa.

 

Maandamano ya wanajeshi ya kuunga mkono Azimio la Arusha, siasa ya ujamaa na kujitegemea Jijini Dar-es-salaam tarehe 06 Februari 1967 yalidhihirishia dunia kuwa uko katika maamuzi sahihi. Kama hiyo haitoshi imedhihirika pale misingi ya Azimio la Arusha ilipoachwa taifa likaenda mrama.

 

Sauti yako Mwalimu bado inasikika ulipowahutubia Watanzania siku ya mashujaa tarehe 01 Septemba 1979 mara baada ya kumalizika kwa vita vya Tanzania na Uganda na kuipongeza JWTZ kwa ushindi walioupata na kuhakikisha Uganda inajitawala katika misingi ya usawa na kudhamini utu wa mtu pale uwanja wa Taifa.

 

Pamoja na mambo ya siasa Mwalimu umesikika katika masuala muhimu ya Taifa na Kimataifa Mwalimu ulifungua washa ya misitu pale Mwadui Shinyanga akiwa mstari wa mbele kulinda rasilimali za misitu tulizonazo katika hotuba yako uliyoitoa tarehe 14 Septemba 1984.

 

Hayo ya Kimataifa tena sio yakusema umefanya mengi mno kuanzia nchi zisizofungamana na upande wowote, Afrika, Asia, Amerika, Bara Hindi, nchi za Scandinavia, Amerika ya Kusini na Mashariki ya mbali.

 

Mwalimu sauti yako inasikika kimataifa pale alipohutubia mkutano wa sita wa nchi zisizofungamana na upande wowote nchini Cuba katika Jiji la Havana, tarehe 05 Septemba 1979 iliyohusu masuala ya ulinzi na usalama wa Taifa huru.

 

Suala la Ukombozi Kusini mwa Afrika na duniani kwa ujumla hilo kwako lilikuwa ni suala linalopewa kipaumbele Mwalimu ulihutubia wakati uhuru wa Msumbiji tarehe 25 Juni 1975 katika jiji la Maputo. Pia ulikabidhiwa majengo ya chama cha ukombozi cha Msumbiji – FLERIMO kwa serikali ya Tanzania tarehe 05 Julai 1976 na kutamka yatakuwa shule, kwa kuwa elimu ni kipaumbele kwa taifa lolote ili kuleta maendeleo ya watoto wa sasa na kizazi
kijacho.

 

Ziara Mwalimu Nyerere nchini Uingereza 1975 alihutubia mbele ya Malkia Elizabeth wa 11 ambapo, ililenga kuongelea suala la uhuru wa Zimbabwe na suala la ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini na utawala wa walio wengi weusi.

 

Hivyo jinsi gani Uingereza itasaidia kuharakisha uhuru wa Zimbabwe na mlowezi kaburu wa Afrika ya Kusini kuachia madaraka kwa weusi walio wengi.

 

Kutokana na masilahi waliyokuwa nayo wazungu katika nchi hizo mbili Waandishi wa Habari walikulenga mara kwa mara kwa ajili ya mahojiano, lakini moja ya mahojiano hayo ni kuhusu Uhuru wa Zimbabwe na Afrika ya Kusini mwaka 1976 tarehe 23 Septemba. Mwandishi alitaka kujua mazungumzo yako Mwalimu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Amerika Henry Kissinger.

 

Mwalimu ulisema “Lazima wavamizi watambue na wakubali utawala wa weusi waliowengi lengo sio kuwapa silaha wapigania uhuru bali tunaamini majadiliano na maridhiano lakini ikishindikana tutatumia umoja wetu kuwaambia waondoke Zimbabwe”.

 

Ulifanya hivyo kwa Msumbiji, Angola, Namibia ukawapa sehemu ya ardhi ya Tanganyika waweze kujijenga na kupigania uhuru wao, hii ypte inaonyesha ni jinsi gani ulidhamini uhuru wa mtu uhuru wa taifa lolote duniani . Hakika tunaona fahari tunapoadhimisha miaka 58 ya uhuru na kurejea jina lako kama mwamba ambao utasimama milele.

 

Sauti yako Mwalimu inasikika katika nyanja mbalimbali maana hakubaki nyuma katika kuwatia moyo wanawake katika kugombania haki zao pia, ulitoa hotuba wakati ukifungua mkutano wa wanawake wa Afrika wa (African women Conference) Jijini Dar-es-salaam tarehe 02 Agosti 1962, uliofanyika katika ukumbi wa Jiji Dar-es-salaam –City hall.

 

Mwalimu nani asiyejua kuwa wewe ni mcha mungu lakini ulisema waziwazi katika hotuba yako pale Zanzibar kuwa Tanzania haina dini, ila watu wake wana dini. Hivyo, ulipata fursa ya kuhutubia kilele cha ufunguzi wa kanisa Butiama Musoma 07 Novemba 1963. Ahutubia, akifungua share government state factors Mkoa wa Mwanza 08 Januari 1967.

 

Tanzania ya viwanda ilianza kitambo sana Mwalimu ulihamasisha viwanda, ambapo uliacha viwanda 414 vya serikali lakini hukuacha kuhamasisha sekta binafsi kujenga viwanda.

 

Mwalimu sauti yako inasikika katika hotuba yako uliyoitoa tarehe 21 Agosti 1965 ulipoweka jiwe la msingi la kiwanda cha viberiti kilichopo eneo la Karanga – mjini Moshi.

 

Mwaka 1986 Mwalimu ulingatuka katika madaraka ya urais na uliendelea na kufanya safari mbalimbali mikoani kama kutembelea viongozi wa Chama na Serikali Mkoa wa Kagera na kuhutubia katika viwanja vya shule ya msingi lubuli Bukoba Mjini 10 Septemba 1986.

 

Azungumza na kujibu maswali ya wanachama wa CCM Tawi la Damwa tarafa Bunyezi Karagwe Kagera.

 

Hakika hotuba yao maarufu ambayo Watanzania wengi wanaijua ni ile uliyoitoa Mkoa wa Tabora wakati wa sherehe za Mei Mosi mwaka 1981, ya hadithi ya Mwanamwali aliyekuwa mlimani. Ambayo ina funzo kubwa kwa viongozi wetu wanapodhamiria kutenda lililo jema kwa nchi wasigeuke nyuma watakuwa jiwe na kusaliti watanzania, kwa sasa jemedari tunae hatuna shaka Dkt John Pombe Magufuli.

 

Mwalimu ulitilia manani suala la sayansi na tekinolojia kwa kuwa ulijua hakika dunia ya leo inakoelekea bila hivyo Tanzania itabaki nyuma. Ulifanya mkutano huo katika ukumbi wa kerimjee Dar-es-salaam tarehe 18 Oktoba 1989 na kuelezea umuhimu wa sayansi na tekinolojia ili tusiachwe nyuma.

 

Kwako Mwalimu hakuna jambo dogo wala kubwa yanapokuja masilahi ya Watanzania Mwalimu ulihutubia Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara tarehe 10 April 1999, upandaji miti kitaifa. Mwana mazingira namba moja ulieweka msitu mzuri pale Butiama na ni kati ya marais waliofanikiwa kutenga maeneo mengi hapa Tanzania ya kuhifadhi mapori yetu yawe ya akiba au ya wanayama pori.

 

Aidha ulikaribishwa katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama Mei Mosi (01 Mei 1995) Mkoani Mbeya mwaka 1995 na kupata fursa ya kuongeza na hadhara iliyokuwepo na Watanzania kwa ujumla. Hotuba hii imeweka misingi imara sana kwa Watanzania na funzo ambalo halitasahaulika katika historia ya nchi kuhusu suala zima la ubinafsishaji.

 

Pia, ulipata nafasi ya kuongeza na waandishi wa habari mwaka 1995 nyumbani kwako Msasani Jijini Dar-es-salaam. Hotuba ile yenye utajiri mkubwa wa kutuasa kwa kutuonyesha miiko na misingi ya uongozi, pia kiongozi tumtakaye Tanzania awe na vigezo gani.

 

Kama hiyo haitoshi hotuba yako maarufu sana kwa Watanzania ile ya Kilimanjaro Hoteli ulipoongea na waandishi wa habari, tarehe 18 April 1995 kubwa likiwa la kutuhatarisha na kutuasa juu ya nyufa zilizojitokeza za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Umoja umoja Mwalimu umetuasa kwa sasa muungano wetu ni imara zaidi.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika shamra shamra za miaka 58 ya Uhuru ameweza kuweka jiwe la msingi la daraja la kihistoria litakalounganisha Mkoa wa Geita na Mwanza. Daraja kubwa Afrika Mashariki na Kati hiki ni kielelezo muhimu kwa watanzania kwa aliyoyakusudia Baba wa Taifa yanafanyika Uhuru na Maendeleo .

 

 

Yapo mengi ya kujivunia tunapoadhimisha miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika maendeleo makubwa yanaonekana na vita aliyoipigania kwa hali na mali Baba wa Taifa inaonekana . Dhidi ya maadui watatu Ujinga , Umasikini na Maradhi.
Miaka 58 ya Uhuru Tanzania sio nchi masikini tena ni nchi Tajiri ina kila kitu kinachostahili kuleta maendeleo, tuna rasilimali watu iliyojizatiti na imeelimika ipasavyo kuleta maendeleo. Mungu Ibariki Tanzania UHURU NA KAZI, UHURU NA MAENDELEO. PUMZIKA KWA AMANI MWALIMU.