Home Mchanganyiko Chuo cha uhasibu Arusha chazindua kituo cha kukuza mawazo ya biashara.

Chuo cha uhasibu Arusha chazindua kituo cha kukuza mawazo ya biashara.

0

*******************************

Happy Lazaro,Arusha.

Arusha.Chuo Cha uhasibu Arusha  kimezindua kituo cha kukuza mawazo ya biashara kwa wanachuo ili kuwawesha kuweza kujiajiri na hata kukopesheka katika mabenki mbalimbali.

Aidha kituo hicho pia  kinalenga kuwaunganisha wanachuo hao na taasisi mbalimbali za kifedha ili waweze kukopesheka kwa urahisi  kupitia mawazo yao ya biashara .
Akizungumza Jana wakati wa uzinduzi wa  kituo hicho ,Mkuu wa chuo hicho ,Profesa Eliamani Sedoyeka amesema kuwa,kituo hicho kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuwajengea Vijana hao uwezo wa kujiamini katika kutekeleza azma ya uchumi  wa viwanda .
Profesa amesema kuwa,wamefikia hatua ya kuanzisha kituo hicho kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa kwa Vijana ya kushindwa kuandaa mawazo ya biashara yatakayowawezesha kujiajiri na hata kuweza kukopesheka kwenye Taasisi hizo.
“tumeamua kuzindua kituo hiki ambacho kitaleta manufaa makubwa sana kwa wanachuo wetu kwani wengi wao hawana uelewa namna ya kuandaa mawazo ya biashara na kwa kuanzia tuna wanachuo 15 tayari ambao wameshaanza mchakato huo huku tukitarajia kupokea wanachuo 40 .”amesema Profesa Sedoyeka.
Aidha amewataka Vijana kuchangamkia fursa hiyo kwani kupitia kituo hicho wataweza kuwa na biashara kubwa na wataweza kujiajiri wao na kutoa ajira kwa vijana wengine ,na hivyo ndoto zao kuweza kutimia .
Naye Mkuu wa mkoa wa Arusha ,Mrisho Gambo amesema kuwa ,kitendo kilichofanywa na chuo hicho ni mfano wa kuigwa kwani kina manufaa makubwa Sana kwa wanachuo kuweza kuondoka na mawazo ya biashara yaliyoandaliwa kitaalamu zaidi.
Gambo amesema kuwa, changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwakabili Vijana wengi ni ukosefu wa mitaji ili waweze kujiajiri ila kupitia kituo hicho Vijana wataweza kuunganishwa na taasisi za kifedha moja kwa moja na kuweza  kukopesheka.
Aidha amewataka wanachuo kuchangamkia fursa hiyo ya kipekee huku akivitaka vyuo vingine kuiga mfano Kama huo ili kuwasaidia wanavyuo wao.
Mmoja wa wanachuo,Bahati Lucas amepongeza hatua hiyo kwani itawasaidia sana kuondoka na mawazo ya biashara moja kwa moja chuoni hapo na kwenda kuyafanyia kazi na kuondokana na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira iliyopo.