Home Mchanganyiko JAFO AKATAA OMBI LA SH.MILIONI 148 KUKARABATI JENGO LA HOSPITALI YA WILAYA...

JAFO AKATAA OMBI LA SH.MILIONI 148 KUKARABATI JENGO LA HOSPITALI YA WILAYA SHINYANGA

0

Na Mwandishi wetu, SHINYANGA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo amekataa ombi la Sh.Milion 148 kwa ajili ya kukarabati jengo la utawala la hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga lililojengwa miaka michache iliyopita.

Akiwa katika ziara wilayani humo ya kukagua ujenzi wa majengo mapya ya hospitali hiyo, Waziri Jafo amesema hakubaliana na ombi hilo huku akisema ni bora kujenga jengo jipya kuliko kutumia kiasi hicho kwa ajili ya kukarabati jengo moja.

“Gharama hizi ni sawa na kujenga upya jengo kuliko kutumia fedha hizo kukarabati jengo moja tena likihusisha kubadilisha paa na kurejesha rangi za kuta pekee,”amesema

Hata hivyo,  Jafo amembana mtaalam wa halmashauri hiyo ampe mchanganuo wa gharama hizo lakini mtaalam huyo alishindwa kueleza wamepataje gharama hiyo ya ukarabati.

Kadhalika,  Jafo alitembelea ujenzi wa majengo mapya  ya hospitali yaliyojengwa baada ya halmashauri ya Wilaya hiyo kupokea Sh.Bilion 1.5 ambapo aliwapongeza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack na Mkuu wa Wilaya hiyo Yasinta Mboneko kwa kusimamia vyema fedha hizo na kufanikisha ujenzi wa majengo manane Mazuri ya Kisasa.

 Aidha, Jafo amewaambia wananchi waliokuwa kwenye eneo hilo kuwa  kazi nzuri iliyofanywa na Mbunge wa Jimbo hilo la Solwa,  Ahmed na  Mbunge wa Viti Maalum Azzah Hilal imewezesha kupatikana kwa fedha za hospitali hiyo pamoja na vituo kadhaa vya Afya katika halmashauri hiyo ya Shinyanga.