Home Mchanganyiko MAAFISA HABARI WAPONGEZWA KWA KUISEMEA VIZURI SERIKALI

MAAFISA HABARI WAPONGEZWA KWA KUISEMEA VIZURI SERIKALI

0

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi  akitoa maelekezo kwa uongozi wa Chama cha Maafisa Habari Tanzania (TAGCO) wa kuendeleza mpango wa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa maafisa habari wa serikalini leo alipokuwa akifunga mafunzo ya maafisa hao yaliyokuwa yakifanyika jijini Dodoma kwa siku tano.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi akimkabidhi cheti  Afisa Habari kutoka Ofisi ya Rais Utumishi Menejimenti na Utawala Bora Bibi.Happy Shayo katika sherehe ya kufunga Mafunzo ya Maafisa Habari Serikalini leo yaliyokuwa yakifanyika Jijini Dodoma kwa siku tano ambayo yaliandaliwa na uongozi wa chama cha maafisa habari Tanzania (TAGCO).

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi (aliyeketi watatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa Habari kutoka Ofisi za Mikoa na Serikali za Mitaa baada ya kufunga mafunzo ya Maafisa Habari Serikalini yaliyokuwa yakifanyika Jijini Dodoma kwa siku tano,wa kwanza kulia ni Katibu wa Chama cha Maafisa Habari Serikalini Tanzania (TAGCO).

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi akionyesha Jarida la Nchi Yetu linaloandaliwa na Idara ya Habari MAELEZO, lililo sheheni taarifa mbalimbali za utekelezaji wa serikali ya awamu ya tano kwa miaka minne maara baada ya kukabidhiwa jarida hilo katika sherehe za kufunga mafunzo ya Maafisa Habari Serikalini yaliyokuwa yakifanyika Jijini Dodoma kwa siku tano.

………………

Na Shamimu Nyaki – WHUSM,Dodoma

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo  Dkt.Ally Possi amewapongeza Maafisa Habari,Uhusiano na Mawasiliano Serikalini kwa kutangaza vizuri shuguli za Serikali ikiwemo miradi inayotekeleza ambayo itawaletea wananchi maendeleo.

Dkt.Possi ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya kimkakati ya Uandishi wa Habari za Serikali ya awamu ya pili kwa  Maafisa Habari,Uhusiano na Mawasiliano Serikalini ambapo amewataka kutumia elimu waliyopata kuendelea kuhabarisha umma kwa weledi na kwa usahihi habari zinazohusu Serikali.

“Maafisa Habari mnafanya vizuri katika kutangaza shughuli za Serikali kwa wananchi,naomba muendelee kufanya hivyo kwa kuwa kada yenu ni muhimu katika kufikisha ujumbe wa Serikali kwa wanachi na mtumie kalamu zenu vizuri ili kulinda na kudumisha amani ya nchi yetu”alisema Dkt. Possi.

Aidha Dkt.Possi amewataka waandaaji wa mafunzo hayo kuendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na kutumia mifumo tofauti ya ndani na  nje ya nchi pamoja na kufanya tathmini ili kuona mabadiliko yaliyopatikana kutokana na mafunzo hayo.

Hata hivyo Dkt. Possi aliwashauri Maafisa Habari wote wa Serikali kujiunga na Chama cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) ili kurahisisha mawasiliano miongoni mwao pamoja na kushirikiana katika kazi wanazofanya  ikiwemo kubadilishana uzoefu na kusaidiana kijamii na kitaaluma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi  Idara ya Habari –MAELEZO Bw.Rodney Thadeusi amesema kuwa jukumu la maafisa habari wa Serikali ni kutoa taarifa sahihi na  kwa wakati zinazohuzu Serikali kwa wananchi kutumia njia zote za mawasilano .

“Maafisa habari kazi yetu kubwa ni kuisemea Serikali tusiposema sisi wengine watasema na wengine wanaweza kusema ambayo sio sahihi na wakati mwingine kukosoa hata yale mazuri ambayo Serikali inatekeleza kwa wananchi wake hivyo tuendelee kutumia taaluma yetu kuitangaza vizuri  Serikali”alisema Bw.Rodney.

Naye  Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bibi.Sara Msika amesema lengo la  mafunzo hayo ni kuendelea kuboresha taaluma ya maafisa hao katika kipindi hiki ambacho dunia imekuwa na mabadiliko makubwa katika kada hii ya uandishi wa habari .

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo  Afisa Habari kutoka TBC Bibi.Catherine Nyoni ameshukuru waandaaji wa mafunzo hayo kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa Maafisa Habari Serikalini ambayo yamesaidia  kuboresha taaluma yao pamoja na kubadilishana uzoefu.

Mafunzo hayo ya siku tano yalioandaliwa na Idara ya Habari –MAELEZO pamoja na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) yamekuwa na mada mbalimbali ikwemo namna ya kutumia mitandao ya kijamii kuhabarisha umma pamoja na uandishi mzuri wa habari za Serikali.