Home Mchanganyiko WATAALAM WAJADILI MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KUTOA HUDUMA ZA AFYA

WATAALAM WAJADILI MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KUTOA HUDUMA ZA AFYA

0

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Ellen Mkondya akizungumza katika mkutano wa tatu wa kisayansi kuhusu matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma za afya nchini.  Mkutano huu umewashirikisha wataalam kutoka hospitali mbalimbali nchini pamoja taasisi nyingine.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia mkutano huu leo.

Mkuu wa Idara ya Tehama Muhimbili, Bw. Patrick Muro akitoa mada kwenye mkutano kuhusu matumizi ya teknonolojia katika kutoa huduma za afya. Wengine ni watoa mada wakiwa kwenye mkutano.

Washiriki wakisikiliza watoa mada kuhusu matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma za afya nchini.

…………………

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanya kongamano la tatu la kisayansi kujadili matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma bora za afya katika zama za maendeleo ya kidijitali. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Hedwiga Swai amesema Muhimbili imefanya uwekezaji mkubwa kwenye mifumo ya TEHAMA na imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Serikali katika matumizi ya teknolojia.  

“Kongamano hili litahusisha washiriki kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila pamoja na washiriki kutoka nje ya Dar es Salaam ambapo watatoa uzoefu wao na kujadili jinsi ya  kutumia teknolojia ya kidijitali katika nyanja mbalimbali za afya na kuona wapi tumefanikiwa na maeneo yapi tunahitaji kufanya vizuri zaidi,” amesema Dkt. Swai.

Dkt. Swai amesema kongamano hili litatoa fursa kwa washiriki kupata elimu ya teknolojia mbalimbali zilizopo ambazo zinaweza kutumika katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma za afya.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri MNH, Dkt. Ellen Mkondya amesema Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ndio hospitali kubwa nchini inapaswa kujizatiti kwenye eneo la teknolojia katika utoaji wa huduma za afya ili kusaidia hospitali za rufaa za kanda kujifunza kutoka muhimbili.

“Teknolojia na uvumbuzi vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku, hivyo ni lazima tutumie fursa hiyo kuhakikisha kuwa maendeleo haya ya kidijitali yanasaidia utoaji wa huduma za afya kama tiba mtandao, utunzaji wa kumbukumbu za wagonjwa  pamoja na kuzuia magonjwa,”amesema Dkt. Mkondya

Kongamano hilo lilitanguliwa na na mafunzo kwenye maeneo mbalimballi ikiwamo jinsi ya kufanya utafiti,  namna ya kuandika miradi ya maendeleo na namna ya kutumia TEHAMA katika kufanya utafiti.

Katika kongamano hilo mada mbalimbali zinatarajiwa kuwasilishwa ikiwemo utunzaji wa kumbukumbu za wagonjwa kieletroniki, sheria na kanuni zinazosimamia tiba mtandao, uzoefu na changamoto za tiba mtandao, saikolojia ya mitandao ya kijamii na mchango wa mitandao ya kijamii katika sekta ya afya.