Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akikagua bonde la Ntambuko lililopo kijiji cha Kinyeto wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Singida.
Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akizungumza na wakulima (hawapo pichani) wanaotekeleza kilimo cha umwagiliaji kwenye bonde la Kinyeto Ntambuko Singida vijijini.
Muonekano wa bwawa la Msange lililopo Singida vijijini. Uwepo wa bwawa hilo umeshindwa kuonyesha tija kwa wakulima kutokana na kukosa fedha ya kukamilisha mradi huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida vijijini, Elia Digha (kushoto) akimuonesha Naibu Waziri mradi wa skimu ya umwagiliaji unaotekelezwa kwa tija kubwa ya wakulima wa kata ya Msange mkoani Singida.
Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akikagua shamba la vitunguu vinavyolimwa kupitia teknolojia ya umwagiliaji kwa njia ya matone katika Kijiji cha Msange mkoani Singida.
Mkurugenzi wa kiwanda cha kukamua alizeti cha Simai, Juma Mene (kulia) akizungumza na Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Mtinko Singida DC.
Na Dotto Mwaibale, Singida
NAIBU Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba (MB), amesema kuna haja sasa ya kufungamanisha ‘Elimu Yetu na Kilimo Chetu’ kwa maana ya kuboresha mitaala iliyopo kwenye vyuo vya kilimo, ili kuanza kumwezesha mwanafunzi anapohitimu badala ya kwenda mtaani kusubiri kuajiriwa apelekwe kwanza kwenye elimu ya vitendo walau kwa mwaka mmoja ili kupata uzoefu.
Akizungumza mbele ya Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Singida DC, muda mfupi kabla ya kuanza ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya Kilimo Mazao, kilimo cha umwagiliaji na mfumo wa masoko wa mazao ya wakulima kupitia ushirika, mkoani hapa jana, Mgumba alisema wahitimu wengi wanatoka zaidi na nadharia kuliko vitendo.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ina jumla ya vyuo 14 nchi nzima ambavyo vinafundisha na kuzalisha Maafisa Ugani na wataalamu wengine wa kilimo, lakini pia kuna Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), na vingine nje ya Wizara kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatoa Wahandisi wa Kilimo cha Umwagiliaji.
“Ukitazama wanafunzi walio wengi wanaotoka kwenye vyuo hivyo unakuta wapo vizuri sana kwenye nadharia, mfano kuna mwanafunzi anamaliza hata mkahawa wenyewe haujui, akipata kazi huyuhuyu unamwambia akasimamie kahawa…anafika kule anakuta mkulima anaijua kahawa kuliko mtaalamu,” alisema Mgumba
Alisema ni wakati mwafaka wa kuboresha elimu kwenye mitaala ya kilimo ili kumpa mhitimu uzoefu wa kutosha wa nadharia na vitendo ili kuongeza tija zaidi kwa mkulima lakini pia yeye mwenyewe kujiweka mahiri kama mtaalamu kwa mazao husika.
Naibu Waziri alitoa mfano wa wahitimu wa fani ya udaktari ambao baada ya kumaliza miaka 5 hulazimika kwenda ‘internship’ mwaka mzima na kusisitiza kuwa ifike mahali na hao wa sekta ya kilimo wafanye internship ili kujijenga vizuri kivitendo kabla ya kuajiriwa kama afisa ugani na mtaalamu.
“Walio wengi elimu wanayopewa ni ya kilimo cha jumla. Sasa kama atakwenda kukaa kwenye pamba au korosho na kadhalika kwa mwaka mzima atayajua hayo mazao ipasavyo na mwisho tutakuwa na wataalamu mahiri, na hawa tukija kuwaajiri naamini tutakidhi mahitaji,” alisema Mgumba
Aidha, kupitia ziara hiyo akizungumzia hali halisi ya uzalishaji wa zao la alizeti nchini, alisema bado kuna upungufu kama taifa wa mafuta ya kula kiasi cha kupelekea kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuagiza mafuta hayo toka nje, jambo ambalo anaamini kama tutaongeza tija ya uzalishaji kwenye kilimo cha alizeti basi pengo hilo linaweza kuzibwa.
“Ukizungumza alizeti nchi hii basi ni lazima utaje mkoa wa Singida. Sasa kwanini hatujitoshelezi?….tuna viwanda vingi vya kuchakata mafuta ya alizeti vyenye mahitaji zaidi ya tani milioni 2, na mahitaji ya nchi ili tujitosheleze kwa mafuta tunahitaji mbegu zaidi ya tani milioni moja na nusu,” alisema Mgumba
Hata hivyo Mgumba alisema ili kuwasaidia wakulima kutatua changamoto mbalimbali kwenye kilimo chao ni lazima tuendeleze programu ya SDP1 ambayo inalenga kuwa na vituo vya rasilimali kilimo kila kata.
Mgumba alisema lengo la uanzishwaji wa vituo vya rasilimali kilimo ambavyo ni mpango endelevu bado haujafa, ni kutoa teknolojia na elimu stahiki kwa vitendo kwenye kata, sambamba na kutoa taarifa sahihi kwa wakulima ikiwemo hali ya hewa na tahadhari nyinginezo kutokana na ekolojia ya maeneo husika.
Awali, Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida DC Wilson Shimo, alimweleza Naibu Waziri kuwa pamoja na mambo mengine, suala la uchache wa watumishi wa idara ya ugani, ambapo waliopo ni 17 tu ambao wanashindwa kuwafikia wakulima wote wa vijiji 84 na kata 21 kwa wakati ni tatizo katika ustawi kwenye kilimo.
Aidha, kukosekana kwa zana bora kumepelekea wakulima walio wengi kuendelea kutumia jembe la mkono, na skimu za umwagiliaji kuwa na gharama kubwa kiuenedeshaji kutokana na matumizi ya mafuta ya Dizeli.
Aidha, katika ziara hiyo, Mgumba akiongozana na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Singida alipata fursa ya kutembelea na kujionea hali halisi ya kilimo na uzalishaji kwenye vijiji na Kata mbalimbali ndani ya mkoa wa Singida, ikiwemo viwanda vikubwa na vya kati vya kukamua mafuta ya alizeti.
Maeneo mengine aliyotembelea ni bonde la kilimo la Ntambuko, skimu ya umwagiliaji ya Kata ya Msange, na baadaye alikutana na kufanya mkutano na wakulima wa pamba kupitia AMCOS ya Ughandi.