Home Mchanganyiko Isiwe Sababu ya TBL, yawafikia wakazi wa Kisarawe

Isiwe Sababu ya TBL, yawafikia wakazi wa Kisarawe

0

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe,JokateMwegelo akiongea katika maadhimisho hayo

Wanafunzi kutoka shule mbalimbali hawakubaki nyuma katika maadhimisho hayo

Wanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia katika picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya ya Kisarawe ,Jokate Mwegelo.

*******************************************

Kampuni ya TBL ,imeshiriki kutoa msaada wa kufanikisha kongamano la ukatili wa kijinsia na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, lililofanyika katika wilaya ya Kisarawe,  na kujumuisha wanafunzi kutoka shule mbalimbali za sekondari na washiriki kutoka makundi mbalimbali ya jamii.

 

Kongamano liliandaliwa na Ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto Polisi Wilaya Kisarawe, pamoja na mtandao wa Polisi wanawake TPF NET, ambapo mgeni rasmi katika kongamano hilo alikua ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo.

 

Mwegelo, aliwaasa wanafunzi kuacha  kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi  na kuwasisitiza wajikite zaidi katika masomo ili kuleta mustakabali mzuri wa maisha yao na taifa kwa ujumla.

 

Vilevile alizungumzia  changamoto za Dawati la Jinsia na watoto Polisi Wilaya Kisarawe ambazo ni kutokuwepo kwa Ofisi za Dawati la Jinsia, uhaba wa vitendea kazi pia umuhimu wa kuwa na  kuwepo kituo kimoja kwa ajili ya kushughulikia kesi za ubakaji na kuwaomba wadau kushirikiana kwa pamoja kuzifanyia kazi kwa ajili ya kuliwezesha Jeshi la Polisi kutoa huduma bora kwa wananchi.

 

Akiongea kuhusu ushiriki na kuunga mkono kongamano hilo, Meneja Mawasiliano wa TBL, Abigail Mutaboyerwa, alisema TBL itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Alisema mwaka jana TBL ilitumia maadhimisho haya kwa kuendesha kampeni yake inayolenga kuleta mabadiliko kwenye jamii  iitwayo “#IsiweSababu” (#NoExcuse), kuelimisha jamii kuhusu unywaji wa kiustaarabu na kutokutumia pombe kama sababu ya unanyanyasaji wa kijinsia.

 Mwaka huu TBL, itatumia njia mbalimbali kutoa elimu ya uelewa kwa jamii ikiwemo kuendesha semina kwa wafanyakazi wake na jamii katika maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha Dawati. Vile vile wafanyakazi wa kampuni ya TBL wataungana na Polisi pamoja na wadau mbalimbali kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia. 

Aliongeza kusema kuwa kampeni hii ya #IsiweSababu itaendelea kutoa elimu mbalimbali ikiwemo kuhimiza jamii kuchukua hatua na kuvunja ukimya na pale pombe kutumiwa kama sababu moja wapo za vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na sababu zingine zinazotumika kulaumu vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake, vitendo vya ukatili dhidi ya wanaume pamoja na watoto hasa watoto wa kike.

 TBL, inaamini kuwa ukatili wa kijinsia unaweza kutokomezwa nchini endapo jamii nzima itashirikiana na kuahidi kuchukua hatua kukemea vitendo hivyo kwa kushirikiana na serikali ili kuhakikisha vyombo vya maamuzi vinalivalia njuga suala hili na inaahidi kuendelea kuunga mkono maadhimisho haya