***************************************
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia Kaimu Katibu Mkuu, Neema Msitha, limesema kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la uandaaji za Marathoni pamoja na mbio nyingine za barabarani nchini, ambapo Mbio hizo zimekuwa na mchango mkubwa sana katika kuendeleza mchezo wa riadha pamoja na kukuza uchumi nchini.
Hata hivyo pamoja na mchango mkubwa; kumekuwa na changamoto nyingi za uendeshaji wa mbio hizo zikiwemo baadhi ya waandaji kuandaa mbio bila kusajiliwa, kukosa ulinzi barabarani (traffic control), kukosekana kwa huduma za afya (ambulances),kukosa huduma ya maji ya kunywa katika vituo vya kukimbilia pamoja na baadhi ya wandaaji kushindwa kulipa zawadi kwa washindi, kukosa wataalam/wasimamizi wenye weledi, jambo ambalo linapelekea kuwepo kwa udanganyifu, Changamoto ambazo zimepelekea mgogoro mkubwa baina ya wandaaji, washiriki wa mbio hizo (wakimbiaji) pamoja na wadau wengine wa mchezo wa riadha.
Kutokana na kuwepo kwa changamoto hizo kuanzia tarehe 1 Januari 2020, vibali vyote vya kuendesha mbio za Marathoni na mbio nyingine za Barabarani ngazi ya Taifa, mkoa na wilaya vitatolewa na Baraza la Michezo la Taifa baada ya kupitiwa na Shirikisho la Riadha Tanzania. Vibali hivyo vitatolewa baada ya Baraza kujiridhisha kuwa muandaaji wa mbio hizo amekidhi matakwa ya uendeshaji wa mbio hizo.
Aidha BMT limezielekeza mamlaka za usimamizi wa Michezo ngazi ya Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa hamna mbio yoyote ya barabarani inafanyika bila kibali cha Baraza la Michezo la Taifa.
Kwa mujibu wa Sheria ya BMT waandaji wote wa mbio hizo wanapaswa kulipia asilimia moja (1%) ya tiketi/viingilio vya mbio, kwenda katika mfuko wa maendeleo ya Michezo BMT,Vilevile kuanzia leo tarehe 3 Disemba 2019, Baraza la Michezo la Taifa limeifungia mbio ya “Kigamboni International Marathon” kwa muda wa mwaka mmoja, baada ya kufanyika kwa mbio hiyo tarehe 1 Disemba, 2019, bila kufuata Sheria na kanuni za uendeshaji wa mbio za Marathoni. Mwandaaji wa mbio hizo pia anatakiwa kuhakikisha anakamilisha kulipa zawadi alizotakiwa kutoa katika mbio hizo kabla ya tarehe 12 Disemba, 2019.