Home Mchanganyiko MBUNGE MTATURU ASAIDIA MABATI 50 KKKT MBWANJIKI

MBUNGE MTATURU ASAIDIA MABATI 50 KKKT MBWANJIKI

0

MBUNGE wa Singida Mashariki Mhe Miraji Mtaturu amekabidhi mabati 50 yenye thamani ya shilingi laki 975,000 kwa ajili ya kusaidia kupaua kanisa la KKKT mtaa wa Mbwanjiki kata ya Ikungi.
 
Msaada huo ameukabidhi ikiwa ni utekekezaji wa ahadi yake aliyowahi kuitoa wakati wa harambee iliyofanyika kanisani hapo akiwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi.
 
Akikabidhi msaada huo Mhe Mtaturu amemshukuru Mwinjilisti Meleckzedeki kwa nafasi aliyompa ya kutekeleza ahadi yake katika siku ya ibada.


 
“Niwashukuru viongozi wetu wa dini kwa kuendelea kuiombea amani nchi yetu,niwaahidi kuendelea kushirikiana nanyi katika jimbo letu hili,”alisema Mhe Mtaturu.
 
Amewapongeza viongozi wote wa vijiji na vitongoji waliochaguliwa hivi karibuni na kuahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha na kuwaomba wananchi pia wawape ushirikiano ili kuongeza kasi ya kuleta maendeleo kama ilivyo dhamira ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.


 
“Wananchi msidanganywe na yeyote juu ya mchakato wa uchaguzi kwani ulisimamiwa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi wa nchi yetu,kujitoa kwa chama cha siasa haizuii uchaguzi kuendelea na kama walikuwa na hoja wangepinga mahakamani ili wapate ufafanuzi,”alisema Mtaturu.

Amewaomba viongozi waliochaguliwa na kula kiapo kwenda kufanya kazi kwa uaminifu,uzalendo na weledi mkubwa katika kuwahudumia wananchi bila kuangalia itikadi za vyama,dini au rangi zao.

Akitoa neno la shukrani kutokana na msaada huo Mwinjilisti Meleckzedeki Mundu ameshukuru kwa msaada huo ambao utasaidia kukamilisha kanisa jipya.

“Mhe mbunge tunakushukuru sana kwa msaada huu,tunafurahishwa sana na kujitolea kwako kwa kuwa hii sio mara ya kwanza umekuwa ukisaidia maeneo mengi,kwa kweli tunakuombea sana ili kile ulichopunguza kiongezeke zaidi,tunashukuru msaada huu utakamalisha lengo tulilonalo la kukamilisha kanisa jipya,ubarikiwe sana,”alisema Mwinjilisti huyo.


 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbwanjiki Omari Kulungu amemshukuru mbunge kwa kutimiza ahadi yake kwa kanisa na kuwaomba waumini kuendelea kumpa ushirikiano ili aweze kusaidia katika mambo mengi ya kuleta maendeleo.
 
“Mhe Mbunge huyu sisi tunamuona ni mkombozi wetu kwenye mambo mengi yaliyokwama,niwaombe ndugu zangu tumpe ushirikiano,mimi mwenyekiti wenu ahadi yangu kwenu baada ya kuapishwa nitasimamia ujenzi wa shule ili watoto wetu waweze kusoma hapa hapa Mbwanjiki,”alisema Kulungu.