Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani akizungumza na wakandarasi na wauzaji wa vifaa vya umeme katika kikao cha pamoja leo jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani akisisitiza jambo kwa wakandarasi na wauzaji wa vifaa vya umeme katika kikao cha pamoja leo jijini Dodoma.
Mmoja wa wakandarasi kutoka mkoani Arusha, Michael Njarita akizungumza katika kikao cha wakandarasi na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani leo jijini Dodoma.
Wakandarasi wa umeme vijijini na wauzaji wa vifaa nchini ambao wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Mhe Dk Medard Kalemani leo jijini Dodoma katika kikao cha pamoja.
……………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Nishati, Mhe Medard Kalemani,amesema kuwa hadi kufikia Juni 31 mwaka 2021 kila kijiji nchini kitakuwa kimefikiwa na umeme hivyo amewataka wakandarasi wote waliopewa tenda kuhakikisha wanamaliza ndani ya muda waliopangiwa.
Hayo ameyasema leo jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na wakandarasi wa miradi ya umeme vijijini REA na wauzaji wa vifaa nchini na kuwataka kuzingatia makubaliano waliyoingia na serikali pamoja na kufanya kazi kwa uadilifu.
Pia imewaonya wakandarasi wanaochelewesha miradi kwa visingizio mbalimbali kwa kuwachukulia hatua za kisheria, kimkataba na hatopewa kazi nyingine katika miradi inayofuata.
Dkt.Kalemani amesema kuwa kazi kubwa imefanywa na serikali katika kupeleka umeme vijijini ambapo mpaka sasa tayari vijiji 8115 vina umeme kati ya vijiji 12268.
” Kama wakandarasi wetu mkimaliza kazi kwa wakati kwa kuzingatia mikataba yetu basi kufikia Desemba mwaka huu tutakua tumewasha umeme kwenye vijiji 10446 na kubakia vijiji 1822 Nchi nzima hivyo kufikia Desemba tutakua tumewasha umeme kwa asilimia 80.
Rais wetu ana matarajio makubwa na sisi na ametuamini hivyo hivyo kwa watanzania wana imani kubwa na sisi, niwatake mzingatie mahitaji yetu kama Nchi na hasa tunapoijenga Tanzania ya viwanda mnapaswa kuelewa bila umeme hatuwezi kufanikisha hivyo nendeni mkamalize miradi kwa wakati,” Amesema Dk Kalemani.
Amesema kuna viwanda vitano vya vifaa vinajengwa ambapo serikaki ikijiridisha navyo hadi kufikia Januari itasitisha uagizaji wa vifaa nje ya Nchi lengo likiwa kuwapunguzia wakandarasi gharama za uagizaji wa vifaa nje ya nchi, kuongeza mapato kwa serikali pamoja na kutoa Ajira kwa vijana.
Amewataka kutumia mkutano huo kufikia muafaka wa kutafuta njia ya kufikia malengo waliyojiwekea na kuwahakikishia kuwa serikali kupitia REA itawalipa wakandarasi fedha zao kwa wakati ili kuepuka visingizio vya kuchelewesha miradi.
Waziri Kalemani pia amewaonya watoa huduma kuacha kukwamisha miradi ya serikali kwa kuwacheleweshea vifaa wakandarasi na wakiendelea kufanya hivyo Sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.
” Rais wetu anafanya kazi kubwa kuwaletea maendeleo watanzania, tunamshukuru kwa kutupatia Bilioni 492 kwa ajili ya miradi hii, sasa ni jukumu letu kuhakikisha vijiji vyetu vyote vinawaka umeme, ” Amesema Dk Kalemani.