Home Mchanganyiko RAIS MAGUFULI AKATAA BIL.8/- KUTUMIKA KUFUNGA CCTV JENGO LA UHAMIAJI

RAIS MAGUFULI AKATAA BIL.8/- KUTUMIKA KUFUNGA CCTV JENGO LA UHAMIAJI

0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji, viongozi mbalimbali pamoja na wananchi katika eneo linapojengwa jengo la Makao Makuu ya Uhamiaji mjini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisikiliza maelezo ya ujenzi wa Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji jijini Dodoma.

PICHA NA IKULU

…………………

Na.Alex Sonna,Dodoma

RAIS Dk.John Magufuli amegomea Idara ya Uhamiaji kutumia kiasi cha Sh.Bilioni nane kuweka mfumo wa ulinzi ikiwemo kamera za CCTV kwenye jengo la Makao Makuu ya Idara hiyo linalojengwa jijini Dodoma na kuagiza kupitiwa upya gharama za ujenzi wa jengo hilo.

Agizo hilo amelitoa leo alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Makao Makuu ya Idara hiyo jijini Dodoma.

Amesema amekuwa akikubali maombi mbalimbali ya idara hiyo lakini suala la kutumia vifaa vya ‘security system’ Sh.Bilioni nane nakataa na kuwataka kununua milango watakayofungua wenyewe badala ya kujifungua.

“Sina wasiwasi na muundo wote unagharimu Sh.Bilioni 12 kwa kuwa ni jengo la ghorofa nane na ghorofa moja ya chini, pia kuna gharama za ukamilishaji Sh.Bilioni 2.7 hii pia ni sawa kwa kuwa ‘finishing’ inatumia gharama kubwa, lakini hizi Sh.Bilioni nane ni kwa ajili ya CCTV kamera na milango ya kujifungua nakataa, kweli jengo ni zuri lakini mmeweka vingine ni unnecessary,”amesema

Rais Magufuli ameongeza “Msiwafanye watu kwa kutamka CCTV kamera maana yake ni kitu cha ajabu sana, wapo watu wana CCTV kamera kwenye maeneo yao, nimewaambia mimi nilifunga wakati ule kwa milioni tatu, sasa hii CCTV kamera ya Sh.Bilioni nane ikoje najua mmetumia terms za kisayansi ili mtengeneze hela.”

Rais Magufuli amesema amegomea kipengele hicho na kuwataka kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama.

Ameagiza Kamishna wa idara hiyo na Wizara zinazohusika wakae na kupitia gharama walau zisifike Sh.Bilioni 20.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, amesema askari 34 wa idara hiyo wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kuwataka kufuata misingi ya uadilifu na bidii katika kazi.

Awali, Kamshina Jenerali wa Uhamiaji, Dk.Anna Makakala, amesema Rais alitoa Sh.Bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya Idara ya Uhamiaji Dodoma.

“Mheshimiwa Rais uliagiza kujengwa jengo zuri la kisasa linaloendana na hadhi ya uhamiaji,jengo hili litakuwa na hadhi ya kitaifa na kimataifa linatarajiwa kukamilika Novemba 27, mwaka 2020 na litakuwa la ghorofa nane na uwezo wa kuchukua watumishi 1200,”amesema.

Amesema mradi umefikia asilimia 20 na mkandarasi yupo eneo la mradi anaendelea na ujenzi.