Home Mchanganyiko WAZIRI WA KILIMO MHE JAPHET HASUNGA AZINDUA MSIMU WA KILIMO MWAKA 2019/2020

WAZIRI WA KILIMO MHE JAPHET HASUNGA AZINDUA MSIMU WA KILIMO MWAKA 2019/2020

0

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akichimba mashimo kwa ajili ya kupanda mahindi wakati akizindua msimu wa kilimo Kitaifa mwaka 2019/2020 leo tarehe 22 Novemba 2019 katika eneo la Vwawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa pamoja na wakulima wakisafisha shamba kwa ajili ya kupanda mahindi wakati akizindua msimu wa kilimo Kitaifa mwaka 2019/2020 leo tarehe 22 Novemba 2019 katika eneo la Vwawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa shambani wakati akizindua msimu wa kilimo Kitaifa mwaka 2019/2020 leo tarehe 22 Novemba 2019 katika eneo la Vwawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiondoka shambani akiwa pamoja na wakulima mara baada ya kumaliza kazi ya kupanda mahindi wakati akizindua msimu wa kilimo Kitaifa mwaka 2019/2020 leo tarehe 22 Novemba 2019 katika eneo la Vwawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.
 
Na Mathias Canal,
Wizara ya Kilimo-Songwe
 
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 22
Novemba 2019 amezindua msimu wa kilimo Kitaifa mwaka 2019/2020 ambapo amewataka
wakulima kote nchini kulima mazao ya chakula na biashara kwani serikali
inaendelea kuimarisha masoko ya mazao ndani na nje ya nchi.
 
Katika uzinduzi huo wa msimu wa kilimo uliofanyika
katika eneo la Vwawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe
amewahakikishia wakulima kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imeanzisha
kitengo cha masoko chini ya wizara ya Kilimo ambacho moja ya kipimo chake
kiutendaji ni kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ndani na nje ya nchi.
 
Alisema serikali imeweka msisitizo katika kuimarisha
mazao mbalimbali ya chakula, biashara pamoja na mazao ya mbogamboga na matunda
hivyo wakulima hawapaswi kuwa na wasiwasi na masoko ya mazao yao kwani
yataendelea kuimarika maradufu.
 
Mhe Hasunga ameitaka Mamlaka ya udhibiti wa Mbolea
Tanzania (TFRA) kuhakikisha kuwa inasimamia utekelezaji wa maagizo ya serikali
ya kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanauza mbolea kwa bei elekezi ili
kuwanufaisha wakulima kwani mbolea ni miongoni mwa Pembejeo muhimu kwa ajili ya
kuhakikisha kuwa wakulima wanalima mazao yenye tija.
 
Alisema kuwa mfanyabiashara yeyote atakayebainika
kuuza mbolea zaidi ya bei elekezi anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa
ni pamoja na kufutiwa leseni ya kufanya biashara hiyo.
 
Kuhusu Mbegu za mazao, Mhe Hasunga ameitaka Taasisi ya
Udhibiti wa mbegu nchini (TOSCI) kuhakikisha kuwa mbegu zinazopelekwa kwa
wakulima nchini zinakuwa katika ubora unaostahili huku akiagiza wauzaji wa
mbegu feki kuchukuliwa hatua.
 
“Vilevile naagiza Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kuhakikisha
kuwa wanazalisha mbegu za kutosha na kuzifikisha kwa wakulima kwa wakati ili katika
msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 kuwa na uzalishaji mkubwa na tija kwa
wakulima” Alisema
 
Kwa
upande wa Viuatilifu, Waziri Hasunga ameiagiza Taasisi ya Utafiti na Udhibiti
wa Viuatilifu ukanda wa Kitropiki (TPRI) kuhakikisha wanafanya ukaguzi nchi
nzima ili kubaini na kuondoa viuatilifu feki vyote sokoni.
 
Ameongeza
kuwa TFRA inapaswa kutoa elimu ya kutosha kwa wakulima kote nchini kuhusu
matumizi sahihi ya Viuatilifu ili kuondoa dhana ya wakulima kuwa na malalamiko
mengi kuhusu viuatilifu.
 
Aidha, Mhe Hasunga amesisitiza kuwa serikali inayoongozwa
na Dkt Magufuli haitawapangia bei ya mazao yao wakulima hususani mazao makuu ya
chakula na biashara kwani wakulima wanapokuwa wanalima mazao yao hakuna watu
wanaowasaidia hivyo wakati wa kuuza pia wanapaswa kuamua bei kulingana na soko.
 
Mhe Hasunga pia amewataka wakulima kujihusisha zaidi
na kilimo kinachozingatia hifadhi ya udongo (Climate Smart Agriculture) kwa kuchimba mashimo na kupanda mbegu
kuliko kilimo kinachoharibu udongo kilichozoeleka.