Wajumbe wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania ( ALAT) wakiangalia jengo la soko la kisasa la Magomeni inalojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 8.9.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Ndugu Aron Kagurumjuli, akiwa na wajumbe wa kamati ya ALAT Taifa , wakikagua Zahanati ya Mikoroshini iliyopo kata ya Msasani, katika ziara ya viongozi wa ALAT waliyokuwa wakikagua miradi ya Halmashauri hiyo jana.
Muonekano wa ndani wa soko la kisasa la Magomeni .
***************************************
Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania ( ALAT) imeipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwakutumia Local Fundi (Force Account).
Akizungumza na watendaji wa Halmashauri hiyo mara baada ya kukamilisha ziara ya kukagua miradi ya Halmashauri hiyo, Makamu Mwenyekiti wa ALAT , Stephano Mhapa amesema kuwa Mkurugenzi Mtendaji Aron Kagurumjuli na timu yake wamefanikisha kujenga miradi mikubwa ya maendeleo kwa kutumia mafundi wa kawaida jambo ambalo limeonyesha nizamu ya matumizi mazuri ya fedha za serikali.
Amefafanua kuwa mradi wa Zahanati ya Mikoroshini iliyopo Kata ya Msasani imejengwa kwa shilingi milioni 400.8 kwa kutumia mafundi wa kawaida wakati kwa mkandarasi wakutangaza tenda ingetumia milioni 700 na kwamba Halmashauri hiyo imeokoa kiasi cha shilingi milioni 300.
Aidha Mhapa amesema kuwa“ ukiangalia Zahanati hii imekamilika vizuri na imara , tumejionea wenyewe, Mkurugenzi na timu yako tunakupongeza sana, na halmashauri nyingine ziige mfano huu kutoka kwako, kazi ni kubwa uliyoifanya lakini gharama yake ni ndogo, haya ni matumizi mazuri ya fedha za serikali.”
Akizungumzia mradi wa Soko la kisasa la Magomeni, linalojengwa kwa shilingi zaidi ya bilioni 8.9 na Kituo cha Afya kilichopo Kigogo kinachojengwa kwa shilingi milioni 700 , Mhapa amesisitiza kuwa Halmashauri ya Kinondoni inapaswa kuigwa na Halmashauri nyingine kwa kazi kubwa wanayoifanya sambamba na kuwa na matumizi mazuri ya serikali.
“ Halmashauri ya Kinondoni tangu mwaka 2015 imekuwa ikipata hati safi na hiyo ni kutokana na kuwa na nidhamu ya matumizi mazuri ya fedha za serikali, hati safi inamanisha kwamba mnapokea pesa za serikali lakini pia mnakusanya mapato ya ndani na kuyatumia vizuri” ameongeza.
Kuhusu asilimia 10 ya fedha kwa ajili ya mikopo ya vijana , wakina mama na walemavu,ambayo ni bilioni tatu, Katibu wa ALAT Elirehema Kaaya ameipongeza Halmashauri kwakufanya vizuri kwani kiasi hicho cha fedha ni sawa na bajeti nzima ya Halmashauri nyingine.
Kaaya amesisistiza kuwa kazi anayoifanya Mkurugenzi Kagurumjuli ndio inayotakiwa na Rais Dk. John Magufuli na hivyo kuagiza Halmashauri nyingine ziige mfano wake.
“ Umefanya matumizi mazuri na sahihi ya fedha ambazo ni kodi za wananchi wanyonge, kilichofanyika na Mkurugenzi mtedaji wa Kinondoni ni kwamba , Mhe. Rais Magufuli na Waziri wa Tamisemi Suleman Jafo wanasisitiza kutumia local fundi (Force Account) ninashauri wakurugenzi wengine wasikilize maagizo yanatotolewa na serikali.” Amesisitiza Kaaya.
Awali akizungumza na viongozi wa ALAT, Mkurugenzi Mtendaji Kagurumjuli amesema kuwa Halmashauri imefanikiwa kupata bilioni 32.8 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa miradi mitatu ya kimkakati ambayo itaongeza mapato kwa kiasi kikubwa.
Kagurumjuli alitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzo wa soko la kisasa la Magomeni, wenye thamani ya shilingi bilioni 8.9, ujenzi wa soko la kisasa la Tandale wenye thamani ya shilingi bilioni 8.7 na uboreshaji wa fukwe ya Osterbay (Coco Beach) wenye gharama ya shilingi bilioni 13.