Home Biashara TBS IMEWAPATIA ELIMU WENYE VIWANDA VINAVYOZALISHA BIDHAA AMBAZO HAZIJATHIBITISHWA MKOANI SINGIDA 

TBS IMEWAPATIA ELIMU WENYE VIWANDA VINAVYOZALISHA BIDHAA AMBAZO HAZIJATHIBITISHWA MKOANI SINGIDA 

0

Baadhi ya vipodozi vyenye viambata sumu vilivyokamatwa katika ukaguzi huo uliofanyika Singida Manispaa Mkoani Singida .Ukaguzi huo umefanyika Mkalama,Shelui,Kiomboi,Manyoni na utaendelea Itigi.

*******************************

Na Neema Mtemvu, Singida

WENYE viwanda mkoani Singida, vinavyozalisha bidhaa ambazo hazijathibitishwa ubora wamepatiwa elimu kuhusiana na umuhimu wa bidhaa hizo kupata alama ya ubora na wameipokea kwa mwitikio mkubwa na wengine kuanza mchakato wa kutuma maombi ili kuthibitisha bidhaa zao.

Wafanyabiashara hao wenye viwanda mkoani humo, wameahidi kutumia elimu waliyoipata kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ili nao wajitokeze kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, hatua itakayoongeza kasi ya kuunga mkono juhudi za Serikali za ujenzi uchumi wa viwanda.

Elimu hiyo ilitolewa mkoani hapa kuanzia Novemba 11, mwaka huu na Maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na inatarajiwa kuhitimishwa Novemba 25, mwaka huu.

Elimu hiyo ilikwenda sambamba na ukaguzi wa kushtukiza kwenye maduka ya kuuza vipodozi na kufanikiwa kukamata vipodozi vyenye viambata sumu, ambavyo vimepigwa marufuku kutokana na kuwa na madhara kwa binadamu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Singida jana Mkaguzi wa Shirika hilo, Domisiano Rutahala alisema kwa muda wa siku 16 wamekuwa wakitoa elimu kuhusu umuhimu wa bidhaa zinazozalishwa kupata alama ya ubora kwa wenye viwanda vya kukamua mafuta ya alizeti na kuzalisha unga wa mahindi mkoani Singida.

“Maofisa wa shirika letu tupo hapa kwa ajili ya zoezi la kuwafikia wenye viwanda na wazalishaji ambao bidhaa zao hazijathibitishwa kupata elimu, kuwasikiliza na kuwasaidia kufikia viwango,” alisema Rutahala.

Aliongeza kwamba zoezi hilo limeanza kufanyika mkoani Singida. Alitaja maeneo ambayo elimu hiyo imetolewa kuwa ni Singida Manispaa, Kiomboi , Shelui,Mkalama na Manyoni

Zoezi hili litaendelea na halmashauri ya Itigi,” na kuongeza kuwa wenye viwanda hivyo walifurahi kufikiwa na elimu hiyo na wengine walianza mara moja kutuma maombi kwa ajili ya bidhaa zao kuthibitishwa na shirika hilo.

Kuhusu ukaguzi kwenye maduka ya vipodozi, Rutahala alisema walifanikiwa kukamata vipodozi vyenye viambata sumu ambavyo vimepigwa marufuku kutokana na kuwa na madhara kwa watumiaji.

Vipodozi hivyo vinaondolewa kwenye soko kutokana na kuwa na madhara mbalimbali kwa watumiaji.

Baadhi ya madhara ya vipodozi hivyo ni kusababisha saratani ya ngozi, kupunguza kinga ya ngozi na kuathiri mfumo wa homoni za mwili hivyo Rutalala, aliwashauri watumiaji kuacha kutumia vipodozi vilivyopigwa marufuku.

Wakati huo huo, shirika hilo limewataka wenye maduka ya chakula na vipodozi kujisajili kupitia mfumo unaopatikana kwenye tovuti ya shirika hilo, ili waweze kupatiwa vibali vinavyotakiwa kwa ajili ya kufanya biashara hizo.