**************************************
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Julius Mtatiro ahakikishe anaondoka na Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho hadi Tunduru ili wakahakiki ni kwa nini wakulima hawajalipwa.
“Nimefurahi kusikia minada ya korosho inakwenda vizuri. Lakini sijafurahia habari ya Tunduru. Mheshimiwa Rais aligiza sh. milioni 40 zipelekwe kwa wakulima. Na ninajua kwamba zimeshalipwa. Sasa ni kwa nini wakulima bado wanadai?, alihoji.
“Ukitoka hapa kwenye mkutano nenda pale jengo la Bodi ya Korosho. Ondoka na Mtendaji Mkuu wake, mwende Tunduru akafuatilie ni kwa nini malipo ya mwaka jana hayajalipwa hadi sasa.” Bw. Mtatiro ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru.
“Nataka afuatilie fedha zimekwama kwa nani. Kaimu Mkuu wa Mkoa ukigundua wanaokwamisha ni viongozi wa ushirika, shughulika nao hukohuko kama ambavyo umekuwa ukifanya,” amesisitiza.
Ametoa agizo hilo leo mchana wakati akifungua kongamano la siku moja la Wakandarasi na Wazabuni wa mikoa ya Kusini lilioandaliwa na benki ya CRBD kwenye ukumbi wa Benki Kuu (BoT) mjini Mtwara.
Akizungumzia kuhusu kongamano hili ambalo kaulimbiu yake ni “Pamoja nawe kukuza uchumi”, Waziri Mkuu amewataka wakandarasi hao baada ya kupata elimu kidogo kuhusu shughuli za benki hiyo, anataraji kuwa wataenda kwenye Halmashauri zao na kutafuta ……..
“Serikali inajenga miradi mikubwa kama vile bwawa la kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji la Mwalimu Nyerere, bomba la mafuta la kutoka Hoima hadi Tanga na miradi ya maendeleo kama ile ya barabara, reli, ujenzi wa hospitali, madarasa na nyumba za walimu. Miradi yote hii inawatarajia ninyi wakandarasi mkaijenge.”
Alisema Serikali imeendelea kuimarisha na kusogeza karibu kwa wananchi huduma za jamii ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu. “Katika kipindi cha Januari hadi Juni 2019, kwa shule za msingi, Serikali imejenga madarasa 473, matundu ya vyoo 1,405, nyumba za walimu 24 na kukamilisha maboma ya madarasa 2,760. Kwa shule za sekondari, Serikali ilijenga madarasa 465, matundu ya vyoo 736, nyumba za walimu 23 na kukamilisha maboma ya madarasa 2,392,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hii kutoa wito kwa viongozi na watendaji wazingatie utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa kutenga zabuni zenye thamani ya chini ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya wazabuni Watanzania ili kuwajengea uwezo na kushiriki katika zabuni. Alisema Serikali kwa upande wake itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa CRDB kwa kubuni programu hiyo ya tofauto ambayo imelenga kuwainua wakandarasi wadogo na wa kati.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki qa kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Gelasius Byakanwa alisema hadi sasa jumla ya tani 67,000 za korosho zimeuzwa mkoani humo kupitia minada mitatu.
Oktoba 30, mnada wa kwanza ulipofanyika bei ilikuwa sh. 2,468/- kwa kilo na mnada wa tarehe 15 Novemba, ulishihudia bei ikipanda na kufikia sh. 2,890/- kwa kilo, alisema.
Alisema katika msimu huu, korosho zimeingiza sh. Bilioni 1.75 ambapo kati ya hizo, sh. Bilioni 1.20 zimeshaingizwa kwenye akaunti na kupelekwa kwa wakulima.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa benki ya CRDB, Bw. Abdulmajjid Nsekela alisema bei hiyo inamsaidia mteja kwa kutoa ushauri, kumwezesha na kushirikiana naye kuijenga nchi.
“Leo tuko Mtwara, lakini tumeshaendesha makongamano kama haya katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza. Na hapa Mtwara tumejumuisha pia mikoa ya Lindi na Ruvuma,” alisema.
Alisema benki hiyo ina hisa trilioni 6.3 ambazo ni sawa na asilimia 20 ya hisa za mabenki yote na kwa upande wa amana, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema amana za benki hiyo zinafikia trilioni 4.9 ambazo ni sawa na asilimia 23 ya amana za benki zote nchini.