Home Mchanganyiko TRA YAFAFANUA MABADILIKO YA SHERIA KWENYE VIWANGO VYA KODI

TRA YAFAFANUA MABADILIKO YA SHERIA KWENYE VIWANGO VYA KODI

0

Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Rahabu Kibona (kulia) akichukua maelezo ya Mlipakodi kwa ajili ya maandalizi ya kusajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN) wakati wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi Wilayani hapo.

 

Afisa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Emmanuel Msambwa (kulia) akimuelimisha Mfanyabiashara wa duka la nguo wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wakati wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi Wilayani hapo.

Afisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Ernesta Shirima (kushoto) akiwaelimisha Vijana wa Bodaboda wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro kuhusu umuhimu wa kuhamisha kadi za vyombo vya moto wakati wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi Wilayani hapo.

*********************************

Na Veronica Kazimoto

Mvomero

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa ufafanuzi wa mabadiliko ya
viwango vya kodi kama vilivyoainishwa na Sheria ya Fedha ya mwaka
2019 ambapo mabadiliko hayo yamegusa Sheria za Kodi ya Mapato,
Ongezeko la Thamani (VAT), Usajili wa Vyombo vya Moto pamoja na
Usalama Barabarani.

Akizungumza wakati wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani
Morogoro katika Wilaya ya Mvomero, Afisa Msimamizi wa Kodi Mkuu wa
TRA, Julius Mjenga amesema kuwa, mabadiliko katika sheria ya kodi ya
mapato, jedwali la viwango vya kodi kwa wafanyabiashara wadogo wakazi,
vimepunguzwa kutoka sh. 150,000 hadi kufikia sh. 100,000, kwa wale
wenye mzunguko wa mauzo yanayozidi sh. milioni nne hadi milioni 7 kwa
mwaka.

“Kwa wafanyabiashara wenye mauzo kati ya sh. milioni saba hadi sh.
milioni 11, viwango vya kodi vimepunguzwa hadi kufikia sh. 250,000 kutoka
sh. 318,000 iliyokuwepo hapo awali,” alisema Mjenga.

Pia, kwa wafanyabiashara wenye mauzo kati ya sh. milioni 11 hadi sh.
milioni 14, viwango vya kodi vimepunguzwa hadi kufikia sh. 450,000 kutoka
sh. 546,000.

“Lengo la kupunguza viwango hivi ni kukuza ridhaa ya kulipa kodi kwa hiari
na kuongeza Mapato ya Serikali,” alifafanua Mjenga.

Kwa upande wa sheria ya usajili na uhamishaji wa umiliki wa vyombo ya
moto, Mjenga ameeleza kuwa, ada ya kupata nakala ya kadi ya gari ni sh.
50,000, pikipiki ya magurudumu matatu (bajaji) sh.30,000 na pikipiki ni sh.
20,000 badala ya sh. 10,000 iliyokuwa ikitozwa kwa vyombo vya aina hiyo
kabla ya tarehe 1 Julai, 2019.

Aidha, akizungumzia juu ya mabadiliko ya viwango vya leseni za udereva
chini ya sheria ya usalama barabarani, Mjenga amesema kuwa, leseni ya
udereva inalipiwa sh. 70,000 kila baada ya miaka mitano ambapo kabla ya
mabadiliko ilikuwa inalipiwa sh. 40,000 kila baada ya miaka mitatu.

“Mabadiliko haya kwa ujumla wake yamelenga kuongeza fursa kwa
walipakodi na wananchi kwa ujumla kuongeza ufanisi katika biashara zao
na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali. Hivyo, natoa rai kwa walipakodi
wote kutumia fursa hii adhimu kwa maendeleo ya taifa letu,” alieleza
Mjenga.

Wiki ya elimu kwa mlipakodi katika Mikoa ya Morogoro na Pwani
itamalizika tarehe 17 Novemba, 2019 ambapo shughuli zinazofanyika ni
pamoja na usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), kupokea
mrejesho, kusikiliza kero na kujibu maswali yanayoulizwa na
wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa ujumla.